Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yachota mbinu Indonesia kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni

Muktasari:

  • Indonesia imefanikiwa kujenga uchumi mkubwa unaokadiriwa kuwa karibu mara 20 ya uchumi wa Tanzania



Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan-Trade) imewataka Watanzania kutumia fursa zinazotokana na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia, ikisema zinaweza kuchochea ukuaji wa biashara, uwekezaji, viwanda, teknolojia na elimu nchini.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Julai 3, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Indonesia yaliyofanyika ndani ya Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), huku viongozi kutoka Tanzania na Indonesia wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tan-Trade, Profesa Ulingeta Mbamba amesema Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Indonesia, hususan katika maendeleo ya viwanda, biashara, utalii na mageuzi ya uchumi.

Amesema Indonesia imefanikiwa kujenga uchumi mkubwa unaokadiriwa kuwa karibu mara 20 ya uchumi wa Tanzania, huku ikiwa na idadi ya watu inayokadiriwa kuwa takribani mara nne ya Tanzania.

Profesa Mbamba amesema pato la taifa la Indonesia linakadiriwa kufikia Dola 1.5 trilioni za Marekani (Sh3.94 trilioni), jambo linaloifanya nchi hiyo kuwa mfano muhimu kwa Tanzania katika safari ya kujenga uchumi wa viwanda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Profesa Ulingeta Mbamba, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku Maalumu ya Indonesia yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

"Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Indonesia. Tumeona hatua kubwa walizopiga katika maendeleo ya viwanda, biashara na sekta nyingine za uchumi ambazo zinaweza kutupa uzoefu wa kuharakisha maendeleo yetu," amesema.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi, huku ushirikiano wa kimataifa ukiwa miongoni mwa nguzo muhimu za kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.

Profesa Mbamba pia amewataka vijana na wanafunzi kutumia fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa na Serikali ya Indonesia, akisema elimu ni eneo muhimu litakalosaidia kuongeza ujuzi, ubunifu na ushindani wa Watanzania katika soko la ajira.

Aidha, amesema Indonesia imepiga hatua kubwa katika sekta ya utalii, hivyo Tanzania inaweza kujifunza mbinu mbalimbali za kukuza sekta hiyo sambamba na kutangaza bidhaa na huduma zake katika soko la Indonesia.

"Maonyesho haya ya kimataifa yanatoa nafasi ya kujifunza kutoka kwa mataifa mbalimbali yanayoshiriki. Tunapaswa kutumia fursa hizi kupata maarifa na kuyatumia katika kuendeleza uchumi wetu," amesema.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Profesa Mbamba amesema lengo la Tanzania kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani litategemea kasi ya kukuza biashara, uwekezaji, viwanda na ushirikiano wa kimataifa.

Naibu Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Priadj Soelaiman amesema Tanzania ni miongoni mwa washirika muhimu wa biashara wa Indonesia barani Afrika, hivyo nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Amesema Tanzania na Indonesia zinaendelea kushirikiana kupunguza pengo la biashara baina yao na kupanua ushirikiano katika sekta za viwanda, kilimo, teknolojia, uwekezaji na biashara ya bidhaa.

"Tunafanya maadhimisho haya ya Siku ya Indonesia kama sehemu ya juhudi za kuimarisha na kuweka uwiano wa biashara kati ya Indonesia na Tanzania. Tunafurahishwa kuona hatua nzuri zinaendelea kupatikana," amesema.

Amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kushiriki katika matukio mbalimbali ya biashara yatakayofanyika Indonesia Oktoba mwaka huu ili kutafuta masoko mapya, washirika wa kibiashara na fursa za uwekezaji zitakazonufaisha mataifa yote mawili.