TIOB, DSE kuboresha mitaala elimu ya kifedha

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB) , Patrick Mususa (katikati) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam ( DSE) wakisaini hati ya makubaliono
Muktasari:
- Ushirikiano unalenga kukuza ujuzi wa kifedha, soko la mitaji, na uwekezaji, huku ukihimiza ubunifu na maendeleo ya uchumi nchini.
Dar es Salaam. Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB) kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), wameingia makubaliano ya kuboresha mitaala ya elimu ya kifedha ili kutoa mafunzo kwa sekta za kibenki, taasisi za kifedha, jamii na wafanyabiashara.
Makubaliano hayo yameingiwa leo, Jumanne, Januari 21, 2025, kwenye hafla ya utiaji saini wa hati ya ushirikiano wa taasisi hiyo na DSE, katika makao makuu ya soko hilo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIOB, Patrick Mususa, amesema ushirikiano katika safari hiyo ya pamoja kati yao na DSE unahusisha uboreshaji wa mitaala iliyopo ili kutoa mafunzo kwa sekta ya kibenki.
“Elimu ya masuala ya mitaji na jinsi ya kuzalisha mitaji na kuwekeza inapaswa kuingizwa kwenye mtaala. Elimu hii itawafikia watoa huduma katika benki na taasisi mbalimbali za kifedha na hata kuwafikia wale waliopo kwenye jamii kama makundi maalumu na wafanyabiashara,” ameeleza.
Amesema kupitia ushirikiano huo, elimu na mafunzo mbalimbali yataratibiwa huku vyanzo mbalimbali vya ubunifu vikichagizwa katika kuleta huduma mpya kwenye sekta ya kifedha.
“Elimu hii itatolewa kwa benki, watendaji wanaounga mkono na kuhimili vifungu vya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na mawakala wa soko la hisa, na wale wanaoanzisha na kuibua bidhaa zinazozalisha mitaji. Serikali na kampuni binafsi zinazoleta hisa sokoni pia zitahimizwa kuzalisha mitaji na kuhimili soko kwa ujumla kwa manufaa ya kiuchumi,” amesema.
Kadhalika, Mususa amesema kipaumbele kingine cha ushirikiano huo ni kuhakikisha ukuaji wa sekta ya fedha na masoko ya mitaji ili kukuza uchumi wa nchi.
“Tangu mwaka 1993, kipaumbele cha taasisi hiyo na soko la hisa ni kukuza soko la mitaji, japo kuwa kipindi hicho kulikuwa na uhaba wa mabenki na vyanzo hafifu vya mitaji, kutokana na historia ya miamala ya kipindi hicho kuwa midogo,” amesema.
Mususa ametambua juhudi za DSE katika kujenga masoko ya mitaji kwa upande wa hati fungani na hisa kwa takriban miaka saba na kusema kuwa kwa kipindi chote hicho soko hilo limefanikiwa.
“Soko hili limeibua hati fungani mbalimbali za mabenki na za serikali na kuwezesha miradi mipya ya maji kama Mto Tanga, pamoja na kuunga mkono miradi ya kikandarasi ya miundombinu. Mashirikiano haya yanatupa matumaini makubwa, na tupo tayari kushirikiana na soko hili,” amesema.
Aidha, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesema ushirikiano huo umelenga kuimarisha ujuzi wa kifedha, kukuza ubora wa kitaalamu na kuendeleza ukuaji wa soko.
“Kwa kufanya kazi pamoja, tutahakikisha kwamba watu binafsi, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla wanaelewa jukumu muhimu la masoko ya fedha na benki katika kuunda utajiri na kuwezesha maendeleo ya kiuchumi,” amesema.
Kadhalika, Nalitolela amesema TIOB ina urithi wa kuunda wataalamu wenye ujuzi wa benki, huku DSE ikikamilisha hilo kwa kuwapa wadau maarifa kuhusu masoko ya mitaji na mikakati ya uwekezaji.
“Tunapoimarisha ushirikiano, tunaweka msingi wa ushiriki mkubwa zaidi katika masoko ya fedha, kukuza uwekezaji na kuendeleza maendeleo endelevu ya kiuchumi,” amesema.