Wanawake wafundishwa nidhamu ya mikopo kuepuka migogoro
Muktasari:
- Miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni kuchukua mikopo bila kuwashirikisha wenza wao, hali inayoweza kusababisha migogoro pale biashara zinapokumbwa na changamoto.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wanawake nchini kuwaeleza na kuwashirikisha wenza wao kuhusu shughuli za kiuchumi wanazozifanya ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza iwapo mambo yataenda kombo.
Amesema kumekuwa na changamoto za baadhi ya wanawake kuchukua mikopo bila kuwashirikisha wenza wao, hali inayoweza kusababisha migogoro pale biashara zinapokumbwa na changamoto.
Akizungumza jana, Aprili 25, 2026, kwenye kongamano la Mwanamke na Kafiti, lililoandaliwa na Kafiti Foundation kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation, amesema wanawake wasifanye siri katika mambo hayo, kwani kufanya hivyo hakusaidii kujenga uchumi endelevu.
“Kuna mgogoro uliwahi kufika mezani kwangu, mwanamke alikuwa amechukua mkopo wa Sh60 milioni bila kumjulisha mumewe. Mke alishindwa kulipa mkopo huo na taarifa zikafika kwa mumewe, alishangaa kwani mahitaji yote alikuwa anayatoa yeye,” amesema Mtanda.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kiuchumi zitakazosaidia kuinua familia na kuchochea maendeleo ya Taifa.
“Mwanamke akiwa na uwezo wa kiuchumi, familia yote inanufaika, hivyo ni muhimu kutumia vizuri fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha na maendeleo,” amesema Mtanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, amesema taasisi hiyo imejikita katika kuwafikia wanawake, vijana na makundi maalumu kwa lengo la kuwaingiza katika uchumi rasmi.
Amesema kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, zaidi ya wajasiriamali 1,250,000 wamefikiwa nchini katika sekta mbalimbali, zikiwemo kilimo, uvuvi, madini na biashara ndogondogo.
“Fedha zilizotolewa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanawake wanapata mitaji na elimu ya kukuza biashara zao ili ziwe endelevu,” amesema Mwambapa.
Naye Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, amesema benki hiyo imetoa mikopo ya zaidi ya Sh513 bilioni katika Kanda ya Ziwa, na Sh240 bilioni zimeelekezwa Mkoa wa Mwanza pekee.
“Hali hii inaonesha umuhimu wa Mwanza katika uchumi wa nchi, lakini bado kuna kundi kubwa la wajasiriamali ambalo halijafikiwa na huduma za kifedha, hivyo kuanzishwa kwa CRDB Bank Foundation kumelenga kuziba pengo hilo,” amesema Raballa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kafiti Foundation, Mapuli Kafiti, amesema lengo la taasisi hiyo ni kuwafikia zaidi ya wajasiriamali milioni tano nchini kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na masoko.
Amesema ushirikiano na taasisi za kifedha unasaidia kuhakikisha wajasiriamali wanakuza biashara zao kwa njia endelevu na zenye tija.
Mbunge wa Ilemela, ambaye pia ni mwanzilishi wa Kafiti Foundation, William Kafiti, amesema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanainuka kiuchumi kupitia miradi ya kijamii na uwezeshaji wa moja kwa moja.
Amesema wameanza na makundi ya bodaboda na sasa wamehamia kwa wanawake wajasiriamali, huku wakiahidi kuendelea kupanua wigo wa miradi hiyo ili kila mmoja anufaike na fursa za kiuchumi.