Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maisha ya wananchi yapime maendeleo si Pato la Taifa

Wakazi wa kijiji cha Rugese kata Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera wakiwa katika  foleni ya maji  ambapo inawalazimu kuamka  saa 9 alfajiri ili kuwahi foleni hiyo kama walivyokutwa kijijini hapo hivi karibuni.  Katika kata hiyo kuna Mradi wa maji uliofadhiliwa na Benki ya dunia ambao haukukidhi mahitaji ya wakazi wa vijiji vitano vya kata hiyo. Picha na Shaaban Ndyamukama

Muktasari:

  • Takwimu za Serikali, zinaonyesha ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) umepungua kidogo. Katika mwaka 2017 kwa mfano, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.3 za mwaka 2016. Licha ya kushuka huko kwa ukuaji wa GDP, bado kiwango hicho kimeonekana kuwa juu kuliko nchi zote za Afrika Mashariki kwa mwaka 2017.

Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kati ya asilimia sita hadi saba kwa mwaka. Hata hivyo, wakati mikakati ya kukabiliana na umaskini ikiimarishwa, idadi ya watu maskini bado ni kubwa nchini.

Takwimu za Serikali, zinaonyesha ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) umepungua kidogo. Katika mwaka 2017 kwa mfano, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 7.3 za mwaka 2016. Licha ya kushuka huko kwa ukuaji wa GDP, bado kiwango hicho kimeonekana kuwa juu kuliko nchi zote za Afrika Mashariki kwa mwaka 2017.

Hata hivyo, baadhi ya wachumi wanaona ukuaji wa GDP sio kipimo sahihi cha maendeleo, bali ustawi wa maisha ya wananchi ndiyo yanapaswa kuwa kipimo muafaka cha kuangalia mabadiliko yaliyopo.

Wakizungumza katika mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baadhi ya wachumi maarufu duniani wameitaka Serikali kutopima maedeleo kwa GDP.

Katika wasilisho lake lililohusu kuweka usawa wa masoko kati ya Serikali na wananchi, mchumi maarufu na mshindi wa Tuzo ya Nobel, Profesa Joseph Stiglitz anasema Serikali haipaswi kuhesabu maendeleo kwa kuzingatia GDP bali yawahusishe wananchi kwanza.

“Serikali haipaswi kujikita kwenye kuongeza GDP pekee. Malengo ya maendeleo ni kuwezesha ustawi wa wananchi. Soko linaloendeshwa na ukuaji wa GDP litawanufaisha watu wachache tu na hakutakuwa na mabadiliko katika jamii,” anasema Profesa Stiglitz.

Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Columbia anasema GDP ni kipimo cha masoko ambayo pato lake siyo ishara sahihi ya hali ya jamii. Kwamba, GDP inaweza kukua lakini kipato cha wananchi kikashuka kutokana na faida kubwa ikwenda nje hivyo kiwango cha maisha kuzidi kushuka zaidi na zaidi.

Aliyekuwa mchumi mkuu wa Benki ya Dunia, Profesa Kaushik Basu anasema tangu wakati wa Azimio la Arusha, hayati Mwalimu Julius Nyerere alizungumzia maendeleo katika ustawi wa wananchi.

Anasema katika historia ya dunia kumekuwa na mikutano mingi iliyoshirikisha mawazo ya watu kuhusu maendeleo shirikishi akiutaja ule wa Bandung mwaka 1955 uliokuwa wa vuguvugu la nchi zisizofungamana na upande wowote na Azimio la Arusha wa mwaka 1967.

Anasema mikutano hiyo inafanana na Azmio la Stockholm ambalo wataalamu wa uchumi walikutana mwaka 2016 na kuweka misingi ya maendeleo inayozingatia zaidi watu.

“Ni furaha kwamba umuhimu wa tamko la Stockholm linapatikana katika Azimio la Arusha la mwaka 1967 ambalo linaeleza msingi wa maendeleo ni watu,” anasema. Mwenyekiti wa bodi ya ESRF, Philemon Luhanjo anasema hoja na maoni ya wataalamu na wadau wa maendeleo ni nguzo muhimu za kuishauri Serikali jinsi ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.

“Tunaangalia jinsi sera zinazvyoathiri maisha ya watu duniani kote. Ni muhimu tupande sera zetu za uchumi na kijamii kwa kuhakikisha kila mtu anakuwa na kipato. Sera zetu zielekeze maendeleo ya watu badala ya vitu,” anasema.

Umaskini Tanzania

Akieleza sababu ya umaskini kuongezeka nchini wakati akifungua mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema licha ya Tanzania kuwa na utajiri wa rasilimali, amani na utulivu bado maisha ya wananchi wengi ni duni.

Alisema Tanzania ina utajiri wa rasilimali akitoa mfano wa maziwa kama Viktoria, Tanganyika, Rukwa, Nyasa na mito mingi inayotoa fursa za uvuvi na uzalisha wa umeme. Pia, hakusahau utajiri wa madini kama dhahabu, almasi, tanzanite, chuma, makaa ya mawe na uranium pamoja na gesi ya asili, na helium.

Hata kwenye utalii, alisema Tanzania ni kituo kikubwa chenye kilometa 1,200 za fukwe za bahari, hifadhi za wanyama isiyo na machafuko ya kikabila, kisiasa wala kidini.

Alitaja chanzo cha matatizo hayo kuwa ni pamoja na ukosefu wa teknolojia akitoa mfano wa wachimbaji wadogo wa madini wanaoshindwa kupata madini ya kutosha kutokana na uduni wa zana wanazotumia.

“Ukosefu wa mitaji unasababisha kushindwa kugawana rasilimali hizo. Kutokuwapo kwa uwiano kati ya uchumi na kilimo, mifugo na uvuvi ulioajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni tatizo jingine,’’ alisema.

Viwanda

Katika hatua nyingine, kabla ya mkutano huo, wataalamu hao wa uchumi walikuwa na mjadala mwingine ambapo walijikita katika uchumi wa viwanda.

Wakati Serikali ya awamu ya tano ikipiga kampeni ya uanzishaji wa viwanda, wataalamu wameshauri kujikita kwa vitakavyosindika mazao ya kilimo kinachoajiri wananchi wengi.

Akizungumza katika mhadhara uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, Profesa Stiglitz alisema Tanzania inatakiwa kuweka mikakati itakayowezesha uzalishaji wa bidhaa na kuuza katika masoko ya kimataifa.

“Tanzania inapaswa kuwa na mikakati endelevu itakayowezesha uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya soko la nje na kuiwekea maono mapya ya maendeleo,” alisema Profesa Stiglitz.

Kuhusu kilimo, Profesa Stiglitz anasema ili kuinua uchumi wa viwanda lazima kiimarishwe ili kuongeza ajira na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani.

Anasema kuuongezeka kwa uzalishaji wa kilimo kunachangia kukua kwa miji kwa namna nyingine kwa maendeleo ya Tanzania hasa katika utalii.

“Serikali ina jukumu kubwa la kufanya mabadiliko kuelekea uchumi wa kisasa ambao si wa uzalishaji tu wa viwandani bali utoaji huduma na kilimo cha kisasa ndiyo muhimu,” anaongeza mtaalamu huyo.

Idadi ya watu

Kuhusu ongezeko la watu, Profes Stiglitz anasema hadi mwaka 2100 idadi ya watu duniani itaongezeka mara nne ya waliopo sasa wengi wakitokea Afrika.

Kutokana na makadirio hayo, anashauri haja ya Afrika kujipanga kuzalisha ajira milioni 500 ili kukabiliana na ukosefu wa ajira utakaojitokeza kutokana na ongezeko hilo la watu. Idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi itaongezeka mpaka bilioni 2.1 au zaidi.

Akizungumza baada ya mhadhara huo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Profesa Adolf Mkenda alisema suala la viwanda si la kuhamisha uzalishaji kutoka nchi zilizoendelea tu bali kuzalisha bidhaa zinazohitajika nchini.

“Lazima tuzalishe bidhaa tunazotumia na tujifunze kwa wenzetu bila hivyo tutabaki kama uchumi wa casino mahali ambapo watu wanakuja kucheza kamari tu au tuwe kama nchi ya Barbados ambayo wanakwenda kupumzuka ufukweni tu,,” alisema.

Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Mwesiga Baregu anasema sera ya Tanzania ya viwanda haitafanikiwa ikiwa itazalisha bidhaa zisizoshindana kwenye masoko ya nje.

“Uzalishaji wa kilimo bado uko chini, lakini mazao ya kilimo yanahitajika kwenye masoko ya nje. Kwa hiyo tuimarishe kilimo kwa ajili ya kuuza mazao yake nje ya nchi na kutengeneza viwanda vya mazao hayo,” anasema Profesa Baregu.