Wawekezaji wazawa waibana Serikali

Mkutano huo wa kujadili mapitio ya sera ya uwekezaji uliratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) uliofanyika mjini Moshi.
Moshi. Serikali imetakiwa kuweka ukomo wa mambo ya kuwekeza baina ya wawekezaji wa ndani na wa nje kwa lengo la kuwawezesha wazawa kujijenga na kukua zaidi ili kuinua uchumi wa Taifa.
Hayo yalisemwa jana na baadhi ya wawekezaji wa ndani wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa mkutano wa kujadili mapitio ya sera ya uwekezaji ulioratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) uliofanyika mjini hapa.
Mmiliki wa hoteli za kitalii Moshi, Arusha na Karatu, Joachim Minde alisema umefika wakati Serikali kuweka bayana mambo yanayopaswa kuwekezwa na wageni kutoka nje ya nchi badala ya kuwaruhusu kuwekeza hadi kwenye mambo madogo yanayofanywa na wamachinga.
Alisema wanashangazwa na maneno ya Serikali kuwa Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya gesi na mafuta na kuwa kauli hizo ni aibu kwa taifa na inaonyesha ni jinsi gani Serikali inawadharau Watanzania na kuwafanya wageni kuendelea kuwanyanyasa wazawa kuwa hawawezi.
“Ni aibu kubwa waziri kusema Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza na ndiyo maana milango wanafunguliwa wageni. Wewe Mtanzania ukitaka kufanya jambo unaulizwa uko na nani kama huna mzungu nyuma yako hupewi ushirikiano. Wameshaona ili uwekeze, ni lazima uwe na mzungu. Jamani hata wao huko walikotoka walianza na umachinga wakapanda ngazi hadi wakawa wawekezaji, hakuna aliyeanza juu,” alisema Minde.
Ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo mkoani Kilimanjaro, Boniface Mariki alisema anashangaa kuona Serikali inawakumbatia zaidi wawekezaji wa nje kuliko wazawa.
“Wawekezaji wazawa hawathaminiwi na Serikali kama ilivyo kwa wawekezaji wa nje,”alisema.