G7 yaahidi fedha zaidi kudhibiti Ebola, wasisitiza usalama Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- G7 na nchi saba zenye uchumi mkubwa duniani ambazo ni Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza, Canada na Japan.
Ufaransa. Viongozi wa kundi la nchi saba zilizoendelea kiuchumi duniani (G7) wameahidi kutoa fedha zaidi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Ahadi hiyo ilitolewa wakati wa kilele cha mkutano wa G7 uliofanyika nchini Ufaransa, ambapo viongozi hao wameeleza mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo umekuwa tishio la usalama wa afya duniani, baada ya kusababisha vifo vya watu 197 nchini DRC na wawili Uganda.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumatano, Juni 17, 2926, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa hatua za haraka za kimataifa na kuunga mkono mwitikio madhubuti na ulioratibiwa kwa ushirikiano wa nchi wanachama wa G7 pamoja na mataifa washirika yaliyoalikwa kwenye mkutano huo.
Nchi washirika zilizounga mkono msimamo huo ni Kenya, Misri, India na Korea Kusini.
“Tumedhamiria kutoa na kuhamasisha msaada kwa mwitikio wa pamoja wa kimataifa utakaowezesha maendeleo na usambazaji wa chanjo maalumu, vifaa vya uchunguzi na matibabu ya kukabiliana na mlipuko huu katika miezi ijayo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mkutano huo pia ulipongeza hatua ya Marekani ya kutenga zaidi ya dola milioni 370 kwa ajili ya huduma za afya na misaada ya kibinadamu katika ukanda huo.
Aidha, utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umetangaza nyongeza ya dola milioni 500 kwa juhudi za kukabiliana na Ebola.
Mbali na fedha hizo, Marekani imetangaza kutoa dola milioni 650 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu katika eneo la Maziwa Makuu, huku Umoja wa Ulaya ukiahidi euro milioni 493 kwa ajili ya misaada ya dharura, chanjo, matibabu na kuimarisha usalama wa afya katika eneo la Maziwa Makuu na Uganda.
Kati ya fedha hizo za Umoja wa Ulaya, euro milioni 84 zitatolewa mara moja kusaidia shughuli za kibinadamu, maendeleo na tafiti zinazohusiana na mlipuko huo.
Viongozi hao wameleza Mpango wa Bara la Afrika wa Maandalizi na Mwitikio dhidi ya Ebola kwa sasa unakusanya dola milioni 518 kusaidia nchi za Afrika kujiandaa, kugundua haraka na kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia wamezitaka nchi nyingine na washirika wa maendeleo nje ya G7 kuongeza rasilimali kwa ajili ya kukabiliana na tishio hilo la afya ya dunia.
Wakati huohuo, viongozi hao wamethibitisha kuendelea kuunga mkono mpango wa kibinadamu unaoratibiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ambao unalenga kuwafikia watu milioni 87 wanaohitaji msaada wa kuokoa maisha mwaka 2026.
Kuhusu mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea kufanyika nchini Marekani, Canada na Mexico, viongozi wa G7 wamewahakikishia mamilioni ya mashabiki pamoja na timu 48 zinazoshiriki usalama wao umepewa kipaumbele.
“Tunahitaji kuhakikisha wanaweza kushiriki kwa usalama. Kwa kuzingatia mamlaka ya kila nchi, tumejizatiti kuimarisha uratibu kati ya mamlaka zetu za kitaifa na kuweka mwafaka kuhusu taratibu za safari, karantini na kujitenga kwa watu waliotoka katika maeneo yaliyoathirika, kwa kuzingatia viwango vya juu vya kimataifa vya afya ya umma na usalama,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, viongozi hao wameonya juhudi za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Ebola vinaweza kukwamishwa na mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC.
Kutokana na hali hiyo, wametoa wito kwa pande zote zinazohusika kuheshimu makubaliano yao na kutekeleza kikamilifu makubaliano ya Washington ya amani na ustawi pamoja na mfumo wa Doha.
Aidha, wamezitaka taasisi na wadau wanaoshiriki katika mwitikio wa dharura kuboresha uratibu na kuepuka kurudia shughuli zinazofanana ili kuhakikisha hatua za haraka na zenye ufanisi zaidi katika kukabiliana na janga hilo.
Katika muktadha huo, viongozi hao wamehimiza wadau wote kuoanisha shughuli zao na mipango pamoja na mahitaji yaliyobainishwa na Umoja wa Mataifa.
Mktano wa G7 mwaka huu umejumuisha mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani yakiwemo Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza pamoja na Canada na Japan.
Mbali na hayo, zimealikwa pia Kenya, Brazil, Misri, India, Korea Kusini, Qatar, Syria na Ukraine.
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa Dailynation