Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TPDC kuanza utafiti wa gesi, mafuta kwa teknolojia ya kisasa

Muktasari:

  • TPDC imezindua mradi wa kisasa wa kuchukua taarifa za mitetemo katika kitalu cha Lindi na Mtwara ili kubaini akiba ya mafuta na gesi.

Lindi. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza rasmi mpango wa utekelezaji wa mradi wa uchukuaji wa taarifa za mitetemo (3D Seismic Data Acquisition) katika kitalu cha Lindi na Mtwara, hatua inayolenga kubaini ukubwa wa akiba ya mafuta na gesi asilia katika maeneo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Julai 16, 2025, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Meneja wa mradi huo, Dk Shaibu Nuru amesema teknolojia hiyo ya kisasa inalenga kuongeza maarifa ya kina kuhusu uwepo wa mafuta na gesi ardhini.

“Mradi huu ni wa miezi 18 na unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi huu Julai. Tutasitisha wakati wa msimu wa mvua kubwa na kuendelea mara mvua zitakapomalizika,” amesema Dk Nuru.

Mtambo wa utafiti wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Lindi na Mtwara, ambapo kwa mkoa wa Lindi utafiti huo utafanyika Halmashauri ya Mtama. Picha na Bahati Mwatesa

Amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuleta fursa mbalimbali kwa wananchi wa Lindi na Mtwara, ikiwemo ajira na kuchochea mzunguko wa biashara katika maeneo husika.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi wakati wa utekelezaji wa mradi huo, hasa katika maeneo ambayo shughuli zitafanyika.

“Tukianza mradi lazima tushirikishe viongozi wa dini, serikali na wananchi kwa ujumla ili kufanikisha lengo la mradi huu ambao una faida kubwa kwa Taifa,” amesema Dk Nuru.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amesema serikali iko tayari kushirikiana na TPDC kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio.

“Mradi huu unatarajiwa kufanyika katika vijiji nane vya Halmashauri ya Mtama. Niwaombe TPDC wahakikishe wanawashirikisha viongozi wa serikali, wazee maarufu na watendaji wa vijiji wakati wanatekeleza shughuli zao,” amesema DC Mwanziva.

Katika hatua nyingine, TPDC imewahusisha pia wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Lindi kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huu unatajwa kuwa ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini, huku matarajio yakiwa ni kuongeza rasilimali za taifa na kukuza uchumi wa mikoa ya kusini.