Biden aendelea na mipango kuunda Serikali

Muktasari:

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden anaendelea na mchakato wa kuunda utawala wake huku Rais aliyeshindwa katika uchaguzi uliopita, Donald Trump akiendelea kuwasilisha kesi mahakamani.

Washington, Marekani. Rais mteule wa Marekani, Joe Biden anaendelea na mchakato wa kuunda utawala wake huku Rais aliyeshindwa katika uchaguzi uliopita, Donald Trump akiendelea kuwasilisha kesi mahakamani.

Jana, Biden alikutana na kikundi cha washauri wake ambao wanamsaidia kuweka msingi wa utawala mpya na kumwandaa kula kiapo cha kuchukua madaraka ifikapo Januari 20, mwaka ujao.

Biden alimshinda Trump katika uchaguzi huo baada ya kupata kura za majimbo 290 dhidi ya 214 za mshindani wake.

Katika kura za wananchi Rais huyo mteule alipata zaidi ya kura milioni 75 wakati mshindani wake akiwa na zaidi ya kura milioni 70.

Miongoni mwa washauri hao ni wataalamu wa masuala ya kifedha wanaotoka chama chake cha Democratic pamoja na wale wenye mrengo usio wa kihafidhina akilenga kuakisi mjadala unaoendelea ndani ya chama hicho juu ya namna ya kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la DW, Rais huyo mteule anawatumia watu waliopangilia sheria kali za kimazingira wakati wa utawala wa Rais Barack Obama.

Licha ya Rais Trump na maofisa wengi wa chama cha Republican kuendelea kutoyakubali matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3, uchunguzi wa maoni ya raia uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa ushirikiano na shirika la utafiti la Ipsos, umeonyesha kuwa asilimia 80 ya Wamarekani, wakiwemo nusu ya Warepublican, wanamkubali Biden kama mshindi halali.

Mmoja wa Warepublican hao ni Seneta Mitt Romney ambaye alisema kuendelea kupinga matokeo ni doa kwenye sura ya Marekani.

“Sielewi ninapowasikia watu wanaosema uchaguzi ulikuwa na mizengwe na wizi. Kwa maoni yangu hilo siyo sahihi, na pili, ni hatari katika mchakato wa uhuru kwa sababu macho yote ya dunia yanaitazama Marekani, kuangalia jinsi tunavyoushughulikia uchaguzi huu,” alisema Romney.

Kwa upande mwingine, Rais Trump anaendeleza mchakato wake wa kimahakama, akishikilia madai yake ya udanganyifu katika uchaguzi alioupoteza bila hata kuambatanisha malalamiko yake na ushahidi ulio bayana.

Tayari majaji wameyatupilia mbali malalamiko ya Trump katika majimbo ya Michigan na Georgia na wataalamu wa sheria wanasema mashtaka yake yana nafasi finyu ya kuweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyompa ushindi Biden.

Licha ya hali hiyo lakini sehemu kubwa ya maofisa wa chama cha Republican wameendeleza mshikamano na Rais wa Trump wakisema anayo kila haki ya kulalamika pale anapoamini kuwa hakutendewa haki.

Wakati hayo yakijiri, shughuli za kuhesabu kura bado hazijakamilika katika majimbo kadhaa yaliyokuwa na ushindani mkali. Rais Trump anaongoza katika jimbo la North Carolina huku Biden akiongoza katika majimbo ya Georgia na Arizona, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la uchunguzi la Edison Research.