Bosi wa Nissan atoweka Japan ‘kimafia’

Aliyekuwa bosi wa kampuni ya kutengeneza magari ya Nissan, Carlos Ghosn 

Aliyekuwa bosi wa kampuni ya kutengeneza magari ya Nissan, Carlos Ghosn ametoweka kitatanishi nchini Japan, ambako ameshtakiwa kwa kukiuka kanuni za fedha na sasa yuko Lebanon huku polisi wa kimataifa, Interpol wakitoa taarifa ya kumsaka.

Kigogo huyo alitoweka Japan akiwa nje kwa dhamana, ambayo awali ilipingwa vikali na upande wa mashtaka.

Haijafahamika aliondokaje Japan, lakini serikali ya Ufaransa, ambayo ilisema haikujua mipango ya bosi huyo wa zamani wa Renault kutoroka nchini Japan, ilisema tajiri huyo alinufaika na ofisi ya ubalozi wake jijini Tokyo.

“Mamlaka za Ufaransa hazikutaarifiwa kuhusu kuondoka kwake Japan na haikuwa na taarifa kuhusu mazingira ya kuondoka huko,” ilisema wizara ya mambo ya nje, ikiongeza kuwa ilipata taarifa hizo katika vyombo vya habari.

Lakini taarifa hiyo inasema Ghosn alinufaika na usaidizi wa ofisa ubalozi wa Ufaransa jijini Tokyo, na kwamba kulikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya ofisi ya ubalozi, Ghosn na wanasheria wake.

“Hali yake, pamoja na maombi ya baadhi ya kanuni za kisheria zilifuatwa kwa umakini wakati wote na ubalozi wetu mjini Tokyo,” ilisema wizara hiyo.

Ghosn, ambaye ana uraia wa Ufaransa, Lebanon na Brazil, aliamriwa kusalimisha hati zake za kusafiria ikiwa ni sehemu ya masharti ya dhamana yake baada ya kukamatwa mwezi Novemba, 2018 jijini Tokyo.

Kigogo huyo wa Nissan mwenye umri wa miaka 65 anakabiliwa na mashtaka ya kutangaza mshahara wake wa mamilioni ya dola chini ya kiwango wakati akiwa mwenyekiti wa Nissan, ambayo ni mshirika wa kampuni ya kutengeneza magari ya Ufaransa, Renault.

Ghosn pia anatuhumiwa kuhamishia hasara zake binafsi katika kampuni ya Nissan.

Ukosefu wa taarifa kamili kuhusu kutoroka kwake kumeibua ubashiri kuhusu jinsi mtu huyo maarufu alivyofanikiwa kuondoka.

Alitakiwa kuweka dhamana ya dola 13.4 milioni za Kimarekani kabla ya kesi yake iliyopangwa kusikilizwa mwaka huu. Akihofiwa kuwa angeweza kutoroka, alitakiwa asalimishe hati zake tatu za kusafiria na kuwekwa chini ya uangalizi mkali na aliwekewa masharti mengi ya kutumia simu zake na kompyuta.

Asingeweza kutoka nyumbani kwake kwenda kununua maziwa bila ya kuonekana, lakini akatoweka.

Kuna hisia nchini Japan kuwa alisafirishwa kutoka Japan kwa kuwekwa kwenye boksi la vifaa vya muziki, baada ya kundi la muziki kutumbuiza nyumbani kwake.

Lakini wengine wanasema alitumia hati ya kughushi ya kusafiria, kwa mujibu wa jarida la Ufaransa la Les Echos.

Hata jijini Tokyo. Ghosn alikuwa na tabia ya kupotosha taswira yake. Wakati akitoka mahabusu baada ya kuachiwa kwa dhamana, alivalia kama fundi katika jitihada za kukwepa vyombo vya habari. Alivaa kofia ya bluu na kuziba uso na kinyago.

Wakati akifikishwa mahakamani, alitimuliwa kutoka Nissan na kampuni ya Mitsubishi Motors, kampuni ya tatu ambayo ilikuwa katika umoja aliounda, na baadaye kujiuzulu utendaji mkuu wa Renault.

Ghosn alithibitisha yuko Lebanon, Jumanne iliyopita na kulaumu mfumo wa haki wa Japan.

“Sasa niko Lebanon na sitawekwa ndani na mfumo usio wa haki wa Japan ambako hatia huamuliwa mapema (kabla ya mashtaka), ubaguzi ni mkubwa na haki za msingi za binadamu zinakiukwa,” alisema tajiri huyo.

“Sijakimbia haki, nimekimbia ukosefu wa haki na mashtaka ya kisiasa,” alisema Ghosn, akiongeza kuwa anaweza kuongea kwa uhuru na vyombo vya habari, kitu ambacho aliahidi kukifanya kuanzia wiki ijayo.