Binadamu wa ajabu wanaoweza kuzama ndani ya maji dakika 13

Muktasari:

  • Wengi huweza kuzama majini kwa dakika kati ya mbili hadi tatu

Wakati mvua zikiendelea kunyesha na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo nchini, kwingineko duniani jamii ya Bajau hiyo ndiyo starehe yao.

Inakadiriwa binadamu ana uwezo wa kubana pumzi kwa takribani dakika mbili ndani ya maji.

Lakini jamii ya Bajau inaelezwa kuwa mabingwa wa kuzama ndani ya maji, wakidumu hadi kwa dakika 13 katika vilindi vya maji vya futi 200.

Kwa mamia ya miaka, watu wa jamii hii wamekuwa wakiishi baharini ikiaminika maumbile yao kijenetiki ndiyo yanawawezesha kuwa na uwezo wa kuzama na kukaa majini kwa muda mrefu.

Watu hao wanaojulikana pia kwa jina la Sama-Bajau wanahusisha makundi ya jamii zinazoishi Kusini mwa Asia katika nchi za Philippines, Malaysia, Thailand na Indonesia.

Wanajulikana kwa kuwinda samaki au kusaka vitu wanavyotumia kwenye kazi zao za kila siku.

Mara nyingi hujenga nyumba ndani ya maji ya bahari na kuendesha maisha yao humo.

Utafiti kuhusu seli umebaini mabadiliko ya DNA yanayofanya wengu kuwa kubwa yanawawezesha watu wa jamii ya Bajau kuwa na uwezo kijenetiki wa kukaa ndani ya maji kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili: Wengu ni kiungo ndani ya mwili kinachosaidia kudhibiti usambazaji wa damu. Pia hujulikana kama bandama.

Kamusi hiyo inaeleza bandama ni: Kiungo cha mwili wa mnyama kilicho ndani ya kiwiliwili upande wa kushoto ambacho huzalisha na kutoa chembe hai za damu katika kuimarisha sehemu ya mfumo wa kinga mwili.

Utafiti

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la National Geographic, uliofanywa katika Kituo cha Geogenetics cha Chuo Kikuu cha Copenhagen, nchini Denmark umethibitisha sababu za jamii ya Bajau kuwa na uwezo wa kuzama ndani ya maji kwa muda mrefu. 

Mtafiti Melissa Llardo aliyesafiri Thailand na Indonesia, anaeleza alivutiwa na uhodari wa watu wa Bajau.

“Nilitamani kwanza kukutana na jamii hiyo na si tu kujionyesha na vifaa vya kisayansi na kuondoka. Katika safari yangu ya pili, nilinunua mashine ya ultrasound na kifaa cha kukusanyia mate, tulitembelea makazi yao na kuchukua picha za wengu zao. Nilipata watu wengi na walishangazwa, niliwasikia,” anasema.

Anasema alichukua pia taarifa kutoka jamii ya Saluan, inayoishi Indonesia. Katika utafiti huo, anaeleza aligundua wastani wa ukubwa wa wengu la watu wa Bajau lilikuwa kubwa kwa asilimia 50 kulinganisha na wa Saluan.

Watafiti pia walifuatilia jeni ya PDE10A, inayodhaniwa hudhibiti tezi aina ya thyroid lenye umbo mithili ya kipepeo linalokaa chini ya shingo.

Tezi hilo huzalisha homoni za thyroxine (T-4) na triiodothyronine (T-3). Hata hivyo, jamii ya Saluan haikuwa na jeni hiyo.

Utafiti ulibaini panya wenye homoni hizo wana wengu kubwa na wasiookuwa nayo walionekana kuwa na wengu dogo.

Llardo amehitimisha utafiti wake akisema, mazingira wanayoishi Bajau kwa maelfu ya miaka yamewafanya kuwa na mabadiliko ya kijenetiki.

Shinikizo la chini           

Ingawa wengu linaweza kueleza kwa sehemu jinsi Bajau walivyo na uwezo wa kuzama ndani ya maji, mabadiliko mengine yanaweza kuchangia pia, anaeleza Richard Moon kutoka Chuo Kikuu cha Duke School of Medicine.

Moon aliyechunguza jinsi mwili wa binadamu unavyojihisi unapokuwa kina kirefu na kina kifupi cha maji anasema, kwa kadiri binadamu anavyoendelea kuogelea zaidi ndani ya maji, ongezeko la shinikizo husababisha mishipa ya damu ya mapafu kujaa damu zaidi na inaweza kupasuka na kusababisha kifo.

Kwa upande wake, mwanahistoria wa masuala ya sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Case Western Reserve, Cynthia Beall aliyechunguza watu wanaoishi katika nyanda za juu zaidi duniani, wakiwamo Watibeti wanaosemekana kuishi kwenye ‘paa la dunia’ anafikiri utafiti wa Llardo unafungua fursa za utafiti wa kuvutia, lakini anahitaji kuona ushahidi wa biolojia unaoweza kupimika zaidi kabla hajashawishika kwamba sifa ya jeni inasaidia Bajau kuwa wajuzi wa kuzama majini.

Hata hivyo, kundi hilo linaonekana kuwa sehemu ya watu waliotengwa na ambao hawafurahii haki za uraia au kuishi maisha ya kisasa kama watu wengine duniani.

Pia, wanaathiriwa na maendeleo ya teknolojia katika uvuvi, hivyo utamaduni wao wa kuzamia baharini kuwa katika hatari ya kutoweka.

Kwa mtindo wao wa maisha, pasipo msaada, Llardo ana hofu kuwa kundi hilo huenda likatoweka siku za usoni.


Wataalamu nchini wanasemaje?

Akizungumzia hali hiyo, Profesa wa sayansi ya majini (marine sayansi), Yunus Mgaya anasema mabadiliko kwa viumbe hai hutokea ili kuviwezesha kumudu mazingira wanayoishi.

“Sisi binadamu tupo katika kundi la mamalia, mfumo wetu wa kuvuta hewa hutegemea mapafu yanayopokea oksijeni na kuitumia maisha yaendelee,” amesema.

“Kuna mamalia wengine wanaoishi ndani ya maji kama nyangumi, pomboo, hao hujitokeza nje ya maji na kutoa hewa chafu kupitia tundu lililo juu ya kichwa na kisha huvuta hewa nyingi na huzama kwenye maji.”

 “Tunachoweza kufanya sisi binadamu ni kujifunza kuvuta hewa tukiwa ndani ya maji kwa kuelea.”

“Kuna uwezekano wa binadamu kubadilisha tabia kama watazoea mtindo wa maisha kwa miaka mingi. Kuna uwezekano wa jeni nyingi kubadilisha tabia na kuwabadilisha, kama ilivyo kwa hao watu (Bajau),” anaeleza.

Amerejea historia ya binadamu (evolution) akisema hata Wazungu walitoka Afrika kwenye jua kali na kwenda Ulaya kwenye baridi kali na ndipo ngozi zao zilibadilika na kuwa nyeupe.

“Hata Waeskimo wanaoishi kwenye baridi kali wana uwezo wa kukabili hali hiyo, wewe ukipelekwa kule huwezi kuishi,” amesema Profesa Mgaya.

Kwa upande wake, mtaalamu wa kuogelea kutoka Chama cha Waogeleaji (TSA), Alexander Mwaipasi anasema mwanadamu kukaa ndani ya maji kwa dakika 13 haiwezekani.

“Hayo ni maajabu, kusikia mwanadamu mwenye uwezo huo. Mimi mwenyewe na utaalamu wangu mara ya mwisho nimeweza kuzama kwenye maji kwa dakika 2:25. Hiyo inahitaji mazoezi makali, japo wapo vijana wanaofikisha dakika tatu,” anasema.

Hata hivyo, amesema kuziba pumzi si kipaumbele katika mafunzo ya kuogelea.

“Mtu hakuumbwa kuishi kwenye maji, kwa hiyo tunawafundisha kuvuta hewa wakiwa ndani ya maji kwa mitindo ya uogeleaji,” anasema.