Mageuzi ya sekta ya kilimo Pemba: Nguzo ya uchumi, usalama wa chakula na maendeleo
Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhandisi Idris Hassan (aliyesimama) akizungumza wakati wa zoezi la upandaji wa mikarafuu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Machi, 30 2026.
Sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa visiwa vya Zanzibar, hususan Pemba, ambako idadi kubwa ya wananchi hutegemea kilimo na mifugo kwa ajili ya kipato na chakula.
Katika miaka ya hivi karibuni, juhudi za makusudi zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia taasisi na idara mbalimbali ili kuimarisha sekta hii, kuongeza tija na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wananchi wa Pemba.
Juhudi hizo zimetokana na ushirikiano wa idara mbalimbali zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo Pemba ikiwemo; Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo, Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula, Idara ya Mifugo, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, Idara ya Misitu pamoja na Idara ya Umwagiliaji. Kupitia ushirikiano na juhudi zinazofanyika, sekta ya kilimo Pemba imeendelea kukua kwa kasi kutokana na mchango mkubwa wa idara hizo.
Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhandisi Idris Hassan (kushoto) akimchoma chanjo mbwa wakati alipozindua zoezi la chanjo za mifugo Pemba.
Ushirikiano wao umewezesha kuboresha uzalishaji, kuongeza tija na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha kwa wananchi. Hii imeifanya Pemba kuwa na fursa kubwa ya kuwa kitovu cha kilimo bora na endelevu.
Katika kisiwa hicho, sekta ya kilimo si tu chanzo cha chakula bali pia ni msingi wa uchumi na ustawi wa jamii ambapo kupitia uwekezaji endelevu, ubunifu na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wananchi, ndoto ya kujitosheleza kwa chakula na kukuza uchumi wa Pemba inaweza kufikiwa kwa urahisi.
Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo
Katika juhudi za kuleta mapinduzi ya kilimo cha kisasa, Serikali imeanzisha Wakala wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo Pemba, ambao una jukumu la kusambaza na kusimamia matumizi ya zana za kisasa za kilimo kwa wakulima. Wakala huu umeleta mabadiliko makubwa kwa kupunguza utegemezi wa nguvu kazi ya mikono na kuongeza kasi ya uzalishaji.
Kupitia wakala huu, wakulima wameweza kupata huduma za trekta kwa gharama nafuu, jambo ambalo limeongeza eneo la kilimo na kupunguza muda wa maandalizi ya mashamba. Aidha, wakala umefanikiwa kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya zana za kisasa, hali iliyochangia kuongeza tija na ubora wa mazao.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya huduma za matrekta katika maeneo mbalimbali ya Pemba, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wakulima wengi zaidi.
Hii imeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo. Kwa Pemba, wakala umejipambanua kama chachu ya mageuzi ya kilimo cha kisasa.
Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula
Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula Pemba ina jukumu la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata chakula cha kutosha, salama na chenye lishe bora.
Idara hii imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sera na mipango ya uzalishaji wa mazao ya kilimo, pamoja na kutoa elimu kwa wakulima juu ya mbinu bora za kilimo. Kupitia programu mbalimbali, idara imehamasisha matumizi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu salama, hali iliyosaidia kuongeza mavuno na kupunguza upotevu wa mazao.
Vilevile, imekuwa ikisimamia uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna kwa kuhimiza matumizi ya maghala bora na teknolojia za kisasa za kuhifadhi chakula.
Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhandisi Idris Hassan akifanya mahojiano na Gazeti la Mwananchi ofsini kwake Weni, Pemba.
Aidha, kupitia tafiti na ufuatiliaji wa karibu, idara imeweza kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kuzitatua kwa wakati. Pia imeanzisha programu mbalimbali za kuhifadhi chakula ili kukabiliana na upungufu unaoweza kujitokeza katika misimu isiyo na mvua ya kutosha.
Matokeo yake ni kupungua kwa uhaba wa chakula na kuimarika kwa lishe kwa wananchi wa Pemba. Pia, katika kuhakikisha usalama wa chakula, idara imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula katika maeneo mbalimbali ya Peba.
Hatua hii imewezesha kuchukua hatua za haraka pale panapotokea uhaba wa chakula, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa mazao mbadala na kusambaza chakula katika maeneo yaliyoathirika.
Idara ya Mifugo
Sekta ya mifugo ni mhimili mwingine muhimu katika uchumi wa Pemba, na Idara ya Mifugo imekuwa na mchango mkubwa katika kuikuza. Idara hii inalenga kuongeza tija kwa wafugaji kwa kuboresha huduma za mifugo, ikiwa ni pamoja na afya ya mifugo, lishe bora na mbinu za kisasa za ufugaji.
Kupitia kampeni za chanjo na matibabu ya mifugo, idara imefanikiwa kupunguza magonjwa yanayoathiri mifugo, hivyo kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na bidhaa nyingine za mifugo. Aidha, imekuwa ikitoa mafunzo kwa wafugaji juu ya ufugaji wa kisasa, ikiwa ni pamoja na ufugaji wa kuku wa kisasa, ng’ombe wa maziwa na mbuzi.
Idara pia imehamasisha uanzishwaji wa vikundi vya wafugaji, ambavyo vinawawezesha kupata mikopo, masoko na huduma za kitaalamu kwa urahisi zaidi. Hii imeongeza kipato cha wafugaji na kuchangia kuboresha maisha yao.
Kupitia juhudi hizi, uzalishaji wa maziwa, nyama na bidhaa nyingine za mifugo umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Vilevile, idara imehamasisha matumizi ya teknolojia katika ufugaji, kama vile uboreshaji wa malisho na matumizi ya vifaa vya kisasa katika uzalishaji. Hali hii imechangia kuongeza kipato cha wafugaji na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
Maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kufikiwa bila uwepo wa mipango madhubuti, sera sahihi na tafiti zinazoendana na mahitaji halisi ya wakulima. Idara ya Mipango, Sera na Utafiti imekuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo Pemba inaongozwa na mikakati inayozingatia ushahidi wa kisayansi na mahitaji ya soko.
Idara hii imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali kuhusu mazao yanayofaa kulimwa katika mazingira ya Pemba, pamoja na mbinu bora za uzalishaji. Matokeo ya tafiti hizi yamekuwa yakitumika kuboresha sera na mipango ya kilimo, hivyo kuongeza ufanisi na tija.
Aidha, idara imekuwa ikiratibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo, ikihakikisha kuwa rasilimali zinatumika kwa ufanisi na malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa. Ushirikiano na wadau wa maendeleo, taasisi za utafiti na sekta binafsi umeendelea kuimarishwa kupitia idara hii.
Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhandisi Idris Hassan akishiriki zoezi la kupanda miti katika Hifadhi ya Msitu wa Ngezi Vumawimbi, Makangale, Wilaya ya Micheweni Pemba wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Aidha, idara imekuwa sehemu muhimu katika kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kwa msingi wa kisayansi na kimkakati. Idara hii inahusika na uandaaji wa sera, mipango ya maendeleo na tafiti zinazo-lenga kuboresha kilimo.
Kupitia tafiti zake, imeweza kutoa mapendekezo yanayosaidia kuongeza tija na kukabiliana na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi. Pia imekuwa kiunganishi kati ya wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hivyo basi, mchango wa idara hii unaonekana katika uwepo wa mipango thabiti inayosukuma mbele maendeleo ya kilimo Pemba.
Idara ya Misitu
Uhifadhi wa mazingira ni jambo muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa sekta ya kilimo. Idara ya Misitu Pemba imekuwa na jukumu la kusimamia rasilimali za misitu na kuhakikisha zinatumika kwa njia endelevu.
Kupitia juhudi za upandaji miti na uhifadhi wa misitu ya asili, idara imechangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda vyanzo vya maji na kuboresha rutuba ya udongo.
Misitu pia imekuwa chanzo cha mapato kupitia utalii wa ikolojia, ambapo wageni huvutiwa na mandhari ya asili ya Pemba. Zaidi ya hayo, idara imekuwa ikielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu.
Hii imechangia kubadili mitazamo ya wananchi na kuongeza ushiriki wao katika uhifadhi wa mazingira. Kwa upande wa mazingira, Idara ya Misitu Pemba imekuwa na jukumu la kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu, ambazo ni muhimu kwa uendelevu wa kilimo na uchumi kwa ujumla.
Misitu huchangia katika kudhibiti hali ya hewa, kuhifadhi maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Idara pia imeanzisha programu za upandaji miti, kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa misitu, na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali hizi. Mbali na hilo, misitu ya Pemba imekuwa kivutio cha utalii, jambo linalochangia kuongeza mapato ya serikali na wananchi.
Idara ya Umwagiliaji
Mabadiliko ya tabianchi yameleta changamoto kubwa katika uzalishaji wa kilimo, hasa kutokana na kutokuwa na uhakika wa mvua. Katika kukabiliana na changamoto hii, Idara ya Umwagiliaji Pemba imekuwa ikitekeleza miradi ya umwagiliaji ili kuhakikisha uzalishaji wa mazao unaende-lea mwaka mzima.
Kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, wakulima wameweza kulima zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka, hali iliyoongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa chakula kutoka nje.
Idara pia imekuwa ikitoa mafunzo kwa wakulima juu ya matumizi bora ya maji na teknolojia za umwagiliaji. Miradi ya umwagiliaji imechangia pia kuongeza ajira na kipato kwa wananchi, kwani imewezesha kilimo cha kibiashara cha mazao kama mboga, matunda, mpunga na viungo.
Maendeleo ya sekta ya kilimo Pemba ni matokeo ya juhudi za pamoja za Serikali kupitia taasisi na idara mbalimbali pamoja na ushirikiano wa wananchi. Kuanzia matumizi ya zana za kisasa, uhakika wa chakula, maendeleo ya mifugo, tafiti na sera, uhifadhi wa mazingira hadi miradi ya umwagiliaji kila sekta imekuwa na mchango muhimu katika kuimarisha kilimo.
Hata hivyo, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masoko ya uhakika, mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa rasilimali. Ni muhimu kuendelea kuwekeza katika teknolojia, elimu na miundombinu ili kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo Pemba inaendelea kukua na kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Kwa kuzingatia juhudi zinazoendelea, ni wazi kuwa Pemba ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa kilimo endelevu, chenye uwezo wa kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza kipato kwa wananchi wake.
Nafasi ya ZALIRI katika kukuza klilimo na kuongeza tija kwa wafugaji Pemba
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo na Kilimo Zanzibar (ZALIRI), ikiwa ni mkono wa kitaalamu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Mali Asili na Mifugo, imekuwa na mchango mkubwa katika kubadilisha sura ya kilimo Zanzibar, hususan katika kisiwa cha Pemba.
Kupitia mbinu za kisayansi na tafiti shirikishi, taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya msingi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuongeza tija kwa mkulima. Jukumu kuu la taasisi hii limekuwa ni kufanya tafiti za mbegu na mbinu bora za kilimo zinazostahimili changamoto za sasa kama ukame na wadudu.
Taasisi inashirikiana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi, ikiwemo vyuo vikuu kufanya tafiti za kina. Kazi hii inahusisha utambuzi wa mimea ya kipekee duniani inayopatikana kisiwani humo na jinsi ya kuilinda dhidi ya uvamizi wa binadamu. Hii imefanya taasisi hiyo kupata mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo na ufugaji.
Moja ya mafanikio hayo ni usambazaji wa mbegu mpya za mpunga zinazostahimili ukame ambapo katika msimu uliopita wa vuli ambao ulikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa mvua, mbegu hizi zimeleta mapinduzi kwa kuruhusu wakulima kuvuna magunia mengi (hadi magunia nane kwa eneo dogo) tofauti na mbegu za asili.
Kutokana na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo kwa upande wa Pemba kumeshuhudiwa mwamko mkubwa wa vijana kujiingiza katika kilimo cha mboga na matunda (horticulture) kutokana na mwongozo wa kitaalamu na ruzuku za Serikali.
Mafanikio haya yameonekana kupitia uzalishaji mkubwa wa matikiti na mazao mengine ya biashara ambayo sasa yanatosheleza mahitaji ya soko la ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Vijana wengi Pemba sasa wanaendesha maisha yao kupi-tia tija inayopatikana shambani.
Wito unatolewa kwa jamii na wawekezaji kuendelea kuunga mkono juhudi hizi za kitafiti ili kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.