Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara watema nyongo, Dk Jafo awapa ahadi

Waziri wa Viwanda na Biashaara, Dk Selemani Jafo akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya biashara nchini uliyofanyika jijini Dar es Saalam. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Wadau na wafanyabiashara wa sekta mbalimbali wamempa kero mbalimbali Waziri  wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo, wakimueleza kuwa zinawasumbua na kukwamisha shughuli zao.

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imempokea Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Seleman Jafo kwa zigo la kero wanazodai zinakwamisha kukua kwa biashara zao.

Hata hivyo, Dk Jafo amewaahidi kuzifanyia kazi kero na changamoto zilizofikishwa na wadau, kwa mustakabali wa kukuza biashara na kuleta maendeleo nchini.

Miongoni mwa kero walizoziwasilisha ni pamoja na utitiri wa taasisi zinazotoza tozo mbalimbali, ushuru, kodi hasa ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), akaunti za wafanyabiashara kufungwa, kutolindwa kwa viwanda vya ndani na viwanda kufungiwa.

Wametoa kilio hicho, jana Ijumaa Julai 12, 2024 katika kikao cha kwanza na Dk Jafo aliyeteuliwa Julai 2 kushika nafasi hiyo, akichukua mikoba ya Dk Ashatu Kijaji aliyepelekwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Paul Makanza amesema kwa muda mrefu wazalishaji wa vinywaji vya kusisimua misuli,  wamekuwa wakitumia HS Code 2602.10.00 ambayo ushuru wake ni Sh91 kwa lita, hata hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania imewaambia HS Code siyo sahihi.

“Wametuambia tutumie mpya ambayo ni gharama yake ni Sh561 hii itaathiri gharama za uendeshaji. Mapendekezo yetu tunaomba tukutane na TRA ili kupata ufumbuzi wa hili, maana athari zake kodi ikitozwa uzalishaji utapungua,” amesema Makanza.

“CTI hatuna tatizo la ulipaji wa kodi, lakini kodi zinavyotozwa kwa kutumia taasisi mbalimbali zinapodai na  kufunga kiwanda. Unapodai na kufunga kiwanda maana yake unaua uwezo wa unayemdai.

“Mara nyingine unaamka asubuhi unakuta akaunti zimefungwa juu kwa juu, biashara zinasimama, katika hili tunaomba ufungaji wa akaunti za wafanyabiashara usiendelee bali kuwepo na uhakiki wa uhakika kwamba kodi inayodaiwa ni sahihi,” amesema Makanza.

Mfanyabiashara Haidary Gulamali, amemwambia Dk Jafo wingi wa utitiri wa taasisi za Serikali, umekuwa ukiwapa wakati mgumu akitolea mfano Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) akidai inakwenda katika ofisi yake kwa lengo la kupima afya za wafanyakazi.

“Wakija bei wanapanga wenyewe, wanakuja na madaktari sasa kwa nini sisi tusipeleke wafanyakazi hawa katika hospitali kupima afya zao, kisha kuwapa vyeti Osha badala ya wao kuja katika ofisi zetu.

“Sijui wanapima nini presha au? maana wanapimia eneo la kazi,” amehoji Gulamali ambaye ni mzalishaji wa magodoro Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Precision Air, Patrick Mwanri aliomba tozo katika taasisi mbalimbali ziangaliwe upya na kuratibiwa vema, huku akiinyoshea kidole Osha ambayo ilikwenda katika ofisi yake katika suala la matibabu.

Mwanzilishi wa Umoja wa Waoka Mikate Tanzania, Lilian Kisanga ameomuomba Dk Jafo kuangalia upya suala VAT katika bidhaa hiyo, akisema linawarudisha nyuma wajasiriamali wanaojishughulisha na bidhaa za mikate.

“Hii sekta imebeba watu wengi, lakini pia tunashindwa kuwa wabunifu au kujiongeza kwa sababu ya VAT tusaidie Dk Jafo,” amesema Kisanga.

Naye, mdau wa biashara kwa njia ya dijitali kutoka kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore, amemuomba Dk Jafo kuitupia jicho sekta hiyo kwa sababu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi.

“Sekta hii haitambuliki kama wafanyabiashara bali tunajulikana kama mafundi. Tunaomba Dk Jafo aangalie kwa mapana zaidi mustakabali wetu wa baadaye tunakwendaje kama wafanyabiashara wa kidijitali,” amesema Wilmore ambaye ni Makamu wa Rais wa Airpay anayesimamia mikakati.

Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula amesema wafanyabiashara wanakumbana na changamoto zingine za matumizi ya kikosi kazi katika ukusanyaji wa kodi na tozo, kuongezeka kwa bidhaa za magendo kunakotishia viwanda vya ndani na kufungiwa kwa mashine za EFD.

Awali Dk Jafo amesema amekutana na wadau hao, kujadili changamoto zinazowakabili ili kupata ufumbuzi na kuongea lugha moja kama Taifa kwa lengo la kuleta maendeleo na kuzalisha ajira kwa vijana.

“Katika kipindi hiki tushirikiane kwa pamoja kuondoa vikwazo na changamoto mbalimbali, ili biashara ikafanye vizuri na kukuza mapato ya nchi kukua. Hakuna mwingine wa kulifanya ni sisi hapa.

“Shauku yangu kuona biashara zinafanya vizuri na biashara zingine zinafanya vizuri pia ili tuwe Taifa lenye ushindani. Kazi yangu ni kupokea kero zenu na kuzipangilia vema kwa ajili ya utatuzi,” amesema Dk Jafo.

Mbali na hilo, Dk Jafo amewataka wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kupendana kwa maendeleo ya Taifa siyo kufanyia mambo ambayo kwa namna moja au yanalenga kuwadidimiza baadhi yao.

“Niwaombe sana wafanyabiashara, wakati mwingine tunapigana sisi kwa sisi, inawezekana unafanya jambo la kumdhuru mfanyabiashara.”

“Inawezekana mwenye kiwanda X na mwingine Y wanafanya shughuli tofauti lakini mmoja wao akamhujumu mwenzake ili asiendelee, sitamani kuona viwanda vikifungwa au kutoendelea,” amesema Dk Jafo.


Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.