Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachimbaji na kilio cha ongezeko la bei ya mafuta

Wakati dunia ikishuhudia hatua mpya ya tahadhari na matumaini katika mvutano wa Mashariki ya Kati kufuatia makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran, macho ya wachumi na wawekezaji yameelekezwa katika mwelekeo wa bei za mafuta duniani.

Ingawa hatua hiyo imeanza kupunguza presha ya soko la nishati kimataifa, athari zake bado zinaendelea kuiumiza sekta nyeti katika nchi zinazoagiza mafuta, ikiwamo Tanzania.

Awali, ilionekana kuwa nafuu ingedumu lakini kukwama kwa mazungumzo ya pande mbili zinazovutana kunaweza kurefusha hali hiyo tete.

Kwa wachimbaji wadogo wa madini ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za mtaji na teknolojia, kupanda kwa bei za mafuta kumekuwa pigo kubwa linalotikisa uhai wa shughuli zao za kila siku.

Licha ya matumaini mapya yanayochochewa na ishara za kupungua kwa mvutano wa kisiasa Mashariki ya Kati, hali halisi mashinani bado ni ngumu.

Ongezeko la bei za mafuta nchini lilithibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kupitia tangazo lake la Aprili 2, 2026, lililopandisha bei za petroli na dizeli katika maeneo mbalimbali.

Katika Mkoa wa Geita, kitovu muhimu cha uzalishaji wa dhahabu, bei zimefikia viwango vinavyobana shughuli za uzalishaji.

Kwa mujibu wa bei hizo mpya, petroli katika Manispaa ya Geita imepanda kutoka Sh3,064 hadi Sh4,020 kwa lita, huku dizeli ikipanda kutoka Sh3,059 hadi Sh4,006.

Katika Wilaya ya Mbogwe, hali ni mbaya zaidi, Petroli imefikia Sh4,058 na dizeli Sh4,044 kwa lita.


Gharama zilivyopanda

kwa wachimbaji wadogo, mafuta si gharama ya pembeni bali ni mhimili wa uzalishaji wao. Kuanzia uchimbaji, usafirishaji wa mchanga, hadi usindikaji wa madini, kila hatua inategemea nishati hiyo.

Masabire Modest, mchimbaji katika migodi ya Mgusu na Nyarugusu, anasema hata wale wanaotumia umeme hawaepuki athari hizo kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji.

“Gharama za kukodi gari zimepanda sana. Kama ulikuwa unalipa Sh500,000 sasa unalazimika kulipa hadi Sh700,000 au zaidi, bila hata kujumlisha posho ya dereva,” anasema.

Anaongeza kuwa hata mafuta yenyewe yamepanda kwa kiwango kikubwa, lita tano za dizeli zilizokuwa zikinunuliwa kwa Sh16,000 hadi Sh17,000 sasa zimefikia Sh22,000.

Wachambuzi wa sekta ya madini wanasema hali hii inapunguza faida na kuongeza hatari ya kufilisika kwa wachimbaji wadogo, ambao mara nyingi huendesha shughuli zao kwa mtaji mdogo na mikopo isiyo rasmi.


Wengine wasitisha uchimbaji

Kwa baadhi ya wachimbaji kutokana na hali hiyo, wamefikia hatua ya kusimamisha shughuli zao za uchimbaji.

Asia Masimba, mchimbaji wa Mgodi wa Matabe wilayani Chato, mkoani Geita anasema hawezi tena kumudu gharama za uzalishaji.

“Nauli ya kwenda mgodini imepanda kutoka Sh10,000 hadi Sh30,000. Hii pekee inanifanya nishindwe hata kufika eneo la kazi. Kwa sasa nimesimama kabisa,” anasema.

Hali kama hiyo inaashiria hatari ya kupungua kwa uzalishaji wa madini nchini, jambo linaloweza kuathiri mapato ya Serikali na mnyororo mzima wa uchumi unaotegemea sekta hiyo ya madini.


Masika nayo yawaongezea maumivu

Wakati huo huo, msimu wa mvua umeongeza mzigo kwa wachimbaji. Ili kuendelea na uchimbaji, hivi sasa wanasema wanalazimika kutumia jenereta kuvuta maji kwenye mashimo, hali inayoongeza matumizi ya mafuta.

Bunga Dadu, Katibu wa wachimbaji wadogo katika Mkoa wa kimadini Mbogwe, anasema gharama zimeongezeka maradufu.

“Hapo awali tulikuwa tunatumia Sh100,000 hadi Sh200,000 kuvuta maji duarani. Sasa kiwango cha chini ni Sh200,000 au zaidi,” anasema.

na kuongeza;

“Unatumia mafuta kila hatua kuanzia kuvuta maji, kusaga mawe hadi kusafirisha. Hata kama dhahabu imepanda bei, bado gharama hizi zinakula faida yote.”


Umeme wa uhakika watakiwa

Baadhi ya wachimbaji waliozungumzia kadhia hiyo wanaona suluhisho la kudumu liko kwenye uwekezaji wa miundombinu ya umeme katika maeneo ya migodi wakisema utapunguza utegemezi wa mafuta.

Sospeter Samweli, mchimbaji wa Matabe anasema gharama zimekuwa kubwa kupita kiasi.

“Dumu la petroli la lita 20 lilikuwa likiuzwa kwa Sh64,000, sasa limefika Sh85,000. Umeme ungepunguza mzigo huu,” anasema.

Anaonya kuwa kusimama kwa uchimbaji kunaweza pia kusababisha baadhi ya wachimbaji kupoteza leseni kutokana na kushindwa kuendeleza maeneo yao kwa muda mrefu.


Jicho lote kwa Serikali

Kutokana na sekta ya madini kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania ikichangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa, changamoto za gharama za uzalishaji zinaweka malengo ya ukuaji katika hatari.

Inaelezwa kwamba kuporomoka kwa shughuli za wachimbaji wadogo kunaweza kuathiri ajira, mapato ya Serikali na ustawi wa jamii zinazotegemea shughuli hizo.

Hivyo, wachimbaji wanaiomba Serikali kuingilia kati kwa kuweka sera nafuu, ruzuku au kuharakisha uwekezaji katika nishati mbadala kama gesi asilia na umeme.

“Tunahitaji mazingira rafiki ya uzalishaji. Bila hivyo, hata kama soko la dhahabu ni zuri, hatutaweza kunufaika nalo,” anasema Dadu.

Kwa upande wake, Rais wa wachimbaji wadogo nchini, John Bina anasisitiza nidhamu ya fedha kama ngao dhidi ya mishtuko ya kimataifa.

“Majanga ya kidunia hayaepukiki. Ni muhimu kuweka akiba ili kuhimili vipindi kama hivi,” anasema.

Hata hivyo, anatoa matumaini kuwa hali inaweza kuanza kuimarika iwapo utulivu wa kisiasa Mashariki ya Kati utaendelea na kusababisha bei za mafuta kushuka zaidi.