Tanzania yamvutia mwekezaji, kujenga kiwanda cha bidhaa migodini
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kulia) akiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oriental Casting and Forging Ltd.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Serikali, kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa katika eneo la Buzwagi Special Economic Zone wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Dar es Salaam. Serikali imeendelea na mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa zinazotumika katika sekta ya madini barani Afrika ili kupunguza utegemezi kutoka nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada Serikali kuanza mazungumzo na kampuni ya China ya Oriental Casting and Forging Ltd kuhusu uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha goroli za chuma zinazotumika kusaga miamba katika migodi.
Kwa mujibu wa Serikali, kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa katika eneo la Buzwagi Special Economic Zone wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
Eneo hilo limetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha bidhaa na vifaa vinavyotumika katika uchimbaji madini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewaambia wanahabari leo Jumanne Juni 30,2026 kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa bidhaa za migodini.
“Hatua hii itapunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje ya nchi na kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini,” amesema Mavunde.
Amesema Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazohitajika kwenye migodi, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza teknolojia na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usambazaji wa bidhaa hizo katika ukanda wa Afrika.
“Lengo letu ni kuona wachimbaji wakubwa na wadogo wanapata bidhaa zinazotumika kwenye uzalishaji wa madini hapa nchini bila kulazimika kuziagiza kutoka nje. Hii itapunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa sekta ya madini,” amesema Mavunde.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oriental Casting and Forging Ltd, amesema wapo tayari kufanya uwekezaji mkubwa wa bidhaa za migodini Tanzania kwa sababu ni Taifa ambalo lina mazingira mazuri ya uwekezaji.
“Sekta ya madini inakua kwa kasi kubwa hivyo ni sehemu salama na rafiki ya kufanya uwekezaji utakaokuwa suluhisho la upatikanaji wa bidhaa za migodini kwa urahisi zaidi,” amesema Songcun.