Rais mteule Nigeria kwenda kupumzika Uingereza

Rais mteule wa Nigeria, Bola Tinubu.

Rais mteule wa Nigeria, Bola Tinubu (70) ameibua gumzo baada ya kuondoka nchini humo kwenda mapumzikoni nchini Uingereza, huku wadadisi wa mambo wakihoji kuhusu afya ya mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akisafiri nje ya nchi mara kwa mara.

Tinubu alishinda urais katika uchaguzi mkuu wa Februari 25, akigombea kupitia Chama cha APC, akichuana kwa karibu na wagombea wengine wawili ambao ni Makamu wa Rais wa zamani, Atiku Abubakar (76) wa Chama cha PDP na Peter Obi (61) wa Chama cha Labour.

Mteule huyo anatarajiwa kuapishwa Mei 29 kuchukua nafasi ya Rais Muhammadu Buhari, ambaye anamaliza muda wake wa uongozi wa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.

Taifa hilo lililokuwa likitawaliwa kijeshi sasa linaendeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi ambapo Tinubu anakuwa Rais wa tatu kuchaguliwa kwa mfumo huo.

Jumanne iliyopita, Wanigeria walishtushwa na taarifa za Tinubu kuondoka nchini humo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya mapumziko kwa kilichoelezwa kwamba alichoka baada ya kampeni alizozifanya.

Wengi wanahusisha safari zake hizo na matatizo ya kiafya, kwamba anakwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kutokana na maradhi yanayomsumbua, jambo ambalo limepingwa vikali na kambi yake.


Akanusha afya dhaifu

Jumatano iliyopita Tinubu alipuuzilia mbali ripoti za vyombo vya habari vya Nigeria kwamba ana tatizo la afya, huku kambi yake ikisema alisafiri nje ya nchi kupumzika na kupanga mipango yake ya mpito baada ya kampeni za uchaguzi wa urais.

Afya ya Tinubu inaangaliwa kwa karibu katika nchi ambayo Rais wa zamani alifariki akiwa madarakani baada ya kuugua kwa muda mrefu na kiongozi wa sasa, Muhammadu Buhari alikuwa akisafiri mara kwa mara kwenda nje ya nchi kwa uchunguzi wa afya. Mwanzoni mwa mwaka 2017 alitumia miezi mitatu kwa likizo ya matibabu nchini Uingereza kutokana na maradhi ambayo hayakutajwa.

Ushindi wa Tinubu katika uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita uliokumbwa na utata, unapingwa mahakamani na wapinzani wake wawili wa karibu.

Gavana huyo wa zamani wa jiji la biashara la Lagos alionekana kuwa dhaifu wakati wa kampeni, akitoa hotuba zake polepole na isiyoeleweka, lakini mara kwa mara alipuuza wasiwasi uliokuwa unaibuliwa kuhusu afya yake.

“Baada ya kampeni kubwa na msimu wa uchaguzi, Rais mteule, Tinubu, amesafiri nje ya nchi kupumzika na kupanga mipango yake ya mpito kabla ya kuapishwa Mei 29,” msemaji wake wa kampeni, Tunde Rahman alisema kwenye taarifa aliyoitoa kwa umma.

Hata hivyo, Tunde hakusema Tinubu amesafiri kwenda wapi lakini alijuza kuwa atarejea hivi karibuni.


Wapinzani wakata rufaa

Wakati Tinubu akiwa mapumzikoni, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Labour, Peter Obi amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa aliyekuwa mgombea wa chama tawala cha APC uliotangazwa mwezi uliopita.

Hiyo si mara ya kwanza kwa uchaguzi wa Rais nchini Nigeria kupingwa mahakamani, ingawa upinzani haujawahi kushinda kesi yoyote kati ya zilizofunguliwa.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, Obi alimaliza katika nafasi ya tatu, mbele ya mgombea mkuu wa upinzani Atiku Abubakar wa Chama cha PDP ambaye naye anapinga ushindi wa Tinubu.

Msemaji wa Chama cha Labour, Yunusa Tanko, alisema Obi amekwenda kupinga ushindi wa Rais mteule na namna Tume ya Uchaguzi ilivyokusanya matokeo ya urais na kuyatangaza.

Waangalizi wa kimataifa kutoka Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Madola walikiri kutokea kwa hitilafu katika mfumo wa kusambaza matokeo kutoka vituoni, uliolenga kuzuia wizi wa kura.

Hivyo basi, Mahakama ya Rufaa itaunda jopo maalumu litakalosikiliza na kuamua kesi hizo ndani ya siku 180.

Iwapo Obi na wapinzani wengine hawataridhika na uamuzi wa jopo hilo, watakuwa huru kwenda katika Mahakama ya Juu ambayo itakuwa na siku 60 za kusikiliza kesi hiyo. Ushindi wa Tinubu ukithibitishwa na Mahakama, anatarajiwa kuapishwa Mei 29.


Changamoto za uchaguzi

Muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo Machi mosi, vyama vyote viwili vya Labour na PDP vilipinga ushindi wa Chama cha APC, vikidai kuwa hitilafu za kiufundi zilitoa nafasi ya kasoro kwenye kuhesabu kura, lakini Tume ya Uchaguzi ilikanusha madai hayo.

Nigeria, Taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika liliwachagua zaidi ya wabunge 900 wa mabunge ya majimbo na magavana 28 kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa, hasa katika mji mkuu wa kibiashara, Lagos.

Kutokana na vurugu, upigaji kura uliahirishwa katika baadhi ya maeneo katika Wilaya ya Eti Osa jijini Lagos na katika wilaya za Asari-Toru na Degema za Jimbo la Rivers ambako uchaguzi ulipangiwa tarehe nyingine.

Maeneo mengine yaliyokuwa na ushindani mkali katika uchaguzi huo ni ya Rivers kusini mwa Nigeria na eneo la Kano la kaskazini. Katika eneo la Adamawa la kaskazini mashariki, mwanamke wa kwanza aliibuka mshindi kwa kuchaguliwa kuwa gavana wa jimbo hilo.

Ripoti zilieleza kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia, rushwa na idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza kupiga kura. Tume ya kupambana na Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha ilisema watu wasiopungua 65 walikamatwa wakidaiwa kuwashawishi wapiga kura.

Katika hatua nyingine, wananchi waliovalia mavazi meusi na kubeba mabango, waliandamana wakiongozwa na mgombea wa Chama cha PDP aliyeshika nafasi ya pili hadi Tume ya Uchaguzi nchini humo na kulizuia lango la kuingia katika afisi hizo, huku wakitaka mamlaka ziandae uchaguzi mpya katika mazingira mazuri yatakayoleta matokeo sahihi.

Karibu vyama vitano vya upinzani nchini humo viliyapinga matokeo ya uchaguzi, vikidai kulikuwa na uchakachuaji.

Ili kuchaguliwa kuwa Rais wa Nigeria, mgombea anapaswa kupata angalau asilimia 25 ya kura katika angalau theluthi mbili ya majimbo 36, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Abuja.