Mwalimu mlemavu anavyofundisha akiwa kwenye baiskeli
Mwalimu Roidy Mwangove akifundisha wanafunzi wa kidatocha nne katika Sekondari ya Itewe nje kidogo ya mji wa Chunya, Mbeya. Picha na Mary Mwaisenye
Muktasari:
Hali kadhalika wapo wenye ulemavu ambao wanaamini kwamba wanahitaji misaada katika maisha yao yote, wamekata tamaa, wanaishi kwa misaada miaka nenda rudi.
Hata hivyo wapo wenye ulemavu wachache ambao wameweza kujiongeza kwa kuchapa kazi na wengine wana mafanikio kuliko hata wasio na ulemavu.
Zipo fikra kutoka kwa watu wengi kwamba mlemavu hawezi kufanya kazi za kujipatia kipato.
Hali kadhalika wapo wenye ulemavu ambao wanaamini kwamba wanahitaji misaada katika maisha yao yote, wamekata tamaa, wanaishi kwa misaada miaka nenda rudi.
Hata hivyo wapo wenye ulemavu wachache ambao wameweza kujiongeza kwa kuchapa kazi na wengine wana mafanikio kuliko hata wasio na ulemavu.
Mmoja wapo ni Mwalimu Roidy Mwangove (42) mlemavu wa miguu yote miwili anayetumia baiskeli ya miguu mitatu kutembea.
Mwangove ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Itewe iliyopo, Chunya, mkoani Mbeya akifundisha wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. ‘Nilizaliwa mwaka 1974 jijini Mbeya nikiwa mwenye ulemavu wa miguu, anasimulia.
Mwalimu huyo anasema alianza masomo katika Shule ya Msingi Mbalizi mwaka 1985 na alipofika darasa la pili alihamishiwa Shule ya Watoto wenye Ulemavu ya Katumba iliyopo wilayani Rungwe na kumaliza darasa la saba.
‘Nilichaguliwa kuingia Shule ya Sekondari ya Mbalizi ambako nilisoma na mwaka 1994 nilihitimu kidato cha nne na kupata daraja la tatu.”
Baada ya kuhitimu kidato cha nne, akiwa na daraja la tatu, Mwalimu Mwangove anasema aliomba ajiunge Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mkoani Morogoro lakini hakuchaguliwa.
Hata hivyo uongozi wa chuo hicho haukumpa sababu ya kutomchagua lakini Mwangovu katika fikra zake anaaamini walimnyima nafasi kutokana ulemavu aliokuwa nao.
Anasema jambo hilo lilimuuma sana na kusababisa kuwa na mawazo ya mara kwa mara na kutafakari kwa vipi atajiendeleza baada ya baba yake kufariki na kubaki na mama yake pekee ambaye naye hali yake ya kipato haikuwa nzuri.
Anafafanua kuwa baada ya kukaa nyumbani bila shughuli yoyote ya kumuingizia kipato alimwomba mama yake amlipie kidato cha tano na sita naye alikubali na mwaka 1998 alijiunga na masomo ya kidato cha tano katika mchepuo wa sanaa unaohusisha masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL) katika Shule ya Sekondari ya Sangu na kuhitimu mwaka 2000 na kupata daraja la tatu,” anasema.
Kwa kuwa alikuwa anaamini na kuupenda ualimu, Mwangove anasema aliamua kuomba kozi ya ualimu katika Chuo cha Ualimu Tukuyu wilayani Rungwe.
“Ikawa kama bahati ya mtende kwani nilikubaliwa kujiunga kusomea Stashahada katika masomo ya Historia na Jiografia.”
Ataja siri ya mafanikio
“Kwa kweli tangu nilipoanza darasa la kwanza Shule ya Msingi Mbalizi niliweka lengo la kuonyesha uwezo wangu kiakili na kuwathibitishia wengine kwamba ulemavu wangu ni wa miguu na si akili.
Anasema alifanya bidii katika masomo ya ualimu na hatimaye alifanikiwa kufanya vizuri kozi yake ya ualimu .
“Awali walijaribu kunikatalia kozi ya ualimu wakionyesha hofu ya mimi kuandika ubaoni, lakini niliwaeleza anayejua ni mimi na Mungu wangu’’.
Apangiwa kufundisha Sekondari ya Itewe
Anasema baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo, alipangiwa kufundisha Shule ya Sekondari Itewe iliyopo jijini Mbeya.
‘‘Nilipowasili hapa, wenzangu walipata hofu ni kwa vipi nitafundisha kutokana na ulemavu wangu wa miguu, lakini niliwaonyesha kwa vitendo wenzangu kwamba licha ya ulemavu wa viungo uwezo akili ninao,” anasisitiza.
Aingia darasani kufundisha na baiskeli
Anasema kutokana na ulemavu aliokuwa nao, hawezi kusimama ubaoni kama ilivyo kwa walimu wengine na badala yake inamlazimu kuingia darasani na baiskeli yake.
“Naingia na baiskeli yangu hadi darasani na hiyo ndiyo inanisaidia kuufikia ubao.”
“Jamii itambue mazingira ya mtu mwenye ulemavu, waelewe kuwa ulemavu na kile mtu alichonacho kichwani haviingiliani kwani yeye anafundisha na wanafunzi wanamuelewa vizuri kama ilivyo kwa walimu wengine.”
Changamoto anazokutana nazo akiwa shuleni
Licha ya kujiamini na kuikubali hali aliyonayo Mwalimu Mwangove anaeleza changamoto anazokutana nazo katika kazi yake kutokana na ulemavu alionao kuwa ni miundombinu mibovu ya kuingia madarasani.
Mwalimu huyo mwenye mke na watoto wawili anasema miundombinu ya kuingia madarasani ni mibaya kiasi cha kusababisha mara kadhaa kuomba msaada wa kuinuliwa na baiskeli yake ili aweze kuingia darasani kufundisha akiwa na baiskeli yake.
Anaongeza kuwa chanagamoto nyingine ni vyoo ambavyo si rafiki kwa watu wenye ulemavu na hivyo kumfanya ajikute katika wakati mgumu.
Ombi lake kwa Serikali
Mwalimu Mangove anaishauri Serikali iwawezeshe watu wenye ulemavu kwa kuwapatia elimu bure hadi vyuo vikuu.
“Serikali iziangalie kwa jicho la huruma shule maalumu za wenye ulemavu kwa kuzijengea miundombinu na hatimaye wanaosoma nao wasaidiwe.”
“Naomba Serikali, taasisi au mtu yeyote anisaidie kuboresha usafiri walau kwa kupata bajaj au gari maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa kuwa baiskeli niliyonayo inanisumbua sana.”
Walimu, wanafunzi wazungumza
Mkuu wa Shule ya Itewe, Mura Njeje anasema licha ya mwalimu Mwangove kuwa na ulemavu lakini anamudu vyema kazi ya kufundisha.
Njeje anasema ni mwalimu mwenye juhudi na busara jambo lililomfanya amteue kuwa mwalimu wa nidhamu.
Mkuu huyo wa shule anasema mwalimu huyo wa nidhamu anatekeleza vizuri wajibu wake na hajawahi kupata malalamiko kutoka kwa wanafunzi anaowafundisha wa kidato cha kwanza hadi cha nne anaowafundisha masomo ya Historia na Jiografia.
Laurent Zachari ni mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo, licha ya kumsifia Mwalimu Mangove pia anaiomba Serikali kujenga miundombinu mizuri kwa wenye ulemavu ili waweze kuwa vizuri.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo analaumu mazingira mabaya ya kuingia darasani kwamba yanampa taabu mwalimu wao huyo.
“Hatujawahi kumkosa katika kipindi chochote lakini anapata wakati mgumu sana kuingia darasani na baiskeli yake wakati mwingine inabidi tumsaidie kwa kumsukuma,”anaongeza mwanafunzi huyo.
Naye Mwanafunzi Egla Shekidele wa kidato cha nne anasema Mwalimu Mangove ni mzuri katika ufundishaji na kwamba kuna haja ya Serikali kuweka miundombinu rafiki kwa walemavu ili waweze kuingia mahali popote ikiwamo kwenye maofisi mbalimbali.