Aliyepandikizwa figo ya nguruwe aruhusiwa

Muktasari:

  • Taarifa ya hospitali imesema mtu huyo alikuwa akipambana na ugonjwa wa figo na alihitaji kupandikizwa kiungo hicho, ili kuokoa maisha yake.

Massachusetts. Richard Slayman (62) kutoka Massachusetts aliyepandikizwa figo iliyobadilishwa vinasaba kutoka kwa nguruwe ameruhusiwa kutoka hospitalini.

Kwa mujibu wa BBC, Slayman ameruhusiwa kwenda nyumbani, ikiwa ni wiki mbili kupita baada ya upasuaji katika Hospitali Kuu ya Massachusetts (MGH).

Taarifa ya hospitali imesema mgonjwa huyo Slayman kutoka mji wa Weymouth, alikuwa akipambana na ugonjwa wa figo na alihitaji kupandikizwa kiungo hicho, ili kuokoa maisha yake.

Katika kufanikisha hilo, madaktari walifanikiwa kupandikiza figo ya nguruwe iliyobadilishwa vinasaba katika mwili wake kwenye upasuaji uliofanyika kwa saa nne Machi 16, 2024.

Baada ya kufanyika kwa upasuaji huo, madaktari wamesema hivi sasa figo yake inafanya jkazi vizuri na Slayman haitaji kupata huduma ya kusafishwa damu (dialysis).

Kwa upande wake, Slayman amepokea taarifa ya kuruhusiwa kwa furaha isiyo kifani, huku akisema ni mojawapo ya nyakati za furaha kubwa maishani mwake.

“Wakati huu, ninapoondoka hospitali nikiwa sina deni la afya ambalo limekuwa ni la muda mrefu. Nina furaha na nilitamani kuwa hivi kwa miaka mingi iliyopita,” amesema Slayman.

Mkuu wa madaktari katika hospitali hiyo, David Klassen amesema upasuaji huo wa kutumia viungo vya wanyama kwenda kwa binadamu, ni tumaini kubwa miongoni mwa wagonjwa wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine, hospitali hiyo imesema Slayman ataendelea kutumia dawa kadhaa za kinga ya mwili na kufuatiliwa kwa karibu na vipimo vya damu na mkojo mara tatu kwa wiki na pia kuonwa na daktari mara mbili kwa wiki.

Aidha, madaktari wamemuonya Slayman kuhusu kurudi kazini, wakisema anahitajika kupumzika kwa muda wa wiki sita.

Imeandaliwa Sute Kamwelwe na Mashirika