Viwanda vya magari vinavyozidi kuchangamkia fursa Tanzania
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo wakati akizindua uuzaji wa magari yaje nchini kupitia Shacman. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kutafuta njia za kukabiliana na athari za ongezeko la bei za mafuta katika shughuli za uchumi na usafirishaji, viwanda vya magari vimeendelea kuona fursa ya kuzalisha magari yanayotumia nishati mbadala ikiwamo umeme.
Hiyo ni baada ya kampuni ya Mansour Group kuanza majadiliano na Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TiSEZA) kuhusu mpango wa kuanzisha kiwanda cha kuunganisha malori ya kisasa yatakayotumia umeme kwa kiwango kikubwa zaidi huku yakitegemea mafuta kwa kiwango kidogo.
Kiwanda hicho kinachotarajiwa kugharimu zaidi ya dola milioni 30 za Marekani (Sh78.696 bilioni) kinatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kampuni hiyo wa kuwekeza katika sekta ya usafirishaji na viwanda nchini Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mansour Automotive, Ankush Arora alibainisha hayo jana usiku wakati ikizindua uuzaji wa magari yaje nchini kupitia Shacman.
Arora amesema wanaendelea na mazungumzo na TiSEZA ili kupata vivutio vya uwekezaji vitakavyowezesha utekelezaji wa mradi huo.
Alisema Tanzania imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutokana na nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini pamoja na maboresho makubwa ya miundombinu yanayoendelea kufanywa na Serikali.
“Tunaiona Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa ukanda mzima. Hii ndiyo sababu tumedhamiria kufanya uwekezaji wa muda mrefu unaojumuisha vituo vya huduma, maghala ya vipuri na hatimaye uzalishaji wa magari nchini,” alisema.
“Hili litafanyika baada ya kumaliza majadiliano kati yetu na Tiseza na bodi ya wakurugenzi wa kampuni yetu, pindi tutakapoweka kila kitu sawa tunatarajia ndani ya miezi 18,” alisema.
Arora anasema kwa sasa kampuni hiyo pia inapanga kufungua vituo 10 vya huduma nchini ndani ya miezi 18 hadi 24 ijayo, huku vituo vitano vikitarajiwa kuanza kazi kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Uwekezaji huo unakuja wakati Serikali ikiendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kupitia Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa bandari kavu katika maeneo ya Kwala, Morogoro, Ihumwa, Isaka na Tabora.
“Hatujaja Tanzania kwa ajili ya kuuza malori pekee. Tunataka kuwa mshirika wa muda mrefu katika sekta za usafirishaji, viwanda na biashara. Tunaona fursa kubwa zinazotokana na ukuaji wa uchumi na uwekezaji wa miundombinu unaoendelea nchini, aliseme.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo alisema uwekezaji unaolenga kufanywa na Mansour utasaidia katika kuongeza idadi ya ajira kwa watanzania huku ukichangia ukuaji wa pato la Taifa kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.
Anasema uunganishaji wa malori yanayotumia umeme kwa kiasi kikubwa pia utaleta urahisi katika usafirishaji mizigo ya gharama nafuu bila kutumia nishati ya mafuta.
Hili ni muhimu hivi sasa wakati ambao ongezeko la mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam kufuatia maboresho ya miundombinu yaliyofanyika limeongeza mahitaji ya vituo vya kuhifadhi na kusambaza mizigo nje ya Dar es Salaam.
Alisema kutokana na kuongezeka kwa mizigo, Serikali imeamua kuwekeza katika mfumo wa kisasa wa usafirishaji unaounganisha Reli ya Kisasa (SGR) na bandari kavu katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha usafirishaji wa makasha kutoka bandarini kwenda kwa watumiaji na nchi jirani.
“Uwekezaji huo unaendana na juhudi nyingine za Serikali za kuboresha usafirishaji wa mizigo, ikiwamo upanuzi wa barabara za Kibaha–Chalinze, Chalinze–Morogoro na Morogoro–Dodoma pamoja na mpango wa kujenga barabara ya mwendokasi kati ya Dar es Salaam na Morogoro,” alisema.
Alisema sehemu ya changamoto ya msongamano inatokana na ongezeko la mizigo bandarini huku miundombinu ya kuhifadhi makasha ikiwa imejikita zaidi Dar es Salaam.
“Bandari kavu za Kwala, Morogoro, Ihumwa, Isaka na Tabora zitakapokamilika, makasha yatahamishwa moja kwa moja kutoka bandarini kwenda katika vituo hivyo kwa kutumia SGR, jambo litakalopunguza idadi ya malori yanayoingia na kutoka bandarini,” alisema.