TRA Kilimanjaro kukusanya Sh32 bilioni Desemba pekee
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala.
Moshi. Ikiwa zimesalia siku 19 kabla ya kuingia mwaka 2026, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imejipanga kukusanya zaidi ya Sh32 bilioni kwa kipindi cha Desemba 2025 ili kufikia lengo la mapato ya mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Desemba 12, 2025 na Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala wakati akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani humo.
Jilala amesema katika makusanyo hayo, wanategemea kukusanya Sh12.485 bilioni, fedha zinazotokana na kodi za ndani na Sh20.9 bilioni fedha zinazotokana na mapato ya forodha.
Aidha, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kuwa nchi inapata mapato ya kutosha katika kuelekea mwaka mpya.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoani humo.
“Tunaelekea mwisho wa mwaka na leo tumekutana na viongozi wa jumuiya za wafanyabiashara Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kuweka mikakati ya namna ya kufikia lengo la makusanyo katika kipindi hiki cha Desemba.
Amesema: “Katika kipindi hiki cha Desemba, tumepanga kukusanya Sh12.485 bilioni kwa kodi za ndani na kwa kodi za mipikani (forodha), tunatakiwa kukusanya Sh20.9 bilioni ukizingatia kwamba Desemba ina mambo mengi.”
Aidha, amesema kwa vipindi vilivyopita wamekusanya kodi za ndani na forodha kwa zaidi ya asilimia 110 ya makusanyo.
“Kama mkoa tunakwenda vizuri, Desemba hii tumeongea na wafanyabiashara watimize wajibu wao maana ili nchi ijitegemee inahitaji kodi, kwa sababu asilimia kubwa ya pato la serikali inatokana na kodi,” amesema Jilala.
Amesema: “Wiki ijayo tutakutana na wenye kumbi za starehe kuelekezana taratibu na kukubaliana namna nzuri ya usimamizi wa mashine za EFD lakini pia ‘Chagga migration’, watu watajaa, kutakuwa na foleni Kilimanjaro, kumbi za starehe zitajaa, kwa hiyo usimamizi wa EFD unahitajika kwa kiasi kikubwa.”
Pamoja na mambo mengine, amesema TRA itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuwahamasisha kulipa kodi kwa hiari, hivyo kuboresha huduma na maendeleo ya taifa.
“Nisisitize pia wafanyabiashara kutoa risiti na wanunuzi kudai risiti kila wanapofanya ununuzi ili kuepuka mkono wa sheria,” amesema Jilala.
Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara wa mkoa huo, Jenes Tairo amesema suala la ulipaji kodi ni la kila mmoja, hivyo akawataka baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waadilifu kulipa kodi kwa wakati.
“Tukilipa kodi kwa wakati na bila ubabaishaji tutaisaidia nchi yetu kutekeleza mipango yake kwa wakati na kwa ufanisi, lakini tukifanya biashara kwa njia za magendo tunaikoseshea serikali yetu mapato,” amesema mfanyabiashara huyo.