Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uzalishaji waongezeka, unywaji bado chini Tanzania

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka mikoa mbalimbali wakipatiwa mafunzo ya utengenezaji wa malisho bora kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026) yaliyofanyika Tanga.

Muktasari:

  • Serikali imebainisha mafanikio makubwa katika kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini kupitia mradi wa Maziwa Faida, huku ikikiri kuwa kiwango cha unywaji bado hakijafikia mahitaji. Wadau wametaka hatua zaidi kuchukuliwa ili kuimarisha soko, bei na uhamasishaji wa matumizi ya maziwa.

Tanga. Wakati Tanzania ikiendelea kupiga hatua katika kuongeza uzalishaji wa maziwa kupitia uwekezaji katika utafiti, teknolojia na ubunifu, changamoto ya unywaji mdogo wa maziwa bado inaibua maswali mapya kuhusu lishe, masoko na mustakabali wa sekta hiyo muhimu ya mifugo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele, amesema licha ya Tanzania kuzalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka, bado kiwango hicho hakitoshelezi mahitaji ya taifa yanayofikia lita bilioni 13 kwa mwaka.

Akizungumza jijini Tanga wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (Taliri Open Day 2026), Dk Madele amesema pengo hilo linaonesha wazi fursa kubwa ya uwekezaji zaidi katika sekta ya maziwa ili kuongeza uzalishaji na tija.

Amebainisha kuwa kupitia mradi wa Maziwa Faida, uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambapo wafugaji waliokuwa wakizalisha lita 3 hadi 5 kwa ng’ombe mmoja kwa siku sasa wamefikia wastani wa lita 15, hatua inayochangiwa na matumizi ya teknolojia bora, malisho na huduma za ugani.

“Pamoja na mafanikio hayo, kiwango cha unywaji wa maziwa nchini bado ni cha chini, kikifikia wastani wa lita 70 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na mapendekezo ya wataalamu wa lishe ya lita 200 kwa mwaka,” amesema Dk Madele.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele (mwenye kipazasauti), akifafanua matumizi ya teknolojia ya kunywesha ndama maziwa kwa kutumia kifaa maalumu na jinsi inavyoweza kuongeza ufanisi kwa wafugaji, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026). Picha na Mbonea Herman.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Suzanne Keatinge, amesema mafanikio ya Mradi wa Maziwa Faida yanaonesha wazi namna ushirikiano wa kimataifa unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Ameeleza kuwa uwekezaji wa zaidi ya euro milioni 3 katika kipindi cha miaka mitano umewezesha kuimarika kwa utafiti, uwezo wa wataalamu na kuongeza tija kwa wafugaji katika ukanda wa pwani.

“Tunajivunia kuona mabadiliko halisi kwa wafugaji na jamii. Ushirikiano huu umeonesha kuwa uwekezaji katika utafiti na watu unaweza kubadilisha maisha kwa haraka na kwa ufanisi,” amesema Keatinge.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taliri, Profesa Erick Komba, amesema mafanikio ya mradi huo yametokana na uwekezaji mkubwa katika tafiti na ushirikiano wa karibu kati ya watafiti, maafisa ugani na wafugaji.

Amebainisha kuwa kupitia mradi huo, Taliri imefanikiwa kuanzisha mashamba darasa, kuboresha miundombinu ya utafiti na kusambaza teknolojia zinazoongeza uzalishaji wa maziwa kwa ufanisi zaidi.

“Lengo letu ni kuhakikisha teknolojia hizi zinawafikia wafugaji wengi zaidi nchini ili kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa sekta ya maziwa,” amesema Profesa Komba.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Wadogo wa Ng’ombe wa Maziwa Wilaya ya Pangani, John Semnkande, amesema takwimu za uzalishaji zinaweza kuwa hazijakamilika kutokana na uwepo wa soko holela la maziwa nje ya mfumo rasmi.

Amesema changamoto za bei ndogo na ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa baadhi ya viwanda zinawasukuma wafugaji kuuza maziwa nje ya mfumo wa ushirika, hali inayodhoofisha ukusanyaji wa takwimu sahihi na maendeleo ya sekta.

Kwa upande wake, mfugaji Kimwinyi Waziri kutoka Pangani amesema kushuka kwa bei ya maziwa na ukosefu wa masoko ya uhakika kunawakatisha tamaa wafugaji wengi, baadhi yao wakihamia kwenye ufugaji wa nyama au shughuli nyingine kama bodaboda.

Naye Selina Michaeli kutoka Lushoto ameeleza kuwa ukame na ukosefu wa elimu ya uhifadhi wa maziwa vinachangia kupungua kwa uzalishaji, huku hali ngumu ya kiuchumi ikifanya familia nyingi kuuza maziwa yote badala ya kuyatumia kwa lishe.

Wadau hao wameitaka Serikali na washirika wa maendeleo kuimarisha masoko, kuongeza bei ya maziwa, kutoa elimu kwa wafugaji na kuhamasisha unywaji wa maziwa hususan mashuleni ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu na yenye manufaa kwa taifa.