Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulanzi ni zaidi ya kilevi, umebeba utajiri

Mhadhiri Mwandamizi wa Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Lewis Mtashobya akionyesha moja ya bidhaa iliyotengenezwa baada ya kuongeza thamani ya pombe ya Ulanzi

Muktasari:

  • Utafiti umebaini kuwa ulanzi unaweza kubadilishwa kuwa bioethanol, viyeyusho vya maabara, spiriti ya kliniki, pafyumu, dawa za kusafishia na siki ya viwandani

Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, wakazi wa Nyanda za Juu Kusini wameufahamu ulanzi kama kinywaji cha asili kinachotumiwa kwa matumizi ya kawaida, huuzwa kwa bei nafuu na huharibika kwa haraka, hivyo kutotambuliwa kama bidhaa yenye thamani kubwa ya kiuchumi.

Hata hivyo, hali hiyo sasa inaanza kubadilika baada ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kubaini kuwa ulanzi unaweza kuwa malighafi muhimu ya kuzalisha bidhaa za viwandani zenye thamani kubwa ya kiuchumi.

Akizungumza jana Jumatano Julai mosi 2026 katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea Mhadhiri Mwandamizi wa Kemia, Dk Lewis Mtashobya amesema utafiti wao umebaini ulanzi ni zaidi ya vile ambavyo watu wanautazama.

“Tumebaini ulanzi unaweza kubadilishwa kuwa bioethanol, viyeyusho vya maabara, spiriti ya kliniki, pafyumu, dawa za kusafishia na siki ya viwandani,” amesema.

Kwa kawaida, lita moja ya ulanzi iliuzwa kwa bei ya kati ya Sh200 na Sh1,000 pekee, hali iliyowafanya baadhi ya wakulima kukata miti inayozalisha ulanzi au kuiacha bila kuitunza kutokana na kutokuwa na faida ya kiuchumi.

Hata hivyo, teknolojia mpya inalenga kuongeza thamani ya ulanzi na kuugeuza kuwa zao la kibiashara, hususan kwa jamii za Nyanda za Juu Kusini ambako hupatikana kwa wingi, hasa katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Iringa.

Dk Mtashobya amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021 unalenga kuongeza thamani ya ulanzi sambamba na kuhamasisha wakulima kuanzisha mashamba badala ya kutegemea miti ya asili inayorithiwa.

Amesema bei ulanzi sokoni imekuwa kikwazo kwa wakulima, hali inayosababisha wengine kukata miti hiyo na kubadili matumizi ya ardhi.

“Wakati wa msimu wa mvua, lita moja ya ulanzi inaweza kuuzwa hadi Sh200 tu na katika misimu mingine hufika Sh1,000. Mapato haya duni yamechangia baadhi ya wakulima kukata miti hiyo,” amesema.

Amesema endapo hakuna jitihada za kuongeza thamani ya zao hilo, Tanzania inaweza kupoteza rasilimali ya asili yenye thamani kubwa kiuchumi na kimazingira.

Kutokana na changamoto hiyo, watafiti wamebuni teknolojia zinazobadilisha ulanzi kuwa bidhaa mbalimbali zenye matumizi ya kibiashara.

“Tunaweza sasa kuzalisha viyeyusho vya maabara kwa ajili ya maabara za sayansi, spirit ya kliniki, pafyumu, bioethanol ambayo ni nishati safi isiyoathiri mazingira. Hizi ni bidhaa zenye uwezo mkubwa wa kibiashara,” amesema.

Ameongeza kuwa bioethanol inayopatikana kutoka kwenye ulanzi ina takribani asilimia 45 ya pombe ambayo pia inaweza pia kutumika kama malighafi ya kutengeneza vinywaji kama whisky.

 “Utafiti wetu umeonyesha hata mabaki ya baada ya kuchakata yanaweza kubadilishwa kuwa bidhaa muhimu na tumeshachapisha tafiti za kisayansi zinazoonesha ubunifu huu,” ameeleza.

Amesema mafanikio hayo tayari yamezalisha haki miliki za ubunifu, hatua inayoweka msingi wa uwekezaji wa kibiashara kupitia ushirikiano na sekta binafsi.

Dk Mtashobya amesema iwapo uzalishaji utaongezwa, kuna uwezekano wa kuanzisha biashara mpya, kuongeza ajira, kuongeza kipato cha wakulima na kuchangia katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kijani unaotumia rasilimali zake.

Amesema ubunifu huo ni sehemu ya juhudi za UDSM kukuza uchumi unaotegemea utafiti kwa kubadilisha rasilimali za ndani kuwa bidhaa zenye uwezo wa kupunguza uagizaji wa bidhaa, kuimarisha viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya sekta ya kilimo nchini.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa walitembela Sabasaba,William Sanga amesema anaiona fursa mpya ya ukuaji wa kiuchumi kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini.

“Hiki ni kitu kizuri sana kama elimu itatolewa kikamilifu na watu wakawa na uhakika wa soko, watu wakiona fursa vizuri, kufanya uwekezaji si suala litakalowasumbua,” amesema.