Tanzania, Msumbiji kuchochea mabadiliko uchumi wa kikanda
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo wakati wakitembelea mabanda ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Julai 3, 2026. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Tanzania na Msumbiji zina nafasi ya kipekee ya kuongoza mabadiliko ya kiuchumi kati ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na rasilimali walizonazo, idadi kubwa ya vijana na nafasi yao katika biashara ya kikanda
Dar es Salaam. Tanzania na Msumbiji zina nafasi ya kipekee katika kuongoza mabadiliko ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na wingi wa rasilimali walizonazo pamoja na wingi wa idadi kubwa ya vijana.
Wito huo umetolewa leo Julai 3, 2026 na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo ya ufunguzi, Chapo ameambatana na mwenyeji wake, Rais Samia na kutoa tuzo kwa washiriki bora wa maonyesho hayo huku wakihutubia mamia ya wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Chapo ametoa wito kwa nchi za Afrika kuharakisha ujumuishaji wa masoko, kuwekeza katika miundombinu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kujenga uhuru wa kiuchumi wa bara hilo.
Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania na Msumbiji zina nafasi ya kipekee ya kuongoza mabadiliko ya kiuchumi kati ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kutokana na rasilimali walizonazo, idadi kubwa ya vijana na nafasi yao katika biashara ya kikanda.
Amesema ushirikiano wa nchi hizo mbili unapaswa kujengwa juu ya msingi wa kuongeza biashara, uwekezaji na uzalishaji badala ya ushindani usio na tija.
“Tuna kila sababu ya kujenga ramani mpya ya maendeleo ya uchumi kati ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kusini,” amesema.
Chapo amesema kwa zaidi ya miaka 50, Maonyesho ya Sabasaba yamekuwa yakileta pamoja wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni jukwaa muhimu la kukuza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Amesema utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) unatoa fursa ya kihistoria ya kuunganisha masoko ya bara hilo lakini mafanikio yake yatategemea uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, nishati na mifumo ya kidijitali.
“Nchi za Afrika zinapaswa pia kuunganisha maeneo ya uzalishaji ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma, mitaji na watu, hatua ambayo itasaidia kuongeza ushindani wa uchumi wa bara hilo katika soko la dunia,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi mgeni wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo katika maonesho ya 50 ya Sabasaba katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia sekta ya usafirishaji, amesema bandari za Tanzania na Msumbiji hazipaswi kuonekana kama washindani bali kama mtandao mmoja wa vifaa na usafirishaji unaokamilishana kwa lengo la kupunguza gharama za biashara, kuimarisha minyororo ya usambazaji na kuongeza ushindani wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Amesema Bahari ya Hindi inapaswa kuwa kitovu cha maendeleo, ubunifu na ustawi wa Afrika kupitia matumizi bora ya bandari, korido za maendeleo na maeneo maalumu ya kiuchumi.
Chapo amewataka wafanyabiashara wa Afrika kutumia fursa zilizopo katika sekta za nishati, kilimo, uchakataji wa mazao, madini, utalii, usafirishaji, viwanda vya kuongeza thamani, uchumi wa kidijitali na maendeleo ya miundombinu.
Ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wawekezaji kuwa Msumbiji iko tayari kujenga ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia kuaminiana, manufaa ya pamoja na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.
Samia ahimiza ubunifu
Kwa upande wake, Rais Samia amesema katika kipindi cha miaka 50, maonyesho hayo yamekuwa daraja la kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi pamoja na kuinganisha Tanzania na dunia. Kupitia maonyesho haya, wabunifu walioanza kama wadogo sasa wamekuwa wakubwa.
“Maonyesho haya ni jukwaa muhimu la biashara na pia ni ishara kuwa Tanzania inaendelea kuaminika kama kituo kikuu cha uwekezaji na biashara na lango la kufikia masoko ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), bara la Afrika na duniani kote.
“Hii inadhihirika na ndugu zetu kutoka China, akina Cathy (Wang), wao ni coordinator (waratibu) wa maonyesho haya kule China lakini wana biashara kubwa ya logistics, wamejeenga pale Ubungo ambayo inafanya biashara zivuke kwenda kote duniani,”amesema.
Amewapongeza washiriki na waandaaji wa maonyesho hayo kwa maboresho waliyoyafanya hasa katika miundombinu. Amewataka kuwa wabunifu ili kuyakuza maonyesho hayo katika viwango vikubwa zaidi za kimataifa.
Rais Samia amesema amefurahi kuona wale aliokuwa nao tangu akiwa ofisa kwenye maonyesho hayo, wapo mpaka sasa akiwamo Mama Anna Mkapa ambaye leo ameshiriki kwenye maonyesho hayo akiwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).
Jukwaa linalounganisha
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema maonyesho hayo ya si tukio la kawaida la kalenda ya biashara, bali ni jukwaa linalounganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji, wanunuzi na wabunifu kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.
Amesema kupitia maonyesho hayo, bidhaa za Tanzania zinapata fursa ya kufikia masoko mapya, teknolojia mpya zinawafikia wazalishaji na sekta binafsi inapata nafasi ya kujenga ushirikiano unaozalisha ajira, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kusisitiza uchumi unaotegemea uzalishaji wa viwanda na biashara yenye ushindani, maonyesho haya yanakuwa daraja muhimu la kuwawezesha wazalishaji wetu kutambua mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Sabasaba si mahali pa kuonyesha bidhaa pekee, bali ni sehemu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu, kufanya majadiliano ya kibiashara na kufungua mikataba mipya ya uwekezaji na biashara,” amesema.
Amesema maonyesho hayo yanaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi shindani unaoongozwa na sekta binafsi.
“Ni kupitia majukwaa kama haya ndipo tunawapa nguvu wajasiriamali wadogo na wa kati, viwanda vya ndani na wabunifu wetu ili washindane katika soko la kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na katika masoko ya kimataifa,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kila mwekezaji na kila mzalishaji aweze kutumia fursa zinazotokana na maonyesho haya.
Miaka 50 ya Sabasaba
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan-Trade), Dk Latifa Khamis amesema katika miaka 50 ya Sabasaba imezalisha fursa ya Sh129.2 trilioni. Amesema hiyo ni ishara kuwa Sabasaba inaakisi mchango mkubwa wa maonyesho hayo katika kukuza biashara, uwekezaji na viwanda nchini.
“Katika kipindi cha nusu karne, maonyesho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, kukuza bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji,” amesema.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yamekwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 huku yakionesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya biashara.
“Kipindi cha miaka 50, jumla ya watu milioni 10.78 wametembelea maonyesho haya huku zaidi ya kampuni 38,056 zikiwa zimeshiriki maonyesho haya na yamechangia kuzalishwa kwa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja,” amesema.
Amesema Tan-Trade inaendelea kuhamasisha matumizi ya Tanzania Brand ili kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini katika masoko ya ndani na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji na Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Sharif Ali Sharif amesema Maonyesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji, wazalishaji na watumiaji wa bidhaa na huduma kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Amesema kupitia maonyesho hayo, Zanzibar imeendelea kupata fursa ya kutangaza vivutio vya uwekezaji, bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuimarisha uhusiano na washirika mbalimbali wa maendeleo.
“SMZ inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi,” amesema.
Chachu ya uwekezaji
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Biashara na Uwekezaji cha Afrika Mashariki (EACLC), Cathy Wang amesema maonyesho ya biashara yamekuwa chachu ya kuongeza kwa uwekezaji nchini kwani baadhi ya wawekezaji wameanzisha viwanda vyao Tanzania.
“Natoa pongezi kwa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Tan-Trade kwa maandalizi ya maonyesho ya kwani yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza uchumi na uwekezaji nchini Tanzania.”
Ametoa shukrani zake kwa Rais Samia kwa uongozi wake wenye maono na kuweka mazingira wezeshi yanayochochea uwekezaji nchini Tanzania. Pia, amemkaribisha Rais wa Msumbiji, Chapo kwa kushiriki katika maonyesho hayo.
“Uwepo wako (Chapo) ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi na kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Msumbiji,” amesema Wang.