Waziri Bashe atangaza bei mpya ya chai

Muktasari:

  • Baada ya kushindwa kupanda kwa zaidi ya miaka mitano, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametangaza bei mpya ya zao la chai itakayoanza kutumika katika mnada wa kwanza wa Februari 10, 2022

Iringa. Waziri wa Kilimo, Husein Bashe ametangaza bei mpya ya chai ambayo ni Sh366 kwa kilo itakayoanza kutumika kwenye mnada wa kwanza utakaofanyika Februari 10, 2023.

 Kwa zaidi ya miaka mitano, bei ya zao hilo haijawahi kupanda kutoka Sh314 jambo lililokuwa linawadidimiza wakulima.

Pamoja na bei hiyo, Waziri Bashe ametangaza kuanza kwa mnada wa chai utakaofanyika kwa njia ya kidigitali.

Katika mkutano wa wadau wa Kilimo cha chai uliofanyika mkoani Iringa jana Januari 18, Bashe alisema bei hiyo ni ya wastani.

Katika mchakato wa kupata bei hiyo, bei zilizotajwa ilikuwa ni Sh400, 380, 320 na 366.

Kwa upande wao wadau wa chai wamesema wamesema bei hiyo itawapatia unaafuu mkubwa wakulima mdogo ambao kwa zaidi ya miaka mitano walikuwa wakiuza bei ya chini.

“Walau wakulima wataanza kufurahia kilimo chao kwa sababu awali bei ilikuwa chini, wengi walikata tamaa wakaachana kabisa na chai,” amesema Elias Mgaya, mkulima wa chai.

Amesema hatua ya Waziri Bashe kuvalia njuga zao la chai litasaidia kufufua kilimo hicho ambacho kilianza kukimbiwa na wakulima wengi hususani vijana.

“Ukiangalia wanaolima chai ni wazee, vijana wameachana kabisa na zao hili kwa sababu haliwalipi, unaenda kuuza kiwandani halafu unalipwa baada ya miezi mitatu, minne hadi mitano,” amesema.

Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi kutoka Bodi ya Chai Tanzania, Remilembe Kafanabo amesema bei ndogo ya chai kwa wakulima ni kati ya sababu za kusuasua kwa zao hilo.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni kutopitika kwa barabara nyingi hasa vijijini, changamoto za masoko, ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima na ongezeko la gharama za uzalishaji.

Amesema pia, bei kubwa ya pembejeo za kilimo ukiachilia mbali mbolea ambayo msimu wa mwaka 2022/2023 imepata ruzuku, pia zimechangia zao hilo kutupwa mkono.