Adaiwa kumkata mkono mwenzie wakigombea ardhi

Muktasari:

  • Mwanaume mmoja ambaye ni mfugaji kutoka Kenya anadaiwa kukatwa mkono na mfugaji mwenzie katika kisa kilichoelezwa cha kugombania ardhi.

Kenya. Polisi Kaunti ya Machakos nchini Kenya wanamsaka mfugaji anayedaiwa kumkata mwenzie mkono kwa kile kinachoelezwa “walikuwa wakigombea ardhi ya malisho ya mifugo.”

Baada ya mtuhumiwa kumkata mkono inaelezwa aliingia mitini ambapo kwa sasa jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta ili kumtia nguvuni.

Muathiriwa wa tukio hilo amefahamika kwa jina la Francis Muteti ambaye mbali na kukatwa mkono wake kwenye kifundo pia alikutwa na majeraha kichwani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko ya nchini humo tukio hilo lilitokea Jumatatu ya mwanzo wa wiki hii ambapo familia ya Muteti iliamua kupeleka mkono uliokatwa hospitalini kwa matumaini ya kuunganishwa tena kupitia upasuaji.

Polisi wamesema walipofika eneo la tukio, Muteti alikuwa akivuja damu nyingi huku akiwa na majeraha makubwa kichwani.

"Maofisa wa polisi walikimbia hadi eneo la tukio katika kijiji cha Kiliala na wakaupata mkono wa kushoto wa mwathiriwa ukiwa umekatwa kabisa kwenye kifundo na alikuwa na majeraha kichwani pamoja na kuvuja damu.

"Wanafamilia walisisitiza waende hospitalini na sehemu ya mwili iliyokatwa ili kujaribu njia mbadala ya kufanyiwa upasuaji. Mtuhumiwa amekimbia na juhudi za kumkamata zinaendelea," ripoti ya Polisi imeeleza.

Aidha, Polisi wameongeza kuwa wamepata panga, ambalo wanashuku kuwa ndiyo silaha iliyotumika katika shambulio hilo.