Bashe ataka minada ya chai ianzishwe 2023

Muktasari:

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ni lazima minada chai ianzishwe mapema mwaka huu ili kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuinua uchumi wa wakulima.


Iringa. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ni lazima minada ya chai ianzishwe mapema mwaka huu ili kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuinua uchumi wa wakulima.

Bashe ametoa agizo hilo jana Januari 18, 2023 Januari 18 alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha wadau wa chai katika ukumbi wa Royal Palm, mjini Iringa, akisisitiza lazima ifike hatua wakulima wanufaike na kilimo cha zao hilo.

Amesema inasikitisha kuona wakulima hawanufaiki na kilimo cha zao hilo huku wakiwepo baadhi yao wanaomwaga chai kwa kushindwa kuiuza na wale wanaouza wakisoma mpaka miezi mitano bila malipo.

Alipoanza hotuba yake kwa kusalimia Chai hoyee, alipojibiwa hoyee akakataa, akisema inatakiwa wajibu hoi kwa sababu ndio ukweli wenyewe.

 “Minada hii haitamgharimu mfanyabishara yeyote, hakutakuwa na tozo na kama mnahofia ‘direct market’ itakuwepo, lazima kuwe na uwazi na tuondoke kwenye hili eneo tulipo,” amesema Waziri Bashe.

Amehoji ikiwa wakulima wataamua kufyeka chai yote kwenye mashamba yao kwa sababu haiwalipi na kupanda mazao mengine itakuwaje?

“Mkulima anapeleka chai kiwandani analipwa baada ya miezi minne au mitano, tunajua chai imepitia kipindi kigumu na kilio cha madeni ya nyuma Serikali tunayashughulikia,” amesema Bashe.

Mbali na kuanzishwa kwa minada hiyo, ameshauri kubadilishwa kwa sheria zitakazowafanya wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuwa wajumbe halali kwenye vikao vya wadau wa chai.

 “Tuambiane ukweli, sitakuwa tayari kuongoza sekta hii kwa hali hii, tutoke hapa tumekubaliana ili wakulima waone wamesikilizwa,” amesema Bashe.

Kwa upande wao baadhi ya wadau wa chai wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika wamesema biashara ya zao hilo ilikuwa bubu na kwamba maagizo ya Bashe yamekuja wakati muafaka.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Chai Kilolo, Vicent Gaifalo alisema suala la minada kwenye zao hilo ni muhimu na kama hilo litafanyika zao la chai litawakomboa wakulima kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Muvyulu inayounganisha vyama tisa vya wakulima wa chai, Wilfred Swale amesema biashara hiyo ilikuwa bubu, hivyo minada itaongeza hamasa kwa wakulima.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chai aliyemaliza muda wake, Anna Makinda amesema lazima kuwepo uwazi na kuongea yaliyo kweli kuhusu chai.

Alisema matatizo ya zao la chai yanatokana na ubinafsi na kwamba, zao hilo limevurugwa.

“Kilolo lilikuwa suala la siku nyingi lakini halikupewa uzito uliostahili, mkulima angetamani bei nzuri huku viwanda vikitamani kulipa bei ndogo kwa wakulima. Hili tatizo tunaliona,” alisema Makinda

Makinda alijiuzulu nafasi yake kikatiba baada ya kuongoza vipindi viwili kwa maana ya miaka sita.