Waziri wa afya Iran aambukizwa corona

Muktasari:

Zaidi ya watu 16 wamefariki dunia nchini Iran kutokana na ugonjwa huo.

Tehran. Naibu Waziri wa Afya nchini Iran, Iraj Haririch ameambukizwa virusi vya corona.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, naibu waziri huyo amegundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo baada ya kuonyesha dalili za homa kali na kufanyiwa vipimo.

Imeelezwa kuwa waziri huyo kwa sasa ametengwa katika eneo maalum na akiendelea na matibabu chini ya uangalizi.

Taarifa zinasema kuwa mpaka sasa ugonjwa huo umeua watu 16 nchini humo huku idadi ya maambukizi ikiongezeaka kwa kasi.

“Watu 95 wameambukizwa virusi hivyo mpaka sasa huku idadi ya visa vipya ikiongezeka siku hadi siku,” ilisema taarifa ya wizara ya afya ya nchi hiyo.

Iran ni miongoni mwa nchi ambazo ziko hatarini katika maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo ambao unasaambaa kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani.

Zaidi ya watu 2,700 wamefariki kutokana na ugonjwa huo mpaka sasa huku kukiwa na watu zaidi ya 80,200 wenye maambukizi ya ugonjwa huo ulianza miezi mitatu iliyopita.