Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kunufaika na madini ya kimkakati duniani

Muktasari:

  • Rais Samia uwepo wa madini ya kimkakati kidunia nchini kunayatamanisha mataifa makubwa kuaingalia Tanzania kwa malengo ya kuja kuwekeza.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefichua kuwa uwepo wa madini ya kimkakati ya kidunia nchini, ikiwemo aina ya Kinywe unatamanisha wawekezaji kutoka mataifa makubwa kuja kuwekeza katika sekta hiyo.

 Hayo amebainisha leo Aprili 17,2023 alipokuwa mgeni rasmi kwenye  utiaji saini wa mikataba ya makubaliano  kati ya Serikali na Kampuni tatu za uchimbaji madini kutoka Perth nchini Australia na Uingereza, hafla hiyo ilifanyika Ikulu Chamwino, Dodoma.

Rais Samia amesema hata katika ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Hariris walizungumzia madini ya kinywe, mradi wa Nikel pamoja na kiwanda cha usafishaji madini kinachotarajiwa kujengwa Kahama.

“Madini haya yanakuza jina la Tanzania duniani na hata nchi zenye nguvu duniani zinaangalia Tanzania, katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu katika usafirishaji wa madini haya hivyo itachochea uwekezaji,”amesema

Rais Samia amesema madini hayo adimu na ya kimkakati kwa dunia kwa sasa yanatafutwa kwani yanahitajika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Yanatumika kutengenezea betri za magari ya umeme, vifaa vya kieletroniki na mitambo mbalimbali Tanzania tumejaliwa kuwa na madini haya na inafanya nchi kuangaliwa zaidi na wawekezaji wakubwa duniani,”amesema

Amesema mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini ya kinywe lakini pia kukaa katika jiografia nzuri ya kuzungukwa na nchi nane ambazo baadhi zina madini hayo kunaifanya Tanzania kuwa katika nafasi nzuri kifursa.

“Kwakuwa tutakuwa na viwanda vya kuchakata madini hapa lakini pia tuna njia za kuaminika katika kusafirisha madini hayo fursa zote hizo zitaifidisha Tanzania,”amesema

Rais Samia amesema pamoja na kuwa na fursa hizo nchini kazi waliyonayo ni kuchagua ni yupi wa kushirikiana naye katika kuvuna madini hayo kwa maslahi mapana ya Taifa.

Sekta ya madini imekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia Pato la Taifa, ambapo kwasasa sekta hiyo inachangia asilimia 9.7.