JAMII: Ngonjera za wakubwa wetu Dar kweli zitalipa?

Takataka kama hizi zimekuwa mwiba kwa viongozi wakiwamo wa Mkoa wa Dar es salaam wanaofikiria kuanzisha shindano la usafi baina ya manispaa zinazounda mkoa huo.
Muktasari:
“Kwa mashindano hayo kila mmoja atakuwa mlinzi wa mwenzake katika kufanikisha zoezi hili kwa manufaa ya jiji,”anasema Sadick.
Jiji la Dar es Salaam ni moja kati ya miji nchini yenye mipango na kampeni nyingi za kudumisha usafi, lakini ukweli bado ni kati ya miji inayoongoza kwa uchafu.
Kutokana na kile kinachoonyesha kukithiri kwa hali hiyo ya uchafu, mapema mwezi huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alinukuliwa na vyombo vya habari akikiri kuwa uchafu umeshamiri katika jiji hili na mkoa wake.
Ndipo kiongozi huyo akatangaza mkakati na hatua za kuikabili hali hiyo.
“Hakuna asiyejua kama Dar es Salaam inaongoza kwa uchafu,” alisema Sadick.
Kwa maneno yake, moja ya hatua ya kukabili hali hiyo ya uchafu ni kuanzisha mashindano baina ya wilaya tatu zinazoundwa jiji hilo kwa lengo la kuhamasisha usafi na kutunza mazingira.
“Kwa mashindano hayo kila mmoja atakuwa mlinzi wa mwenzake katika kufanikisha zoezi hili kwa manufaa ya jiji,”anasema Sadick.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa ambaye naye alikuwa katika maadhimisho hayo, akasema kuwa ili kudumisha mazingira bora kwa Dar es Salaam na Afrika, watu wamkumbuke mwanaharakati wa mazingira nchini Kenya, Profesa Wangai Maathai (marehemu).
Anasema kwamba, kutokana na kuona umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Profesa Maathai alipigania utunzaji wa mazingira na kuhamasisha usafi wa taifa lake kwa manufaa ya wananchi wote.
Kauli hizi za viongozi na maelezo yao yanaelekea kusahau kuwa kwa kiasi kikubwa Dar es Salaam ni tofauti na miji mingine nchini au barani Afrika kwenye suala la miundombinu inayowezesha kuboreshwa kwa mazingira.
Tofauti na miji kama, Arusha au Moshi ambayo kwa hakika wamejitahidi kwenye suala la usafi, Dar es Salaam na hasa wakazi na viongozi wake wamejisahau kwenye suala la usafi, kiasi kwamba unaweza kuzunguka siku nzima bila kukutana na chombo cha kuwekea taka.
Hali hiyo huwalazimu watu wanaokunywa maji, kula matunda ya aina mbalimbali, kuvuta sigara, kutumia vocha za simu ama kitu chochote kingine, kukitupa ovyo barabarani.
Kwa mfano, chupa zinatupwa ovyo ingawa kwa siku za karibuni zimekuwa chumo kwa waokotaji wake, karatasi zinaachwa zikizagaa, wala hakuna sehemu ya kuzihifadhi.
Mbali na ukosefu wa sehemu za kuhifadhia taka hizo, magari yanayosomba taka kutoka maeneo mbalimbali kwenda kuzitupa katika majalala, yenyewe ni zaidi ya uchafu na mara nyingi husambaza taka hizo kwenye barabara yanakopita.
“Uchafu Dar es Salaam ni mtaji wa wakubwa, hata siku moja hauwezi kwisha, utasikia kila siku wakitangaza miradi ya kuumaliza, lakini hakuna kinachofanyika,” anasema George Samuel, mkazi wa Mbagala, Dar es salaam.
Wasiwasi wa Samuel na wengine kama yeye unatokana mipango mingi ikiwamo ile ya kununua vifaa ambavyo watendaji wakuwa wakisema ni bora, lakini uchafu katika jiji hili unaonekana kukithiri kila kukicha.
Wakati kwa upande wake, jiji likisuasua, watu binafsi ambao shughuli zao ni kuokota chupa na vyuma chakavu, kwa siku moja wanasaidia kusafisha mji, lakini bila malipo au hakuna anayewajali.
Mwenyekiti wa Chama cha Mazingira Cooperative society, Christopher Rugemalira anasema chama hicho kinajihusisha na biashara ya taka ngumu ikiwa ni pamoja na vyuma chakavu, mifuko na chupa za plastiki.
“Kutokana na kazi hii tumefanikiwa kusafisha mazingira na kuzalisha ajira. Kwa wilaya ya Ilala tunakusanya tani 200 hadi 300 kwa siku za taka ngumu kati ya tani 800 ya taka zote zinazokusanywa kwa siku.
Kuna vijana na watu wazima kati yetu waliojiajiri wanaendesha maisha yao kwa kazi hii,” anasema Rugemalira.