Hezbollah yaishambulia Israel kwa makombora ikijibu mapigo

Muktasari:

  • Kundi la wanamgambo la Hezbollah kutoka nchini Lebanon limesema limerusha makombora Kaskazini mwa Israel. 

Beirut. Washirika wa karibu wa kundi la wanamgambo wa Hamas, kundi la Hezbollah kutoka nchini Lebanon limerusha msururu wa makombora Kaskazini mwa Israel hii leo na kuua mtu mmoja.

Hatua hiyo inakuja ikiwa inajibu mashambulizi yaliyotanguliwa na Israel ya kurusha makombora yaliyoua watu takribani saba Kusini mwa Lebanon.Vikosi vya uokoaji vya Israel katika mji wa mpakani wa Kiryat Shmona vimefanikiwa Kupata mwili wa kijana wa miaka 25 ambaye vimesema ameuawa katika tukio hilo.

Hata hivyo Hezbollah imethibitisha kurusha makombora hayo ili kulipiza kisasi kwa kile ilichokiita mauaji yaliyofanywa na adui wa Kizayuni (Israel), katika kijiji cha Habariyeh kusini mwa Lebanon.

Shirika la Habari la AFP limesema Hezbollah na jeshi la Israel wamekuwa wakimiminiana risasi karibu kila siku mpakani, tangu Hamas waliposhambulia Israel Oktoba 7 mwaka jana na kusababisha vita huko Gaza.

Taarifa zaidi zinasema kumekuwa na mapigano tangu Oktoba ambapo kuna vifo vya  watu takriban 338 nchini Lebanon, wengi wao wakiwa wapiganaji wa Hezbollah lakini pia wakiwemo raia 57, hii ni kwa mujibu wa AFP.