Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaoficha mafuta kukiona, ununuzi waongezeka

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam,baada ya kufanya ziara katika baadhi ya hifadhi na vituo vya mafuta leo,kulia ni Mkurugenzi Mkuu EURA,Dk James Andilile.Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Serikali imeonya juu ya wafanyabiashara kuficha mafuta, ikihakikisha usambazaji, bei himilivu, na akiba ya kutosha ya nishati hiyo hadi Julai.


Dar es Salaam. Wakati hofu juu ya kuadimika na kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na vita Mashariki ya Kati ikiendelea kuibuka, Serikali imeonya wafanyabiashara kuepuka kuficha bidhaa hiyo na kuuza kwa bei ghali.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dk James Mataragio, alipokuwa akifanya ziara katika baadhi ya hifadhi na vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam leo Jumatano Machi 25, 2026, kwa lengo la kukagua akiba za mafuta na kuhakikisha usambazaji unafanyika bila ucheleweshaji.

“Dhumuni la ziara yetu ni kuangalia stock tulizonazo. Tumepokea taarifa za ucheleweshaji wa kufikishwa kwa mafuta, kwamba malori yanayopakia yanachelewa huku TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wakilaumiwa kuchelewesha vibali,” amesema Dk Mataragio.

Aidha, amesisitiza Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya kampuni itakayoficha mafuta ili iwauzie watanzania kwa bei ghali ijinufaishe na vita vinavyosababisha hofu ya kuadimika kwa nishati hiyo.

“Hatutaki wafanyabiashara watumie fursa ya tatizo lililopo kuficha mafuta ili wauze kwa bei ghali. Serikali hatutasita kuchukua hatua; hii ni uhujumu uchumi,” ameongeza.

Katika ziara hiyo kwenye kituo cha mafuta cha Camel Oil jijini Dar ea Salaam, Meneja Mkuu wa Camel Oil, Saleh Bajber amesema kampuni hiyo inahifadhi ya kutosha kwa miezi miwili ijayo hata kama haitaweza kuagiza mengine.

 “Tumeagiza lita milioni 70 kwa ajili yetu na milioni 84 kwa mtandao wetu. Kwa mwezi huu tayari tumeshasambaza lita milioni 44," amesema.

Bajber amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la mauzo ya mafuta nchini akifichua kuwa limechangiwa na hofu ya wananchi, ambao wameongeza manunuzi yao zaidi ya kawaida.

Akizungumzia hatua hiyo, Dk Mataragio amewatahadharisha wananchi juu ya hofu zisizo za lazima, akiwataka kuacha kununua mafuta kwa hofu na kuyahifadhi ndani akisema hali hiyo ndiyo inayoweza kusababisha kupungua kwa mafuta sokoni.

“Tunawaasa wananchi kwamba hakuna haja ya kupaniki kununua mafuta mengi wala kuficha mafuta. Mafuta tunayo mengi sana,” amesema, akisisitiza uhakika wa upatikanaji wa mafuta.

Dk Mataragio amesema Serikali tayari imejipanga kwa akiba ya mafuta ya hadi mwezi Julai 2026, na itaendelea kuongeza akiba kulingana na hali ya vita Mashariki ya Kati.

“Hakuna anayejua vita vitamalizika lini, hivyo tutaendelea kuweka mikakati zaidi ila kwa sasa tunayo akiba ya kutosha mpaka mwezi Julai,” amesema.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu huyo ameweka wazi kuwa Serikali inafuatilia kila hatua ya usambazaji wa mafuta nchini, akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayejaribu kuficha bidhaa hiyo na akibainika atachukuliwa hatua kama mhujumu uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Dk James Andilile amebainisha Camel Oil ni mdau muhimu katika usambazaji wa mafuta nchini, akisisitiza juu ya Watanzania kuamini na kufuata maelekezo ya Serikali kuhusu upatikanaji wa mafuta nchini na kuacha kuyanunua kwa wingi na kuyahifadhi ndani.

 Dk Andilile amefafanua vita Mashariki ya Kati vimechangia changamoto za upatikanaji wa mafuta, lakini hatua za mapema za Serikali zimesaidia kuhakikisha hakuna upungufu kwa sasa na kwa miezi kadhaa baadaye hata kama hali itaendelea kuwa tete.

“Upatikanaji wa mafuta umeathirika kwa sababu tunategemea mafuta kutoka Mashariki ya Kati, lakini Tanzania tulishachukua hatua mapema. Hivyo hatuna shida ya mafuta mpaka sasa,” amesema Dk Andilile.

Dk Andilile amesema Ewura inafuatilia kila siku hali halisi ya upatikanaji wa nishati na gharama zake.

“Hali hii inaweza kutuathiri hata sisi katika upangaji wa gharama, lakini Serikali inahakikisha usalama na upatikanaji wa mafuta na bei zinabaki himilivu kwa watanzania,” amesema.

Naye Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wasambazaji wa Mafuta nchini (TAPSOA), Augustino Mmasi amesema mafuta yaliyopo nchini yanatosheleza kwa kiwango kikubwa mahitaji huku akisema umoja huo unaendelea kuhakikisha mafuta yanapatikana kila mahali kwa kiwango na bei ileile.

“Jana nilipokutana na TRA, wamenithibitishia mafuta yapo. Hali ya vita ikiendelea hadi kufikia wiki ijayo hali ya usafirishaji huenda ikawa changamoto, lakini Serikali imejipanga kudhibiti athari kwa wananchi,” amesema.

Mmasi amesisitiza usambazaji wa mafuta kila sehemu nchini utaendelea kufanyika kwa uangalizi wa mamlaka hiyo, akihimiza wananchi kutoingiwa na hofu juu ya kukosekana kwa nishati hiyo.

“Sisi ndio taasisi inayohusika na usambazaji wa mafuta kila mahali nchini, hivyo niwasihi msipaniki, nunueni mafuta ya kutosha kutumia siyo ya kuhifadhi,” amesema.