Uzalishaji viazi mviringo wapaisha mapato ya Halmashauri Rungwe
Muonekano wa moja ya shamba la viazi mviringo vinavyo zalishwa mkoani Mbeya. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Uzalishaji wa zao hilo umepanda kutoka tani 507,211 hadi tani 618,278.6 ndani ya miaka mitatu.
Mbeya. Uzalishaji wa zao la viazi mviringo katika Wilaya ya Rungwe umeendelea kuimarika, ukipanda kutoka tani 507,211 hadi tani 618,278.6 ndani ya miaka mitatu, ongezeko linalotokana na kupanuka kwa maeneo ya kilimo na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Akizungumza leo Juni 18, 2026, Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Rungwe, Adam Nkhangaa, amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na upimaji wa afya ya udongo, matumizi sahihi ya pembejeo na upatikanaji wa masoko ya uhakika.
“Tumepanua maeneo ya kilimo kutoka hekta 24,742 msimu wa 2022/2023 hadi hekta 24,982 msimu wa 2024/2025. Pia wakulima sasa wanapima afya ya udongo na kutumia mbolea kulingana na mahitaji,” amesema Nkhangaa.
Ameitaja Kata za Kyimo, Kiwira, Ndato, Ibighi na Isongole kuwa vinara wa uzalishaji kutokana na matumizi ya mbegu bora na usimamizi mzuri wa kilimo.
“Wakulima wengi sasa wanazalisha viazi vyenye ubora kwa kutumia mbegu bora zinazostahimili mazingira,” ameongeza.
Kuhusu mikakati ya msimu ujao, Nkhangaa amesema halmashauri imejipanga kuhakikisha maofisa ugani wanawafikia wakulima wote, pamoja na kuimarisha upimaji wa afya ya udongo kabla ya msimu wa kilimo.
Muonekano wa moja ya shamba la viazi mviringo vinavyo zalishwa mkoani Mbeya. Picha na Hawa Mathias
“Mpango huu utamwezesha mkulima kujua hali ya shamba lake na kupata ushauri sahihi wa mbolea na mazao yanayofaa,” amesema.
Aidha, amesema changamoto iliyokuwepo awali ya matumizi holela ya mbolea bila ushauri wa kitaalamu imeanza kupungua kutokana na uwepo wa vifaa vya upimaji wa udongo kutoka Wizara ya Kilimo.
Katika hatua nyingine, Nkhangaa amesema zao la viazi mviringo limekuwa chanzo kikuu cha mapato ya ndani, ambapo mwaka wa fedha 2024/2025 zaidi ya Sh1.2 bilioni zilikusanywa, sawa na asilimia 22.36 ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
“Parachichi na viazi mviringo ndiyo mazao yanayoongoza kuchangia mapato yetu ya ndani na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema.
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Ndato wameipongeza Serikali kwa kuwekeza katika kilimo, lakini wameiomba kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.
Mkulima, Ezron Jonathan amesema ubovu wa barabara umewafanya wakulima kuuzwa mazao kwa bei ya chini kupitia mfumo wa lumbesa unaowapunguzia kipato.
“Tunaomba barabara ziboreshwe ili tuuze kwa bei halisi badala ya kunyonywa na madalali,” amesema.