Tozo mpya ya bandari kuanza leo
Muktasari:
- Lengo la kuanzishwa kwa tozo hizo ni kupata fedha za kuboresha zaidi miundombinu ya bandari zake ili iendane na mahitaji ya sasa.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeeleza, tozo mpya ya Ada ya Uendelezaji wa Miundombinuya Bandari (PID) iliyositishwa miezi miwili iliyopita itaanza kutozwa kuanzia leo Jumatano, Julai 1, 2026.
Tozo hiyo awali ilipangwa kuwa asilimia tisa ya kodi ya forodha, sasa imepunguzwa hadi asilimia 4.5 ya kodi kwa mizigo yote ya ndani itakayoagizwa kupitia bandari za bahari kuu na asilimia 1.5 kwa ajili ya malighafi ya viwandani na mizigo yote isiyotozwa ushuru wa forodha.
Ada hizo zilizokuwa zianze kutumika Machi 2026 zilikuwa asilimia tisa na kukaibuka ukakasi miongoni mwa wanaopaswa kuzilipa, ambapo TPA ilitangaza kuzisitisha hadi Julai 1, 2026 ili kupata fursa ya kupokea tena maoni ya wadau mbalimbali.
Taarifa kwa umma ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa aliyoitoa leo Jumatano, Julai 1, 2026 imeeleza:’’Ada ya PID itatozwa kwa mizigo yote ya ndani itakayoingizwa kwa kupitia bandari za bahari kuu, isipokuwa mizigo ya kimiminika (Liquid Bulk Cargo).’’
Mbossa amesema ada hiyo imegawanyika katika makundi mawili. Mosi, asilimia 4.5 ya kodi kwa mizigo yote ya ndani itakayoagizwa kupitia bandari za bahari kuu. Pili, asilimia 1.5 kwa ajili ya malighafi ya viwandani na mizigo yote isiyotozwa ushuru wa forodha.
Katika taarifa hiyo, Mbossa amewashukuru wadau wote kwa ushirikiano wao endelevu huku akisisitiza kuwa, “ada hii inalenga kuimarisha miundombinu na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika bandari za bahari kuu nchini.’’
Hivi karibuni wadau wa bandari wakizungumza jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti juu ya kuanza kwa tozo hiyo mpya walisema itasaidia kuendeleza miundombinu ya bandari ili ziweze kuendana na mahitaji ya sasa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange alisema lengo la tozo hiyo ni kusaidia ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya bandari nchini ili ziweze kuhimili ongezeko kubwa la shehena na ushindani wa kikanda.
“Awali tozo ilikuwa asilimia tisa lakini baada ya majadiliano ikashushwa hadi asilimia 4.5. Hii siyo kwa ajili ya Bandari ya Dar es Salaam pekee bali bandari zote nchini. Lengo ni kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki na ya kisasa,” alisema.
Alisema pamoja na kuwepo kwa wawekezaji wanaoendesha baadhi ya huduma bandarini, jukumu la kuboresha miundombinu bado lipo chini ya TPA.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena Tanzania (TSC), Clement Kamendu alisema sekta ya bandari haiwezi kuendelea bila uwekezaji mkubwa wa miundombinu.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mawakala wa Meli Tanzania (Tasaa), Abel Uronu alisema maendeleo ya sekta ya usafirishaji duniani yamebadilisha aina ya meli zinazotumika, jambo linalolazimisha bandari nazo kubadilika.
“Zamani kulikuwa na meli zinazobeba kila kitu, lakini sasa kuna meli maalumu za makontena, magari na mizigo mingine maalumu. Huwezi kuleta meli ya kisasa kwenye bandari isiyo na uwezo wa kuihudumia,” alisema.
Alisema mamlaka nyingi za bandari duniani zimekuwa zikiwekeza kwenye mifumo ya kisasa na teknolojia ili kuendana na kasi ya biashara ya kimataifa.
“Kuna bandari sasa kila kitu kinafanyika kidijitali na watu wachache sana wanahitajika. Hivyo nasi lazima twende na wakati,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS), Ephraim Mwankusye alisema hatua hiyo itazifanya bandari za kisasa na zenye uwezo wa kuhudumia mizigo mingi kwa haraka zaidi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda.
Mwankusye alisema wadau wa sekta hiyo wanaunga mkono utekelezaji wa PID kwa kuwa utaleta mageuzi makubwa katika huduma za bandari nchini.
Kwa nini tozo hizo?
Wakati wadau wakiyasema hayo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha alisema sababu za kuanzishwa kwa tozo hizo lengo ni kupata fedha za kuboresha zaidi miundombinu ya bandari zake ili iendane na mahitaji ya sasa na kuondoa msongamano bandarini na wa malori kwenye maeneo kadhaa ya Dar es Salaam.
Dk Fasha alisema hatua hiyo inatokana na ongezeko la shehena linalotokana na juhudi za maboresho yaliyofanyika katika bandari za Dar es Salaam na Tanga zilizovutia watumiaji wa ndani na nje ya nchi.
Dk Fasha alisema mapato yatakayokusanywa kupitia ada hiyo yatawezesha TPA kugharamia miradi 13 ya kimkakati inayolenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya bandari ndani ya miaka mitano ijayo.
“Iwapo TPA itaendelea na mfumo wa sasa wa kukusanya fedha kidogo kidogo bila ada maalumu, inaweza kuchukua kati ya miaka mitano hadi 10 kutekeleza mradi mmoja tu kati ya miradi tuliyopanga,” alisema.
Kwa mujibu wa TPA, shehena inayopita bandarini inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 32.8 mwaka 2024/25 hadi tani milioni 62 ifikapo mwaka 2030/31.
Dk Fasha alisema ongezeko hilo linaonyesha umuhimu wa kuwekeza mapema katika bandari ili kuepuka msongamano wa mizigo na ucheleweshaji wa huduma.
Akifafanua ukubwa wa ongezeko hilo, alisema tani milioni 32.8 zinazohudumiwa sasa zingehitaji zaidi ya malori milioni 1.3 kama zingesafirishwa kwa wakati mmoja, huku tani milioni 62 zikihitaji takribani malori milioni 2.48.
“Hii inaonyesha ukubwa wa fursa na changamoto iliyopo mbele yetu. Tusipochukua hatua sasa, bandari zinaweza kuwa kikwazo cha biashara na maendeleo badala ya kuwa kichocheo cha uchumi,” alisema.