Hezbollah yaionya Israel

Wanamgambo wa Kundi la Hezbollah la Lebanon.

Muktasari:

 Ni baada ya Israel kufanya shambulio katika ubalozi wa Iran uliopo Damascus nchini Syria na kuua watu saba wakiwAmo makamanda wawili

Lebanon. Kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran limesema litalipa kisasi kwa Israel baada ya kufanya shambulizi na kuwaua makamanda wawili wa ngazi za juu wa Iran na watu wengine watano.

Katika shambulio hilo waliouawa ni Brigedia Jenerali Mohammad Zahedi, Kamanda Mkuu katika Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Naibu wake Jenerali Mohammad Hajriahimi waliuawa.

Hezbollah kundi lenye ushirika wa karibu na wanamgambo wa Hamas wa Palestina limesema hayo baada ya shambulio la Israel lililotekelezwa kwenye ubalozi wa Iran uliopo mjini Damascus, Syria jana.

"Hakika uhalifu huu hautapita bila ya adui kupata adhabu na kulipiza kisasi," limesema kundi la Hezbollah katika taarifa yake kama ilivyoandikwa na Shirika la Habari la AFP.

Hata hivyo, Iran pia imeahidi kujibu mapigo baada ya shambulio hilo dhidi ya ubalozi wake mdogo.

Ubalozi huo ambao uko katika Wilaya ya Mezzeh ya Damascus, ulishambuliwa saa 11 kwa saa za Syria jana Jumatatu.

Picha, kutoka eneo la tukio zilionyesha vifusi huku bendera ya Iran ikiwa bado ikining'inia kwenye nguzo iliyo karibu.

Kundi la Hezbollah kwa muda mrefu limekuwa likishambuliana na Israel katika mpaka wa kusini kati ya Lebanon na Israel tangu kuzuka kwa vita.


(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)