Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima 200 wa mwani Zanzibar wanufaika na Kilimo Mkataba

Wanawake wa Kijiji cha Muungoni wakiwa katika zoezi la kusaini mikataba ya kushiriki katika Mradi wa Kilimo cha Mkataba wa mwani unaotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa ufadhili wa The Big Heart Foundation, wenye lengo la kuongeza uzalishaji wa mwani, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi wa buluu katika eneo la Zanzibar.

Muktasari:

  • Sekta ya mwani Zanzibar inakadiriwa kuajiri zaidi ya watu 26,000, huku wanawake wakichangia zaidi ya asilimia 80 ya nguvu kazi yote.

Dar es Salaam. Wakulima wa mwani wapatao 200 kutoka Shehia za Uzi na Muungoni, Zanzibar, wameanza kunufaika na mradi wa Kilimo Mkataba, mradi unaolenga kuongeza uzalishaji, kuboresha masoko na kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu visiwani humo.

Mradi huo unaotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa ufadhili wa The Big Heart Foundation kupitia mradi wa Seaweed Social Enterprise Project (SESEP), umeanza rasmi utekelezaji wake huku ukilenga kuinua kipato cha wakulima wadogo, hasa wanawake na vijana.

Taarifa iliyotolewa na ZMBF leo Mei 9, 2026 imeeleza kuwa kati ya wakulima wanaonufaika, wanawake ni 175 sawa na asilimia 88, huku wanaume wakiwa 25 sawa na asilimia 12.

Aidha, vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 ni 51, sawa na asilimia 26 ya wanufaika wote.

Kupitia mfumo wa Kilimo Mkataba, wakulima watapatiwa pembejeo bora, zana za kisasa pamoja na mafunzo ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mwani.

Mradi huo pia unalenga kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa zao la mwani kwa kuweka huduma za kuchakata mazao baada ya kuvuna, kuongeza thamani na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ZMBF, hatua hiyo itasaidia kuondoa changamoto ya wakulima kutegemea wafanyabiashara wadogo wanaowakopesha pembejeo kwa masharti magumu, hali ambayo imekuwa ikipunguza kipato chao kwa muda mrefu.

Katika utekelezaji wa mradi huo, kilo moja ya mwani mbichi itanunuliwa kwa Sh250, jambo ambalo linatajwa kuwa litasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi bila kulazimika kuanika na kuhifadhi mwani katika mazingira yasiyo rasmi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Shehia ya Uzi, Othman Haji amesema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wakulima wa eneo hilo.

“Kwa sasa tunapata pembejeo kwa wakati na tuna uhakika wa soko pamoja na bei nzuri. Wanawake ambao ndio wengi katika shughuli za kilimo cha mwani wataweza kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao,” amesema.

Naye Sheha wa Muungoni, Mussa Mbwato amesema vijana wengi wameanza kuvutiwa na kilimo cha kisasa cha mwani kutokana na fursa zinazotolewa kupitia mradi huo.

“Tunashuhudia ongezeko la uzalishaji na thamani ya mazao yetu. Vijana sasa wanaona kilimo cha mwani kama biashara yenye mustakabali mzuri wa kiuchumi,” amesema.

Mratibu wa mradi kutoka ZMBF, Titus Lukurazo amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Amesema lengo kuu ni kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia kilimo cha mwani kama biashara endelevu inayoweza kuongeza mapato ya kaya na kuchangia ukuaji wa uchumi wa buluu Zanzibar.

“Tunawapa wakulima zana, maarifa na masoko ili waweze kubadilisha shughuli zao za kawaida kuwa biashara halisi zinazozalisha mapato ya uhakika,” amesema Lukurazo.

Mbali na kuwasaidia wakulima mmoja mmoja, mradi huo pia unatarajia kuanzisha vituo vya kuchakata mwani, kuunda Jukwaa la Taifa la Wakulima wa Mwani pamoja na mifumo ya usambazaji na mfuko wa maendeleo ya masoko ili kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo.

Sekta ya mwani Zanzibar inakadiriwa kuajiri zaidi ya watu 26,000, huku wanawake wakichangia zaidi ya asilimia 80 ya nguvu kazi yote. Kupitia mradi wa SESEP, wadau wanaamini sekta hiyo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato kwa wananchi pamoja na kuongeza mchango wa uchumi wa buluu katika pato la taifa.

ZMBF imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wadogo wanapata fursa za ushindani katika soko na kuboresha maisha yao kupitia kilimo cha mwani chenye tija na endelevu.