Gachagua ampongeza Odinga kusitisha maandamano

Makamu wa Rais wa Kenya, Rigath Gachagua.

Muktasari:

  • Baada ya kiongozi wa Azimio nchini Kenya, Raila Odinga kukubali kusitisha maandamano yaliyokua yakiendelea nchini humo, Makamu wa Rais wa Kenya Rigath Gachagua amempongeza kwa uamuzi huo.

Kenya. Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amempongeza kiongozi wa Azimio Raila Odinga kwa kukubali kusitisha maandamano dhidi ya serikali.

Raila ametoa tangazo hilo leo Aprili 3, 2023 muda mfupi baada ya Rais William Ruto kumuomba asitishe maandamano hayo na kutoa nafasi kwa mazungumzo.

Akizungumza Jumapili, Aprili 2, Waziri Mkuu huyo wa zamani alikubali wito wa Rais wa mazungumzo, akisema kambi yake iko tayari kwa mazungumzo yatakayoshughulikia masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za maisha.

Katika taarifa kupitia mtandao wa Twitter, Gachagua amempongeza Raila kwa kukubali mazungumzo akimtaja kama mwanasiasa wa kuheshimika.

"Nampongeza Raila Odinga kwa kusitisha maandamano na ghasia na kuchagua kuendeleza masuala yake Bungeni kwa mujibu wa Katiba na sheria za Kenya. Hiyo ni siasa ya heshima," amesema Gachagua.

Gachagua amesisitiza kuwa Kenya inaongozwa kwa sheria na kwamba ghasia na uharibifu wa mali hazina nafasi katika utawala wa Ruto.

 “Kama Rais wetu alivyosema, Serikali itaendelea kujitolea kulinda maisha na mali kesho, keshokutwa, wiki ijayo na miaka ijayo,” ameongeza Gachagua.

Kufuatia hatua hiyo ya kusitishwa kwa maandamano, Gachagua amewataka Wakenya wote kurejea kazini na kuendelea na biashara zao.

Odinga ambaye ni kinara wa siasa nchini Kenya amekubali pendekezo la Ruto la kufanya mazungumzo kuhusu katiba ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kama sharti la kukubali kusitisha maandamano.

 Kuhusu suala la kupanda kwa gharama ya maisha, Raila pia ameitaka serikali kurejesha ruzuku iliyotumiwa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta.

Alisisitiza kuwa kushughulikia gharama ya juu ya maisha itakuwa kipaumbele katika mazungumzo yao.