Hezbollah yaionya Israel ikisema hatuogopi vita

Kiongozi wa Kundi la Hezbollah la Lebanon, Hassan Nasrallah akihutubia mamia ya watu kwa njia ya televsheni

Muktasari:

  • Shambulizi la ndege zisizo na rubani za Israel lililotekelezwa Kusini mwa Beirut na kumuua Sahel al-Arouri limemfanya Nasrallah kuionya Israel

Beirut. Kiongozi wa Kundi la Hezbollah la Lebanon, Hassan Nasrallah amelionya Taifa la Israel kufuatia kifo cha aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi la wanamgambo la Hamas, Sahel al-Arouri.

Shambulizi la ndege zisizo na rubani za Israel lililotekelezwa Kusini mwa Beirut na kumuua kiongozi huyo limemfanya Nasrallah kuionya nchi hiyo dhidi ya kufanya vita dhidi ya Lebanon.

"Iwapo adui atafikiria kupigana vita dhidi ya Lebanon, tutapigana bila kizuizi, bila mipaka na bila vikwazo," amesema Nasrallah katika hotuba yake kwenye televisheni hapo jana.

Nasrallah amesema kuwa, "hatuogopi vita," kama alivyonukuliwa na Shirika la Habari la AFP.

Hamas na maofisa wa usalama Lebanon, waliishutumu Israel kwa kumuua Saleh al-Arouri na wengine sita katika shambulio la Jumanne.

Msemaji wa Jeshi la Israel, Daniel Hagari hakuzungumzia moja kwa moja kuhusu mauaji hayo lakini alisema jeshi lao lilikuwa limejitayarisha kwa hali yoyote.

Kumekuwa na majibizano ya risasi kati ya Hezbollah na Israel karibu kila siku tangu vita vya Israel na Hamas vilipozuka Oktoba 7, 2023 lakini mauaji ya Arouri yamesababisha hofu zaidi ya mzozo.

Tangu mapigano yaanze, watu 171 wameuawa kwa upande wa Lebanon, wengi wao wakiwa wanachama wa Hezbollah na zaidi ya raia 20 wakiwamo waandishi wa habari watatu, kwa mujibu wa takwimu za AFP.

Kwa upande wa Israel, takriban raia wanne na wanajeshi tisa wameuawa, kwa mujibu wa takwimu za jeshi.

Hata hivyo, Hamas imesema Arouri atazikwa leo Alhamisi katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Shatila iliyoko huko Beirut.