Faye amteua Sonko kuwa Waziri Mkuu wa Senegal

Muktasari:

  • Changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kutengeneza ajira za kutosha katika taifa hilo ambalo asilimia 75 ya watu milioni 18 wana umri wa chini ya miaka 35 na kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira ni asilimia 20.

Dakar. Rais wa Senegal, Bassirou Faye amemteua mshauri wake na kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko kuwa Waziri Mkuu, saa chache baada ya kuapishwa jana Jumanne Aprili 2, 2024 kuwa Rais wa tano wa Senegal.

Faye (44) aliapishwa jana katika Ikulu ya Senegal akichukua nafasi ya Macky Sall ambaye alitaka kuiongezea muda madarakani kinyume cha Katiba, jambo ambalo lilipingwa vikali na wananchi waliokuwa wakiandamana.

Saa chache baadaye, utawala wake mpya ulimteua kiongozi wa upinzani Sonko kuwa waziri mkuu.

“Ousmane Sonko ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” amesema Oumar Samba Ba, Katibu Mkuu wa Ikulu alipokuwa akisoma agizo kwenye kituo cha televisheni ya taifa cha RTS.

Sonko (49), alikuwa katika mvutano wa miaka miwili na serikali ambao ulizua machafuko mabaya. Aliondolewa katika kinyang'anyiro cha urais hivi karibuni na akamchagua Faye kama mbadala wake kwenye uchaguzi wa urais.

Faye na Sonko walikuwa miongoni mwa kundi la wanasiasa wa upinzani walioachiliwa huru kutoka gerezani siku 10 kabla ya uchaguzi wa urais wa Machi 24 kupitia msamaha uliotangazwa na Rais wa zamani, Macky Sall ambaye alijaribu kuchelewesha uchaguzi huo.

Kijana huyo ambaye hajawahi kushika wadhifa wa kuchaguliwa, alipata ushindi katika awamu ya kwanza kwa ahadi ya kufanya mageuzi makubwa, alifanya kampeni kwa siku 10 tu baada ya kuachiliwa kutoka gerezani.

“Mbele ya Mungu na Taifa la Senegal, naapa kutimiza kwa uaminifu ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Senegal,” Faye alisema mbele ya mamia ya maofisa na wakuu kadhaa wa nchi za kiafrika katika kituo cha maonyesho katika mji mpya wa Diamniadio, karibu na mji mkuu wa Dakar.

Pia, aliapa kutetea “uadilifu wa eneo na uhuru wa kitaifa na kutoacha juhudi zozote za kufikia umoja wa Afrika”.

Mkaguzi huyo wa zamani wa kodi anakuwa Rais wa tano wa Senegal tangu taifa hilo lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960 na wa kwanza kukiri waziwazi kuwa na wake wengi.

“Ninafahamu kuwa matokeo ya kura kwenye masanduku yanaonyesha hamu kubwa ya mabadiliko ya kimfumo,” Faye alisema katika hotuba fupi baada ya kula kiapo cha urais.

“Chini ya uongozi wangu, Senegal itakuwa nchi ya matumaini, nchi yenye amani na Mahakama huru na demokrasia iliyoimarishwa,” aliongeza.

Faye alikuwa miongoni mwa kundi la wapinzani wa kisiasa walioachiliwa huru kutoka gerezani siku 10 kabla ya uchaguzi wa urais ya Machi 24, 2024 chini ya msamaha uliotangazwa na Rais aliyemaliza muda wake, Macky Sall, ambaye alijaribu kuchelewesha kura hiyo.