Trump amdhihaki Biden kwa kusahau jina lake

Muktasari:

Rais wa Marekani, Donald Trump amemdhihaki mpinzani wake, Joe Biden kwa kusahau jina lake na kumuita “George”, ikiwa ni wiki moja kabla ya uchaguzi.

Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump amemdhihaki mpinzani wake, Joe Biden kwa kusahau jina lake na kumuita “George”, ikiwa ni wiki moja kabla ya uchaguzi.

Trump, 74, amekuwa akimtuhumu Biden, 77, kuwa ni mzee wakati wawili hao wakipambana kabla ya Wamarekani kupiga kura Novemba 3.

Tabia ya Joe Biden ya kufanya makosa katika uzungumzaji iliibuka tena Jumapili jioni wakati alipopata shida kukumbuka jina la Trump wakati akihutubia kwa njia ya video ambayo iliunganishwa katika televisheni.

Mara mbili alimuita mpinzani wake jina la “George” pengine akirejea mmoja wa marais wa chama hicho kutoka familia ya Bush.

“Miaka minne zaidi kwa George, eh, George, eh, yeye tutakuja kujikuta katika mahali ambako kama Trump amechaguliwa, tutakuwa katika ulimwengu mwingine,” alisema Biden, akiwa amekaa pamoja na mkewe Jill, ambaye alionekana kuwa anamsahihisha.

Trump amekuwa akitaka kuonyesha kuwa Biden ana tatizo la afya ya akili na mara moja akarukia vitendo hivyo vya usahaulifu.

“Joe Biden aliniita George jana. Hakuweza kukumbuka jina langu,” Trump aliandika katika akaunti yake ya Twitter.

“Kikundi cha habari za uongo kinafanya kazi ya ziada kufunika hilo!”

Biden, ambaye atakuwa rais mwenye umri mkubwa kuliko wote kama atachaguliwa, amekuwa akimjibu vikali Trump kuhusu afya yake ya akili, akisema ni mbinu za kuwaondoa watu katika kujadili rekodi yake ya urais.

Rais Trump ambaye anahaha kutaka achaguliwe tena kuongoza taifa hilo kubwa duniani, alipata ahueni juzi baada ya kuthibitishwa kwa mteule wake mpya wa Mahakama Kuu, akionekana kukiweka chombo hicho cha juu upande wake.

Bunge la Seneti, ambalo limejaa maseneta kutoka Republican, lilimpandisha Amy Coney Barrett hadi nafasi ya juu likimpa kura 52 dhidi ya 48, baada ya mchakato wa kina na ushindani mkubwa, ambao unamfanya awe mtu wa sita kutoka upande wa wahafidhina kuingia katika mahakama hiyo yenye watu tisa.

“Hii ni siku ya aina yake kwa katiba ya Marekani, kwa Marekani na kw auongozi wa haki usioegemea upande wowote,” Trump akiwa amesimama pamoja na Barrett, alisema.

Barrett, 48, anahakikisha Trump kuacha kumbukumbu kubwa katika mahakama. Trump pia amekuwa akiteua majaji vijana wa mrengo wa kulia katika mahakama za shirikisho katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Wajumbe wa Democratic wamekasirishwa na mchakato uliomthibitisha jaji ambao uko karibu sana na uchaguzi wa rais, na kuonya kuwa Barrett anaweza kupiga kura kubatilisha uamuzi wa mwaka 1973 ambao unalinda haki za kutoa mimba, au kutibua huduma za afya kwa mamilioni ya Wamarekani.

Lakini Barrett, ambaye aliapa juzi, alisema atalinda imani zake binafsi na kazi ya mahakama.