Vita vikali mbio za Urais nchini Iran

Muktasari:

  • Atapoachia madaraka mwezi Juni mwaka huu, atakuwa tayari ameweka ramani ambayo itapaswa kuchunguzwa upya na mrithi wake. Kiongozi ajaye anakabiliwa na kibarua cha kupaka upya rangi uhusiano wa Taifa hilo na mataifa ya ng’ambo.


Inawezekana Iran ikachukua mkondo mpya katika siasa za kimataifa. Rais Mahmoud Ahmadinejad anaelezewa kwamba ni miongoni mwa viongozi waliofaulu kudumisha sera ya mambo ya nje ya Iran.

Harakati zake dhidi ya madola ya Magharibi, zilimsaidia kupata uungwaji mkono kutoka kwa Kiongozi mkuu wa kidini wa  Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Mara zote amekuwa mstari wa mbele kuzikosoa nchi za Magharibi kwa kile anachokieleza kuwa uingiliaji wa mambo ya ndani ya Iran.

Kwa mfano, msimamo wake mkali dhidi ya Taifa la Israel uliongeza hasira kwa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ambayo bado iko kwenye malumbano na Tehran.

Pamoja na kwamba kumekuwa na majadiliano kuhusiana na urutubishaji wa vinu vya nyuklia, hata hivyo Iran imeendelea kukosana na nchi za Magharibi ambazo zinataka kusimamishwa kwa mpango huo. Majadiliano yaliyofanyika hivi karibuni hayakufaulu kufikia suluhu ya pamoja.

Tehran inasisitiza kuwa mitambo hiyo ya nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya nishati ya umeme na siyo  vinginevyo. Rais Ahmadinjad aliyezaliwa Aradan, karibu na Garmsar, Kaskazini mwa Iran ameapa kuendelea kupambana na madola ya kimagharibi.

Atapoachia madaraka mwezi Juni mwaka huu, atakuwa tayari ameweka ramani ambayo itapaswa kuchunguzwa upya na mrithi wake. Kiongozi ajaye anakabiliwa na kibarua cha kupaka upya rangi uhusiano wa Taifa hilo na mataifa ya ng’ambo.

Kuwepo kwa idadi kubwa ya wagombea wanaowania nafasi ya uongozi kwenye uchaguzi wa Juni 14, kumetoa ashirio kuwa Iran inawajibika kujisuka upya katika siku za usoni. Jumla ya wagombea 686, wakiwemo wanaume 656 ambo ni asilimia 96, na wanawake 30 ambao ni asilimia 4 ya wamejiandikisha kuwania kiti hicho.

Miongoni mwa  vigogo waliojiandikisha kugombea kinyang'anyiro hicho ni pamoja na  Ali Akbar Vilayati, Haddad Adel mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Muhammad Baqer Qalibof, Meya wa jiji la Tehran na  Akbar Hashimi Rafsanjani ambaye ni Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.

Licha ya kukoselewa na wapinzani wake, Rais Ahmadinajad amebainisha bayana nia yake ya kumuunga mkono mgombea Esfandiyar Rahim-Mashaei ambaye kwa sasa ni mshauri wake, na amekuwa mtu wake wa karibu kwa kipindi kirefu.

Wakati wa zoezi la kujiandikisha lililomalizika hivi karibuni, wote wawili waliandamana hadi ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya kurejesha fomu na baadaye wakati wa kutoka Rais Ahmadinjad aliwapungia mkono mashabiki huku akionyesha kidole chenye ishara ya herefu “v” akiashiria ushindi kwa mgombea huyo kwenye uchaguzi ujao.

 

Pamoja na hayo wachunguzi wa mambo wanalitupia macho jina la Rafsanjan ambaye anatajwa kuwa na ushawishi mkubwa hasa kutokana na uzoefu wa kisiasa alioupata katika miaka ya nyuma.  Amewahi pia kuwa rais kwa muhula mmoja na baadaye alifanya vibaya katika uchaguzi uliofuta.

Anatajwa kuwa ni mtu mwenye msimamo wa kati anayependelea majadiliano na kuheshimu haki za binadamu. Nchi za Magharibi zinamtizama kama mtu anayeweza kushaurika tena ni “muungwana”.Hata hivyo bado anakabiliwa na safari ndefu ya kuruka viunzi vya kisiasa kutoka kwa wagombea wengine ambao pia wameonyesha upeo mkubwa wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa.

Wakati walipojitokeza kwenye mahojiano na vyombo vya habari, baadhi ya wagombea waliainisha vipaumbele watavyozingatia iwapo watachaguliwa kuingia Ikulu ya Tehran. Miongoni mwa mambo ambayo yalijitokeza kwa wingi kwenye mahojiano hayo,  ni kuhusu suala la kulinda mafanikio ya Taifa la Iran hasa katika uwanja wa teknolojia ya nyuklia.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kujiandikisha wagombea, Wizara ya Mambo ya Ndani inapaswa kuwasilisha haraka majina ya wagombea kwa Baraza la Kulinda Katiba.

 Baraza hilo ambalo lina jukumu la kuchunguza sifa za wagombea hao na kuwaidhinisha,   linawajibika kufanya hivyo kabla ya kuwasilisha maoni na mapendekezo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya siku tano.

Mambo muhimu yanayojadiliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na kampeni za uchaguzi,  ili kuwapa fursa wagombea wote kunadi sera zao bila kuathiriwa na mazingira yoyote na kukwepa upendeleo kutoka kwa taasisi za umma.

Kuna mengi yanatarajiwa kushuhudiwa kwenye uchaguzi huu ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na nchi za Ulaya, ambazo kampeni yake ya kutaka kulishikiza Taifa hilo liachane na mpango wa urutubishaji wa madini ya urani unaelekea kugonga mwamba.

Jambo jingine linalovutia zaidi kuhusiana na uchaguzi huo ni kujitokeza kwa mgombea mwenye umri mdogo zaidi ambaye anaelezwa kuwa na miaka 19. Mgombea huyo anabeba matumaini mapya ya wanasiasa wengi vijana ambao mara zote wamenyimwa fursa za kuchomoza kwenye majukuwaa ya kisiasa.

Hata hivyo,  wachambuzi wa mambo wanasema kuwa bado ni mapema mno kubashiri mwelekeo halisi wa siasa za Iran, hasa kutokana na uchaguzi huu kuwavutia wagombea wengi zaidi ikiwemo  yule mwenye umri mkubwa zaidi ambaye anatajwa kuwa na miaka 87.