Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yas, ZTE kuwezesha wananchi kumiliki intaneti kwa urahisi

Mfanyakazi wa Yas akiwaelezea wanafunzi waliotembelea banda hilo katika maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF) huduma mbalimbali zinazotolewa na mtandao huo wa simu nchini.

Muktasari:

  • Kupitia mpango huo, wateja watapata fursa ya kumiliki rauta ya ZTE 5G kwa kulipa Sh80,000 kama malipo ya awali na kisha kulipia Sh80,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 12.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara, kaya na taasisi mbalimbali nchini sasa wataweza kumiliki huduma ya intaneti ya kizazi cha tano (5G) kwa malipo ya awamu, kutokana na ushirikiano kati ya kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania na kampuni ya teknolojia ya ZTE.

Ushirikiano huo ulizinduliwa jana, Julai 12, 2026 katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, ukiwa na lengo la kupanua upatikanaji wa intaneti ya kasi ya juu kwa gharama nafuu.

Uzinduzi wa huduma hiyo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali, huku Serikali ikisisitiza mageuzi ya kidijitali kama njia ya kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Mauzo na Vifaa vya Intaneti wa Yas Tanzania, Imelda Edward, amesema ushirikiano huo unalenga kuondoa kikwazo cha gharama ambacho kimekuwa kikiwazuia Watanzania wengi kupata huduma bora za intaneti.

“Leo hii, mawasiliano si suala la kuunganishwa na intaneti pekee, bali ni kufungua fursa. Intaneti ya uhakika inawawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao, wanafunzi kupata elimu ya kidijitali, wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na familia kuendelea kuwasiliana,” amesema.

Amesema mahitaji ya intaneti ya uhakika yameongezeka sambamba na ukuaji wa uchumi wa kidijitali, huku huduma nyingi za Serikali, biashara na mifumo ya malipo zikihamia mtandaoni.

Imelda amesema kwa wafanyabiashara nchini, intaneti imekuwa huduma muhimu sawa na umeme kutokana na mchango wake katika malipo ya kidijitali, mauzo ya mtandaoni, huduma kwa wateja na uendeshaji wa shughuli za kila siku za biashara.

“Kila oda inayofanyika mtandaoni, kila malipo ya kidijitali na kila mawasiliano na mteja yanategemea intaneti ya uhakika. Tunawapatia wafanyabiashara suluhisho za kidijitali zitakazowawezesha kushindana, kufanya ubunifu na kukuza biashara zao,” amesema.

Kupitia mpango huo, wateja watapata fursa ya kumiliki rauta ya ZTE 5G kwa kulipa kiasi cha Sh80,000 kama malipo ya awali na kisha kulipia Sh80,000 kila mwezi kwa muda wa miezi 12.

Kwa upande wake, mwakilishi wa ZTE, Wen Jiahao, amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kupanua upatikanaji wa teknolojia za kisasa za mawasiliano kwa gharama nafuu nchini.

“Kwa kuunganisha teknolojia yetu bunifu ya 5G na mtandao mpana pamoja na wigo mkubwa wa wateja wa Yas, tunarahisisha upatikanaji wa intaneti ya kasi na ya uhakika kwa watu binafsi, familia na biashara ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi nchini,” amesema.