Usiyoyajua kuhusu kituo cha biashara Ubungo

Dar es Salaam. Unafahamu nini kuhusu Mradi wa Kituo cha Pamoja cha Kibiashara, unaojengwa eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam?

Kituo hicho cha upangishaji wa maduka kinatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Kituo kinajengwa chini ya Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC), unajengwa kwa miezi 18 kupitia uwekezaji wa Dola 110 milioni (Sh264 bilioni).

Kituo hicho kinajengwa katika eneo la mita za mraba 7,500 mahali palipokuwa Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani kabla ya kuhamishiwa Mbezi ya Kimara.

Akizungumza leo Septemba 17, 2023 wakati wa ziara yake, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameagiza mradi huo kuzingatia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo.

“Nasisistiza Machinga wapewe kipaumbele, pia kuna hofu kwamba kituo hiki kitaua soko la Kariakoo, hapana kitasaidia kupanua huduma,” amesema Profesa Kitila.

Profesa Kitila amesema kituo hicho kitakuwa cha kwanza kwa ukubwa ukanda wa Afrika Mashariki na nchi 16 za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kwa kupokea wafanyabiasha.

Aidha amesema kituo hicho kitakuwa na mauzo ya Dola 500 milioni kwa mwaka na kitasaidia kupunguza matumizi ya dola katika uagizaji bidhaa nje.

“Kwa mwaka jana tulitumia  Dola za Kimarekani   Sh5.394 (Sh9.4 trilioni) kuagiza bidhaa nje, sasa kituo hiki kitakuwa na bidhaa ambazo zingeenda kununuliwa nje,” amesema.

“Lakini nyingine ya kuongeza dola ni mazao yetu kuchakatwa na kusafirishwa kama bidhaa nje.”

Mkurugenzi’s Mkuu wa EACLC, Cathy Wang amesema kituo kitahusisha jengo kubwa la ghorofa litakalokuwa na maduka 2,060 ya wafanyabiashara.

“Jengo hili litakuwa na majengo manne, kila jengo litakuwa na huduma ya bidhaa tofauti, pia tutafungua soko la bidhaa za China badala ya kufuata China. watanunua hapa kwenye kituo,” amesema Cathy.

Kwa mujibu wa EACLC, Kituo hicho kinatarajia kuzalisha ajira 15,000 za moja kwa moja na nyingine 50,000 zisizokuwa za moja kwa moja.