Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti: Maelfu ya Watanzania wanaishi chini ya 'buku jero' kwa siku

Je, unaweza kutumia Sh1,500 kwa mahitaji yako yote kwa siku? Utafiti iliyofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa Watanzania maskini inaonesha uwepo wa kaya zinazotumia wastani wa Sh1,419 kwa siku.

Zaidi ya kaya 11,086 katika vijiji 434 kwenye mamlaka 36 za maeneo maskini zaidi ya mradi (PAAs) yaliyopo katika mikoa 17 nchini, zimeonyesha kuwa kiwango hicho kipo chini kidogo ya mstari wa umaskini wa kitaifa wa Tanzania wa Dola za Marekani 0.80 (Sh2,000).

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kila kaya nchini ina wastani wa watu wanne hadi watano. Utafiti huo wa mwaka 2022 ulionyesha kuwa kati ya Sh1,500 zinazotumiwa na familia, Sh1,125 ni kwa ajili ya chakula, huku Sh375 zikitumiwa kwa matumizi mengine.

Utafiti huo ulifanyika ikiwa ni utekelezaji wa tathmini ya awamu ya pili ya mpango wa PSSN II wenye lengo la kuboresha upatikanaji wa fursa za kiuchumi na huduma za kijamii kwa kaya maalumu ili kuimarisha ustawi wa kaya hizo.

Matokeo yanaonesha kila mwezi jumla ya matumizi ya kaya ni wastani wa Sh152,621 (Dola za Marekani 65.50), na jumla ya matumizi ya chakula ni Sh113,256 (US$48.6). Takriban asilimia 43 ya matumizi ya chakula yanatokana na ununuzi wa chakula na iliyobaki ni kutokana na uzalishaji na zawadi.

“Kipato changu kwa siku ni Sh8,000 na katika matumizi natumia Sh6,000 kwa kujibana sana, nakula asubuhi Sh1,500, mchana Sh1,500 na maji ya Sh500, pia usiku hivyohivyo,” anasema Juma Ramadhan (si jina lake halisi), mkazi wa Mabibo, Dar es Salaam ambaye hujishughulisha na uchomaji wa mahindi barabarani.

“Nimejiwekea ratiba ya kila siku kuweka Sh2,000. Nikisema nijiachie hela yote itaishia tumboni. Hivyo najitahidi kujibana siku nyingine naweka hadi Sh4,000. Unajua lazima uwe na akiba, sisi binadamu lolote linaweza kutokea,” alisema.

Ramadhani anazungumza kipato cha Sh8,000 kilivyo na changamoto kukidhi mahitaji yake, vipi yule wa Sh1,500?

Akizungumza na gazeti hili, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema kwa miaka zaidi ya 20 kumekuwa na uchumi mpana hapa nchini, lakini kinachoonekana ni kushindwa kuuhamishia kwenye uchumi mwembamba.

Alisema ukuaji wa uchumi mpana unapaswa ushushwe chini ndipo watu wa hali ya chini waweze kuinuka kimaisha.

“Hapa maana yake ukuaji wa uchumi ufanywe uwe jumuishi. Uchumi hata ukikua kwa asilimia 100, kama sio jumuishi basi kutakuwa na watu wachache wanaoufaidi na wengi wasioufaidi.”

Profesa Kinyondo alisema kinachopaswa kufanyika ili kuushusha uchumi chini, alishauri kuanzia kwenye kubadili elimu ambayo itawazalisha watu wanaoweza kujiajiri.

“Kuhakikisha mtu akitaka kuwa mjasiriamali mikopo inahitajika, mtu akitaka kuanzisha kampuni yake hapati changamoto yoyote,” alisema.

Alisema pia kikubwa ni kuwawezesha watu waliokwishaanza kujisimamia, ikiwemo kuwapa mitaji, akitolea mfano wakulima wasio na uwezo wa kumudu pembejeo waweze kushikwa mikono, vilevile wajasiriamali.

Alisema kufanya hivyo kutawezesha kuutoa uchumi juu na kuushusha chini na ndipo tutaweza kuumaliza umasikini.

Mchumi, Dk Mwinuka Lutengano kwa upande wake alisema, utolewaji wa msaada wa kifedha kupitia Tasaf bado una msaada sana kwa kaya maskini kutokana na hali za Watanzania wengi.

“Takwimu zinaonyesha lipo kundi ambalo limeendelea kutoka kwenye kundi la kaya maskini kupitia ujira mdogo wanaopewa. Kwa sasa yapo maboresho katika ujira, hasa kutolewa kwa kuhusisha ufanyaji wa kazi ambazo zinakuwa zimeibuliwa ndani ya kijiji (cash for work).

“Hili ni jema, maana linapunguza ile dhana ya uvivu ndani ya jamii. Ila ni vyema aina ya shughuli zinazoibuliwa zikawa zenye tija kwa kijiji na kwa kaya masikini ili kuwe na uendelevu wa ujuzi na maarifa,” alisema.

Dk Lutengano alisema tathimini za mara kwa mara ni nzuri ili kuhakikisha ujira unaotolewa unawafikia walengwa, hasa ambao ni kaya masikini. Na wale ambao si walengwa kuwekwa kando.

Pia alisema, ujira una msaada hasa kwa makundi maalumu ndani ya jamii, mfano wazee ambao wengi hawana kipato cha uzeeni kupitia mifuko ya hifadhi.


Maisha halisi ya kaya hizo

Karibu asilimia 37 ya kaya hukaa katika makao yenye paa zilizotengenezwa kwa nyasi, matope, au majani; asilimia 38 wana kuta zilizojengwa kwa miti, udongo, au nyasi na asilimia 78 wana sakafu zilizotengenezwa kwa mitende, mianzi, udongo, mchanga au samadi.

Kaya hizi kwa wastani zina vyumba viwili vya kulala na kaya moja pekee kati ya kumi inapata umeme, asilimia 65 wanatumia vyoo visivyo na ubora na asilimia 43 wanatumia vyanzo vya maji visivyo na ubora.

Kwa upande wa mawasiliano ya simu, asilimia 48 ya waliohojiwa wana simu za mkononi, na asilimia 10 wana redio. Kuhusu usafiri, si mtu yeyote aliye na gari, chini ya asilimia 1 wanamiliki pikipiki, na asilimia 9.4 wana baiskeli.

Pia, kaya nyingi hupata mapato kutokana na mavuno ya mazao (asilimia 56), wakati ni takriban asilimia 23 tu kati yao wana mapato kutokana na mishahara, asilimia 9 kutoka kwa biashara zisizo za mashambani, na asilimia 7 kutoka kwa mifugo na mazao ya mifugo.

Wakati wa kuangalia mapato yanayotokana na kila shughuli ya kiuchumi, kaya huzalisha Sh350,672 (Dola za Marekani 150.5) kila mwaka. Kati ya hizo, mapato mengi yanatokana na uzalishaji wa mazao (asilimia 81), ikifuatiwa na mishahara kutokana na kazi ya kulipwa (asilimia 10).

Mapato kutoka kwa biashara zisizo za mashambani na mifugo huchangia kidogo sana mapato ya kaya.

Kwa upande wa kazi, kaya zilivyotumia muda wao katika siku saba zilizopita. Katika kazi za nyumbani, hutumia muda mwingi kupika (saa 15), kutunza watoto na wazee (saa 14), na kuchota maji kwa saa 12.

Katika shughuli za kuzalisha mapato, asilimia 50 ya kaya zilifanya kazi kwenye shamba la familia, asilimia 22 zilifanya kazi kwa ujira, na asilimia 15 hufanya kazi za kujiajiri. Kaya walitumia saa 15 shambani, saa 7 kwa kazi ya kulipwa, na saa 4.6 kwa biashara ya kujiajiri kwa pamoja.



Sh1,500 hutumikaje?

Matokeo mengine ya utafiti huo yameonyesha kaya nyingi hutumia nafaka, mbogamboga na viungo, lakini chini ya asilimia 10 ya kaya zimeripoti kutumia nyama, maziwa na mayai katika siku saba zilizopita, na hivyo kuchangia kupunguza tofauti ya lishe.

Vilevile, kaya hizo zinakabiliwa na usalama duni wa chakula. Takriban kaya zote ziliripoti kukumbana na matukio kama kuhangaikia chakula, kuruka mlo, kula kidogo na kukosa chakula katika miezi 12 iliyopita.

Kwa mujibu wa tafsiri ya Benki ya Dunia, mtu aliyepo kundi la watu maskini ni yule asiye na uwezo wa kumudu mahitaji yake ya kila siku kwa kiwango kilichokubaliwa. Kwa sasa watu masikini ni wale ambao matumizi yao ya kila siku ni chini ya Dola za Marekani 1.9 (Sh4,826).