Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sangu: Tofauti za kisiasa zisikwamishe utekelezaji Dira ya Taifa 2050

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, wakati akifungua warsha ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa iliyofanyika Morogoro Juni 17, 2026.

Muktasari:

  • Amesema ushirikiano baina ya Vyama vyote na serikali utakuwa muhimu zaidi wakati Tanzania itakapoanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ajenda ya muda mrefu inayohitaji umoja wa dhamira unaovuka mipaka ya vyama vya siasa.

Dar es Salaam. Serikali imevitaka vyama vya siasa nchini kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kuimarisha mazungumzo, ushirikiano na umoja wa kitaifa wakati Tanzania ikijiandaa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuanzia Julai 2026.

Wito huo umetolewa jana Juni 17, 2026 mjini Morogoro na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu wakati akifungua warsha ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa.

Warsha hiyo iliandaliwa kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jukumu jipya la mahusiano ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa kisiasa.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo,   Sangu alisema vyama vya siasa si washindani wa uchaguzi pekee, bali ni washirika muhimu katika kulinda amani, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuendeleza ustawi wa jamii.

Alisema utayari wa vyama hivyo kushirikiana na Serikali ni msingi muhimu wa kujenga mahusiano imara kati ya dola na makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo vyama vya siasa vyenyewe.

Pia aliwataka viongozi wa kisiasa kuendelea kuwa mabalozi wa amani na kuwaonya dhidi ya kuruhusu watu wachache wenye maslahi binafsi kuigawa nchi au kudhoofisha utulivu wake.

“Leo, tunapojadili mahusiano kati ya Serikali na vyama vya siasa, napenda kuwahakikishia kuwa dhana hii inatekelezwa kupitia falsafa ya 4Rs iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kujenga Taifa lenye amani na umoja,” alisema Waziri Sangu.

Alifafanua falsafa hiyo inayojumuisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya, alisema inaendelea kuongoza juhudi za Serikali za kuimarisha mazungumzo, kujenga imani na kupanua ushirikishwaji wa kisiasa unaojumuisha makundi yote ya jamii.

Waziri Sangu aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali, ikiwemo kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali muhimu ya kitaifa.

Alisema ushirikiano huo utakuwa wa umuhimu mkubwa zaidi wakati Tanzania itakapoanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ajenda ya muda mrefu inayohitaji umoja wa dhamira unaovuka mipaka ya vyama vya siasa.

Akiunga mkono kauli ya Waziri Sangu, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, alisema vyama vya siasa vina ushawishi mkubwa katika jamii ya Watanzania na vinaweza kutoa mchango muhimu katika kuimarisha amani, maelewano na mahusiano mema miongoni mwa wananchi.

Alisema Baraza hilo linatambua dhamira ya Rais Samia ya kuendeleza siasa shirikishi, akitolea mfano uteuzi wa mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo, Eveline Wilbard Munisi wa NCCR-Mageuzi, kuwa Mbunge na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano.

Kwa mujibu wake, uteuzi huo unaakisi imani, ushirikishwaji na ushirikiano katika mfumo wa kidemokrasia wa Tanzania.

Akitoa maelezo ya msingi kuhusu warsha hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema mkutano huo umefanyika kufuatia kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Vyama vya Siasa kilichofanyika Mei 21, 2026.

Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iwasilishe mada itakayosaidia kujenga uelewa kuhusu jukumu jipya la mahusiano kwa manufaa ya ustawi wa Tanzania.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na viongozi kutoka vyama 18 kati ya vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa nchini, vikiwemo ACT Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF).

Mkutano huo ulitoa jukwaa kwa vyama vya siasa, Serikali na wadau wengine kujadiliana namna mazungumzo yenye utaratibu yanavyoweza kuimarisha umoja wa kitaifa, maridhiano na maendeleo jumuishi nchini.