Bobi Wine awatoroka polisi waliozingira nyumba yake

Muktasari:

  • Mwanamuziki na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda,  Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amewatoroka polisi  waliokuwa wameizingira nyumba yake iliyopo eneo la Magere mjini Kampala.

Kampala.  Mwanamuziki na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda,  Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amewatoroka polisi  waliokuwa wameizingira nyumba yake iliyopo eneo la Magere mjini Kampala.

Kuanzia jana usiku hadi leo asubuhi Jumatano Oktoba 9, 2019 polisi waliizingira nyumba hiyo kumzuia mwanasiasa huyo kushiriki tamasha la muziki la Independet Day Music Concert.

Jana  mkuu wa jeshi la polisi nchini humo alitangaza kusitishwa kwa tamasha hilo kutokana na sababu za kiusalama.

Msemaji wa Bobi Wine, Joel Senyonyi amesema mwanasiasa huyo ambaye pia ni kiongozi wa vuguvugu la nguvu ya umma  alitoroka bila polisi kugundua.

Hata hivyo, msemaji wa polisi nchini humo, Patrick Onyango amekanusha kuwa mwanamuziki huyo amewatoroka  na kusema ameondoka nyumbani kwake na polisi wanafuatilia anakoelekea.

Onyango amesema polisi waliizingira nyumba yake baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda kumuandikia barua ya kusitisha tamasha hilo.

“Sio kweli kwamba ametutoroka, tumemuacha aondoke na hakuwa kwenye kizuizi chochote lakini tunafuatilia nyendo zake,” amesema Onyango.