Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufadhili wa maendeleo utakavyobeba utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050

Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Deogratius Kwiyukwa.

Muktasari:

  • Dira 2050 inalenga kuijenga Tanzania kuwa na uchumi mkubwa zaidi, wenye tija na ushindani. Hata hivyo, mafanikio ya azma hiyo yatahitaji mitaji ya muda mrefu, ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na taasisi za kifedha zinazoweza kufadhili miradi ya maendeleo.

Dar es Salaam. Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hautategemea sera nzuri pekee, bali pia uwekezaji wa muda mrefu, maandalizi ya miradi yenye ubora na taasisi zenye uwezo wa kutafsiri malengo ya taifa kuwa matokeo yanayoonekana.

Dira hiyo inalenga kuijenga Tanzania kuwa na uchumi mkubwa zaidi, wenye tija na ushindani. Ili kufikia azma hiyo, kutahitajika fedha za muda mrefu, ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na taasisi za kifedha zinazoweza kufadhili miradi ya maendeleo.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Benki ya Maendeleo ya TIB, ambayo pamoja na kutoa mikopo, ina jukumu la kuwezesha uwekezaji unaochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Deogratius Kwiyukwa, akizungumza leo Julai 13, 2026 jijini Dar es Salaam, amesema maendeleo ya muda mrefu yanahitaji taasisi zenye uwezo wa kuandaa na kusimamia miradi kuanzia hatua ya wazo hadi utekelezaji.

"Dira 2050 ni mjadala muhimu kwa taifa kwa sababu unatukumbusha kuwa maendeleo yanahitaji mipango, fedha na utekelezaji wenye mtazamo wa muda mrefu. Jukumu letu ni kusaidia uwekezaji unaozalisha matokeo katika sekta za uzalishaji, huduma za umma na kwa jamii," amesema Kwiyukwa.

Amesema tofauti na mikopo ya benki za biashara, ufadhili wa maendeleo hulenga miradi inayohitaji mtaji mkubwa, maandalizi ya kina na muda mrefu wa kurejesha fedha.

Miradi hiyo ni pamoja na miundombinu, nishati, umwagiliaji, viwanda, maji, huduma za usafirishaji na ugavi, ambazo ni muhimu katika mageuzi ya uchumi.

Kwa zaidi ya miaka 50, TIB imefadhili miradi katika sekta za miundombinu, kilimo, viwanda, nishati, maji, utalii, elimu, afya na maendeleo ya biashara, ambazo zinaendelea kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kadiri utekelezaji wa Dira 2050 unavyoendelea, mahitaji ya mitaji ya muda mrefu yanatarajiwa kuongezeka ili kuimarisha viwanda, kuboresha kilimo, kuendeleza miundombinu ya usafiri na ugavi, kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuwekeza katika miundombinu ya kijamii.


Kwiyukwa amesema jukumu la TIB ni kuwa kichocheo cha uwekezaji wenye manufaa mapana kwa uchumi.

"Tunasaidia kufungua fursa za uwekezaji zinazoongeza uzalishaji, kuimarisha huduma za umma na kuchangia maendeleo ya taifa. Mafanikio ya ufadhili wa maendeleo hayapimwi kwa kiasi cha fedha kilichotolewa, bali kwa athari zake katika uchumi na maisha ya wananchi," amesema.

Mbali na kutoa fedha, TIB pia husaidia taasisi za Serikali na wawekezaji binafsi kuandaa miradi yenye ubora wa kitaalamu na uwezo wa kuvutia uwekezaji wa muda mrefu.

Kwa mujibu wa benki hiyo, miradi mingi hushindwa kufikia hatua ya kupata wawekezaji kutokana na upungufu wa tafiti za upembuzi yakinifu, tathmini hafifu za hatari na mifumo dhaifu ya ufadhili.

Hivyo, Kwiyukwa amesema maendeleo ya kweli hupimwa kwa matokeo yanayoonekana, ikiwamo kuongezeka kwa uzalishaji viwandani, wakulima kupata masoko bora, biashara kupata umeme wa uhakika, wananchi kupata huduma za maji safi na kuongezeka kwa ajira.

Kwa mtazamo wake, mafanikio ya Dira 2050 hayatapatikana kwa kuwa na maono pekee, bali kwa kuandaa miradi bora, kuwekeza kimkakati na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo, wawekezaji na taasisi za kifedha.

Kupitia utoaji wa mitaji ya muda mrefu na usaidizi katika maandalizi ya miradi, TIB inalenga kuchangia utekelezaji wa Dira 2050 na kuharakisha ukuaji endelevu wa uchumi.