Ajali yaua watu 12, yajeruhi watatu
Gari ya abiria (iliyobebwa) ikiwa imeharika vibaya kufuatia kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Ndii, Kaunti ya Taita Taveta nchini Kenya.
Muktasari:
- Ajali ya barabarani iliyohusisha gari la abiria na roli katika eneo la Ndii huko Voi, Kaunti ya Taita Taveta, nchini Kenya, imesababisha vifo vya watu 12 na majeruhi Watatu, huku chanzo cha ajali hiyo, kikiendelea kuchunguzwa.
Kenya. Watu 12 wameripotiwa kufariki na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani eneo la Ndii huko Voi, Kaunti ya Taita Taveta, kwenye barabara kuu ya Nairobi – Mombasa, huku chanzo cha ajali kikichunguzwa.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea jana, Kamanda Msimamizi Mkuu wa Polisi (OCPD) mjini Voi, Bernstein Shari, amesema abiria 12 walifariki papo hapo baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori.
Gari hiyo ya abiria yenye uwezo wa kuchukua abiria 14 mali ya Chania Sacco, ilikuwa ikielekea Mombasa kutoka Nairobi huku lori la mizigo likitokea Nairobi kwenda Mombasa.
Waathiriwa watatu waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi, mjini Voi; huku uchunguzi kuhusu ajali hiyo ukiendelea.