EU yawawekea vikwazo wanaochochea ghasia DRC

Muktasari:

  • Watu 17 sasa wamewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya ambavyo vimeongezwa hadi Desemba 12, 2023 na zinajumuisha marufuku ya kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya na kuzuia mali zao.


S:

Emmanuel Msabaha, Mwananchi

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya (EU) umewawekea vikwazo wahusika wa ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao ni viongozi wa makundi mbalimbali yenye silaha ikiwamo kundi la M23.

EU imewawekea vikwazo watu wanane wapya, wakiwemo wanachama watano wa makundi tofauti yenye silaha yanayofanya kazi katika maeneo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, mashariki mwa DRC.

Katika orodha hiyo, Willy Ngoma, msemaji wa kijeshi wa M23 ambaye, kwa mujibu wa EU “amechangia na kupanga vitendo vinavyojumuisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini DRC”.

Wawakilishi wa makundi mengine manne yenye silaha wanasemekana kuwajibika kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na pamoja na kuchochea vita nchini DRC.

Wengine wameorodheshwa kwa kuchochea ghasia na kuanzisha vita kwa kujihusisha na unyonyaji haramu na biashara ya maliasili, EU ilieleza katika uamuzi wake.

Katika muktadha wa vita mashariki mwa DRC, Umoja wa Ulaya ulisema kuwa uamuzi wake ni sehemu ya mbinu jumuishi ya EU kuunga mkono juhudi za mamlaka ya DRC kuanzisha amani ya kudumu na kuleta utulivu eneo la mashariki mwa nchi”.


Hivyo, jumla ya watu 17 sasa wamewekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya ambavyo vimeongezwa hadi Desemba 12, 2023 na zinajumuisha marufuku ya kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya na kuzuia mali zao.

Baraza linaahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mambo nchini humo na linaweza kuzingatia hatua zaidi za vizuizi kadri hali inavyoendelea.

Baadhi ya watu waliowekewa vizuizi hivyo ni Protogene Ruvugayimikore ambaye anajulikana kama Ruhinda au Zorro Midende.

Huyo ni kiongozi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR-FOCA), amewekewa vikwazo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kuendeleza migogoro ya silaha.

Willy Ngoma ambaye ni msemaji wa kundi la M23, kundi lisilo la kiserikali lenye silaha linalofanya kazi mashariki mwa DRC, analaumiwa kwa kuamuru vurugu kwa raia na kuchochea migogoro.

Justin Bitakwira anayejulikana kama Bihona-Hayi, waziri wa zamani wa DRC, anatuhumiwa kutoa matamshi ya chuki dhidi ya jamii ya Banyamulenge na kuchochea mashambulizi ya silaha dhidi yao.

Mwingine ni Meddie Nkalubo anayetambulika kama Mohamed Ali, ni kiongozi wa kundi la kigaidi la Uganda la Allied Democratic Forces (ADF), amewekewa vikwazo kwa ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji na utekaji nyara mashariki mwa DRC.