Ongezeko la Pato la Taifa linagusaje maisha yako?
Wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kukua kwa kasi, mojawapo ya maswali yanayoendelea kujitokeza miongoni mwa wananchi ni kwanini takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) na hata pato la Mtanzania mmoja mmoja, hazionekani na kugusa maisha yao ya kila siku.
Ingawa Serikali hutangaza mafanikio ya kiuchumi, wananchi wengi bado wanahisi kama hawanufaiki ipasavyo na ukuaji huo.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha uthabiti wa uchumi wake huku kiwango cha ukuaji wa uchumi kikifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2024.
Hiyo ikiwa na maana kuwa, Pato la Taifa limeongezeka hadi Sh234.1 trilioni mwaka 2025 kutoka Sh211.98 trilioni mwaka 2024, baada ya urekebishaji wa takwimu kwa kutumia mwaka 2019 kama msingi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa sasa pato la kila Mtanzania pia limeongezeka kwa asilimia 7.4 hadi kufikia Sh3.54 milioni mwaka 2025 kutoka Sh3.30 milioni mwaka uliopita.
Hata hivyo, hali halisi inayoonekana kwa wananchi wengi ni kushindwa kukubaliana na takwimu zinazotolewa huku wengi wakihoji ni kwa nini ukuaji huo wa uchumi hauonekani katika maisha ya kila siku.
Baadhi ya wananchi wanadai kutoona ahueni katika maisha yao ya kila siku zaidi wanashuhudia kuongezeka kwa gharama za maisha wakati kipato chao kikibaki kuwa chini.
Alfred Urio, mkazi wa Tabata anasema mshahara anaopata haujaongezeka kwa miaka miwili sasa, huku bei za vitu muhimu ikiongezeka.
“Leo hii hadi chapati uliyokuwa unapata kwa Sh300 sasa ni Sh500 katika baadhi ya maeneo ukiuliza unaambiwa vita ya Marekani, hili linafanyika wakati ambao sisi wa viwandani bado tunalipwa Sh5,000 kwa siku, ni ngumu kuona ukuaji wetu,”
“Hili halionekani katika vyakula pekee hata kodi za nyumba tunazoishi zimepanda, nauli, imekuwa kama tunafanya kazi kwa ajili ya kula na kuishi siyo kutafuta maendeleo, ndiyo maana unaposema kipato changu kimeongezeka nakuwa sielewe,” anasema.
Wachambuzi wa uchumi wanasema changamoto kubwa ipo katika namna ukuaji unavyoongezeka, sekta zinazogusa wananchi wengi moja kwa moja zikiwa hazifikiwi kikamilifu.
Ingawa sekta kama kilimo, ujenzi, madini, biashara na huduma zinachangia sehemu kubwa ya uchumi, bado kiwango cha ajira bora na kipato kinachozalishwa hakigusi maisha ya watu au kuwafikia kwa usawa.
Hii ina maana kuwa ukuaji wa GDP unaweza kutokea kupitia sekta chache au miradi mikubwa ya uwekezaji bila kuleta mabadiliko makubwa ya moja kwa moja kwa kaya nyingi matokeo yake, wananchi wanabaki na hisia kuwa takwimu zinaongea jambo tofauti na maisha yao.
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Dk Felix Nandonde anasema mtu anaposikia Pato la Taifa limeongezeka au uchumi umekua kwa kiwango fulani, mara nyingi hujiuliza jambo hilo linamhusu kwa namna gani, hasa pale anapokabiliwa na changamoto za gharama za maisha, kipato kidogo au ugumu wa kumudu mahitaji muhimu.
“Ni ngumu kwa wananchi wengi kutafsiri sera za uchumi mkubwa (macroeconomics) na kuzihusisha moja kwa moja na maisha yao ya kawaida. Ndiyo maana ni muhimu kuhakikisha mafanikio ya uchumi mkubwa yanatafsiriwa katika maboresho ya uchumi mdogo unaogusa kaya na wananchi mmoja mmoja,” anasema Dk Nandonde.
Anasema moja ya maeneo ambayo Serikali imeonesha mafanikio ni katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuuweka ndani ya viwango vinavyokubalika, hata hivyo anabainisha kuwa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, wananchi hupima mafanikio ya uchumi kwa kuangalia bei za bidhaa muhimu, hususan vyakula wanavyotumia kila siku.
“Kama ni mahindi na maharagwe ili watu wale ugali ni lazima uweke urahisi katika upatikanaji wake kama ni kilimo uwekezeke, ukileta unafuu katika upatikanaji wa mbolea na pembejeo nyingine za kilimo, uzalishaji utaongezeka, mazao yatakuwa mengi sokoni na bei za chakula zitakuwa nafuu. Hapo ndipo wananchi wataanza kuona nafasi yao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” anasema.
Anasisitiza kuwa ili pato la mtu mmoja mmoja liongezeke kwa kasi zaidi, ni muhimu kuwekeza katika sekta wananchi wengi, hasa kilimo kinachoajiri na kuingiza kipato kwa sehemu kubwa ya Watanzania hali itakayosaidia kupunguza umasikini.
Kuhusu umaskini, Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango chake hadi asilimia 25.1 mwaka 2025 kutoka asilimia 26.4 mwaka 2018.
Wataalamu wanasema ili ukuaji wa uchumi uonekane kugusa maisha ya wananchi, lazima uwekezaji uelekezwe zaidi katika sekta zinazogusa watu wengi, hususan kilimo, biashara ndogo na za kati, pamoja na viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao.
Upande wa sekta zinazogusa watu wengi, kilimo ni moja ya eneo ambalo limepigiwa chapuo kutokana na kuajiri watu wengi zaidi nchini.
Utegemezi wa kilimo
Katika Bunge la Bajeti ya mwaka 2026/27 linaloendelea hivi sasa mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo anasema kilimo kinaweza kuwa injini kuu ya uchumi wa Tanzania endapo kitaunganishwa na viwanda vya kuongeza thamani, akibainisha kuwa sekta hiyo inaweza kuchangia hadi asilimia 30 ya Pato la Taifa.
Anasema changamoto kubwa iliyopo ni kuwapo kwa upungufu wa pembejeo zinazohitajika kila mwaka.
“Mahitaji ya mbegu nchini kila mwaka ni tani 130,000 lakini bado kuna upungufu wa asilimia 50.8. Matumizi ya mbolea pia yapo chini ya kiwango kinachohitajika mtu anapaswa kutumia kilo 50 kwa hekta moja, sasa mtu anatumia kilo 20 hivyo lazima tuwekeze zaidi katika pembejeo na kilimo cha umwagiliaji,” anasema.
“Uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ni muhimu ili kupunguza utegemezi wa mvua na kuongeza uzalishaji wa mwaka mzima,” anasema.
Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania wanategemea kilimo kama chanzo chao kikuu cha ajira na kipato.
Idadi hii inajumuisha mamilioni ya wakulima wadogo na familia zao wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.
Hayo yanashauriwa wakati ambao Tanzania inalenga kufikia uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani kwa mwaka ifikapo mwaka 2050 kupitia utekelezaji wa dira ya maendeleo, azma inayoenda sambamba na kujenga uchumi jumuishi.
Ili kufikia hilo, bajeti ya kwanza kuelekea dira hiyo ambayo ni ile ya mwaka 2026/27 imeweka bayana mapendekezo ya hatua mpya za kisera za mapato na matumizi kwa mwaka 2026/27.
Hatua hizo zinalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji, kulinda na kuimarisha sekta ya viwanda nchini kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kujitegemea katika ugharamiaji wa sehemu kubwa ya Bajeti ya Serikali na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali na umma kwa ujumla.
“Bajeti ya mwaka 2026/27 ina dhima ya kujenga uchumi himilivu kupitia mageuzi ya kidijitali, uwekezaji wa kimkakati na sera endelevu za kibajeti kwa ukuaji jumuishi wa uchumi,” alisema Waziri wa Fedha, Khamis Omar Mussa wakati akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma.
Bajeti binafsi changamoto
Wakati watu wakishangaa kusikia pato la mtu mmoja limekua, Mtaalamu wa Fedha, Makame Msafiri anasema watanzania wengi kushindwa kuongeza pato lao binafsi na kujenga utajiri kwa muda mrefu ni ukosefu wa utamaduni wa kupanga matumizi kupitia bajeti.
“Watu wengi hujikita katika kutafuta namna ya kuongeza kipato lakini hawatoi umuhimu sawa katika kusimamia fedha wanazopata hali inayosababisha mapato kuishia kwenye matumizi ya kawaida badala ya kugeuzwa mtaji wa uwekezaji,” anasema.
Anasema ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja haupimwi tu kwa kiasi cha fedha anachopata, bali pia kwa uwezo wake wa kuweka akiba, kuwekeza na kuongeza thamani ya mali alizonazo.
“Hali hiyo ndiyo inayofanya baadhi ya wananchi kubaki katika kiwango kilekile cha maisha kwa miaka mingi licha ya ongezeko la mishahara au mapato ya biashara.”
“Badala ya kutumia mapato ya ziada kuanzisha miradi mipya, kununua mali zinazozalisha kipato au kuwekeza katika elimu na ujuzi, fedha nyingi huishia katika matumizi ya muda mfupi ambayo hayachochei ukuaji wa uchumi wa mtu binafsi,” anasema.
Anasema mtu anaweza kupata nyongeza ya mshahara au biashara yake kuongezeka lakini kama hana bajeti fedha hizo hazitabadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.
“Ukuaji wa pato la mtu mmoja huanza pale anapoweza kuelekeza sehemu ya mapato yake katika uwekezaji, akiba na shughuli zinazozalisha kipato zaidi,” anasema.