Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar kubadili magari yote ya Serikali kuwa ya umeme

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bandria Masoud (kulia), akisikiliza maelezo kutoka kwa mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kuhusu namna mashine ya mafunzo inavyofanya kazi wakati wa ziara yake chuoni hapo. Anayeshuhudia (wa pili kulia) ni Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mussa Chacha. 

Muktasari:

  • Zanzibar imepanga kubadili magari yote ya serikali yanayotumia mafuta na kutumia nishati ya umeme ili kupunguza hewa ukaa, kulinda mazingira na kuharakisha matumizi ya nishati safi.

Arusha. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepanga kubadili magari yote ya Serikali yanayotumia mafuta na kuyaingiza katika mfumo wa matumizi ya nishati ya umeme, hatua inayolenga kuharakisha matumizi ya nishati safi na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mpango huo unalenga pia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kulinda mazingira na kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani.

Mbali na mageuzi hayo, SMZ inalenga kuimarisha mafunzo ya madereva ili kuongeza usalama barabarani, kupunguza ajali na kujenga wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya usafiri na uchukuzi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa SMZ, Bandria Masoud, alipofanya ziara katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kujionea mafunzo ya umahiri wa madereva pamoja na programu za elimu ya usafiri zinazotolewa na chuo hicho.

Masoud amesema mpango wa kubadilisha magari ya Serikali yanayotumia mafuta kwenda kwenye magari ya umeme tayari umeidhinishwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Amesema hatua ya kwanza ya mpango huo imeanza kupitia mabasi ya umeme ya usafiri wa umma, ambayo kwa sasa yako katika majaribio kabla ya kuzinduliwa rasmi.

“Tunajiandaa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa serikali kwa kubadilisha magari yanayotumia mafuta na kutumia magari ya umeme. Rais tayari ameidhinisha mpango huu, na tumeanza na mabasi ya umeme ambayo yako katika hatua ya majaribio,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya uzinduzi rasmi wa mabasi hayo, Serikali itaelekea katika mpango wa kubadilisha magari mengine yote ya serikali.

Pia, amesema licha ya Zanzibar kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi, ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa inayohitaji mikakati mipya ya kukabiliana nayo.

“Ajali za barabarani bado ni moja ya changamoto zetu kubwa. Tumefanya tathmini ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa, ndiyo maana tumekuja hapa kujifunza namna bora ya kuandaa madereva wenye umahiri na uwajibikaji mkubwa zaidi,” amesema.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Profesa Musa Chacha, amesema chuo kinaendelea kuboresha mitaala yake ili iendane na mabadiliko ya teknolojia duniani, hususan matumizi ya magari ya umeme.

Amesema Machi mwaka huu viongozi wa chuo walifanya ziara nchini Japan ambako walijenga ushirikiano na kampuni ya Toyota pamoja na taasisi za Kobe kwa ajili ya kujifunza teknolojia mpya za magari ya umeme.

“Magari mengi yanayotengenezwa Japan na nchi nyingine sasa yanatumia teknolojia ya umeme. Kutokana na uzoefu tulioupata, tumeboresha mitaala yetu kwa kuanzisha masomo ya teknolojia ya magari ya umeme, na mafunzo hayo tayari yanaendelea kutolewa,” amesema.

Profesa Chacha amesema chuo kinaendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa vya kisasa ili kuzalisha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sekta ya usafiri na uchukuzi katika siku zijazo.