Hali yazidi kuwa tete vita vya Israel, Hamas

Muktasari:

  • Idadi ya vifo katika ukanda wa Gaza inakadiriwa kufikia 21,000 ndani ya siku 81 sasa tangu kuanza mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas.

Israel. Hali ni tete na matumaini yanafifia baada ya makadirio ya vifo katika ukanda wa Gaza kufikia 21,000 ndani ya siku 81 tangu kuanza mapigano ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas.  

Oktoba 7, mwaka huu kundi la Hamas lilifanya shambulizi la kushtukiza huko kusini mwa Israel, jambo lililosababisha  Israel kutangaza mashambulizi bila ukomo eneo la ukanda wa Gaza. 

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la kimataifa la Aljazeera, watu 20,915 wameuawa na 54,918 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel kwenye ukanda huo tangu Oktoba 7, 2023, huku  shambulio la Hamas dhidi ya Israel likiuawa watu 1,139 pekee.  

Wizara ya Afya ya Gaza jana ilisema watu 241 waliuawa na 382 kujeruhiwa ndani ya saa 24, huku Jeshi la Israel likithibitisha kushambulia kusini mwa ukanda huo. 

Vyombo vya habari vya Israel pia vimeripoti kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema vita havitakoma huku akihimiza Wapalestina kuondoka eneo la Gaza.

Juzi Netanyahu alinukuliwa katika vyombo vya habari akikiri vita dhidi yao na Hamas vinagharimu zaidi maisha kwa wanajeshi wake na mali, lakini wanalazimika kusonga mbele zaidi ili kulidhibiti kundi hilo.

Hata hivyo, Hamas pia imekataa pendekezo la kusitisha mapigano kwa muda, badala yake kusitishwa mapigano kwa njia ya suluhisho la kudumu ili kurudisha amani ya kudumu.

Kuna mashauriano mbalimbali yamefanyika na mengine yakiendelea kwa pande mbili kwa lengo la kuzuia mwendelezo wa mapigano hayo, lakini matumaini yanafifia.

Kwa mfano, pendekezo la Misri la kumaliza vita hiyo lingefanyika katika awamu kadhaa; kwanza ni kusitisha mapigano kwa angalau siku 14.

Pili, mateka 40 wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza wangeachiwa kwa kubadilishana na Wapalestina 120 walio jela nchini Israel.

Baada ya hapo, Israel ingelazimika kuyaondoa majeshi yake kutoka kwenye ardhi ya Palestina.

Lakini mpango huo ulioungwa mkono na Hamas umekwama na hivyo kuchochea hisia za Hamas kutangaza kutositisha mapigano hayo.